Nabi, Ntibazonkiza Wazinguana Yanga

WAKATI kikosi cha Yanga kikielekea Arusha kwa ajili ya kambi ya siku 10, imeelezwa kwamba, kocha mkuu wa timu hiyo, Nasreddine Nabi, amempiga chini straika wake, Saidi Ntibazonkiza ‘Saido’ na kumuondoa kwenye mipango yake.

 

Uamuzi wa Nabi umekuja kwa kile kilichoelezwa kwamba staa huyo wa Burundi alikwenda kinyume na matakwa ya kocha huyo.

Wakati Saido anapigwa chini, Nabi amekuwa akipewa jeuri na kiwango kikubwa kinachooneshwa na Feisal Salum ‘Fei Toto’ tangu kuanza kwa msimu huu.

 

Saido ambaye alijiunga na Yanga katika dirisha dogo la usajili msimu uliopita na kuteka hisia za mashabiki wengi wa timu hiyo, msimu huu mambo yamekuwa magumu kwake kwani hajacheza mechi hata moja ya Ligi Kuu Bara kati ya mbili ambazo Yanga imecheza.

 

Mbali na ligi kuu, Saido pia hakucheza mechi ya Ngao ya Jamii ambayo Yanga iliifunga Simba bao 1-0.

Mara ya mwisho kwa nyota huyo kuichezea Yanga msimu huu, ni katika mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Rivers United uliochezwa Uwanja wa Mkapa, Dar, wakati Yanga ikifungwa 1-0, huku akitokea benchi.

 

Chanzo kutoka ndani ya Klabu ya Yanga, kimeliambia Spoti Xtra, kuwa nyota huyo amekuwa akikosa nafasi katika kikosi cha Kocha Nabi kutokana na ishu ya nidhamu yake.

 

“Kitu ambacho wengi hawakijui sababu ya kukosekana kwa Saido ndani ya kikosi cha Kocha Nabi tangu kuanza kwa msimu huu, ambapo sababu kubwa ni nidhamu yake kutokuwa nzuri.

 

“Walipokuwepo makocha waliopita alikuwa na utovu wa nidhamu kwa maana ya kutaka kujionesha kuwa yeye ni mkubwa kuliko wachezaji wengine na hata benchi la ufundi.

 

“Kuna tukio la utovu wa nidhamu alilifanya msimu uliopita kipindi kocha alipokuwa Juma Mwambusi, alipokuja Nabi, alimuita, akaongea naye na kumtaka ajirekebishe.

 

“Lakini jambo hilo limeendelea kwake msimu huu kitu ambacho kimemkasirisha kocha na ndio maana kwa sasa Saido haonekani sana kwenye timu.

 

“Kocha anataka kuona kila mchezaji anatakiwa kuwa sawa na mwenzake na hakuna aliye juu kwamba akikosekana timu itafanya vibaya. Ukiangalia kwa sasa Saido hayupo na timu inapata matokeo mazuri” kilisema chanzo hicho.

 

Hivi karibuni, Nabi alizungumzia ishu ya kutompa nafasi kubwa Saido kwenye kikosi chake ambapo alisema: “Saido anacheza nafasi moja na Feisal, hivyo hata kama ungekuwa kocha utamuacha Fei Toto umwanzishe Saido?”

LEEN ESSAU, DAR2176
SWALI LA LEO

Kupanda Kwa Bei ya Mafuta Nchini, Nini Kifanyike Kupunguza Bei?
Toa comment