The House of Favourite Newspapers

Nabi Hataki Utani Ampeleka Gym Morrison kwa Ajili ya Kuwavaa Waganda Wiki ya Mwananchi

0
                       Kocha Mkuu wa Yanga, Mtunisia, Nasreddine Nabi

KATIKA kuhakikisha anaendana na kasi ya wenzake, Kocha Mkuu wa Yanga, Mtunisia, Nasreddine Nabi fasta amewapa program maalum ya gym mastaa wake wawili akiwemo Mghana, Bernard Morrison.

 

Hiyo ikiwa ni siku moja ipite tangu kiungo huyo mshambuliaji aingie kambini juzi Jumatatu jioni huko Kijiji cha Avic Town, Kigamboni nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

 

Staa mwingine aliyeingizwa gym ni beki wa kulia Mkongomani, Shaaban Djuma aliyerejea nchini juzi akitokea nyumbani kwao, DR Congo katika mapumziko.

 

Morrison baada ya kutua kambini kwa mara ya kwanza juzi, alikuta wenzake tayari wameshaanza lakini alipokelewa na shangwe kubwa la mashabiki waliokuwa nje ya uzio uwanjani hapo ambapo walimpigia makofi na kumshangilia.

 

Hii ni mara ya pili Morrison anarejea Yanga kwani awali aliitumikia timu hiyo mwaka 2020 na alidumu kwa miezi sita kabla ya kujiunga na Simba kwa miaka miwili.

 

Taarifa ambazo imezipata Championi Jumatano, licha ya Morrison na Djuma juzi Jumatatu kufanya mazoezi ya kimbinu pamoja na wenzao, lakini kocha ametoa maagizo ya mastaa hao kufanya mazoezi ya fitinesi gym.

 

Mtoa taarifa huyo alisema kuwa wachezaji wote walianza program za mazoezi kwa gym, hivyo kuhakikisha wanaendana na kasi ya wachezaji wenzao wataanzia huko kwanza.

 

Aliongeza kuwa mara baada ya gym, mastaa hao wote wawili haraka wataungana na wenzao leo Jumatano hadi Ijumaa kwa ajili ya mazoezi ya ufundi na kimbinu ili wawe tayari kwa ajili ya mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Vipers FC ya Uganda watakaocheza Wiki ya Mwananchi.

 

Kikosi chote kimekamilika kambini hapa Avic Town mara baada ya Morrison kuripoti jana (juzi) kujiunga na wenzao kujiandaa na msimu mpya. “Morrison alikuwa mchezaji pekee ambaye hajaripoti, Djuma yeye aliripoti kambini tangu Jumapili (wikiendi iliyopita) na kuanza mazoezi mepesi.

“Wachezaji hao wawili wameandaliwa program ya gym kwa ajili ya kuwaongezea fitinesi kwa siku moja ambayo ni leo (jana) Jumanne asubuhi na kesho (leo) Jumatano wataendelea na program nyingine na wachezaji wenzao.

“Program nyingine watakazozifanya za kimbinu na ufundi pekee tukielekea katika kilele cha Wiki ya Mwananchi ambako tutacheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Vipers ya Uganda,” alisema bosi huyo.

 

 

Leave A Reply