NABII BILIONEA MWANAMKE ATIKISA BONGO

NI kishindo cha aina yake! Nabii mwanamke, Dk Lucy Natasha ambaye ametinga Bongo kufanya huduma katika makanisa mbalimbali, ameibua gumzo mjini baada ya Wabongo kufahamu habari zake, Ijumaa Wikienda limekukusanyia habari kamili.

 

Dk Lucy ambaye ni mwanzilishi wa huduma ya kinabii ya Ministries International ya nchini Kenya, alitua Bongo wiki iliyopita ambapo mara baada ya kukanyaga Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar, watu walianza kumjadili kutokana na muonekano na mafanikio yake.

 

“Mh! Huyu nabii si mchezomchezo, angalia msafara wake ulivyo mkubwa, angalia ulinzi, magari yake na ninasikia huko kwao Kenya ni tajiri kwelikweli, anamiliki magari na majumba ya kifahari,” alieleza mmoja wa watu walioshuhudia ujio wake.

Ijumaa Wikienda lilijaribu kuzungumza na mmoja wa wenyeji wa mchungaji huyo ambaye hakupenda jina lake lichorwe gazetini ambaye alifunguka mambo mengi kuhusu huduma na utajiri wa nabii huyo. “Huyu nabii ni maarufu sana Kenya na nchi mbalimbali kama vile Afrika Kusini, Rwanda, Burundi na kwingineko duniani kwani anatoa hudumu katika nchi zaidi ya 50.

 

“Ana kipawa cha ajabu sana, alianza kuhubiri akiwa na umri wa miaka tisa akiwa shule ya msingi. Amekua hivyohivyo akihubiri na bahati nzuri mama yake pia alikuwa mchungaji, akasoma na kuhitimu masomo ya Biblia na sasa ni nabii.

 

GUMZO KILA KONA

“Amekuwa maarufu zaidi kupitia huduma zake anazofanya kwani anafanya kama semina katika nchi mbalimbali, anafundisha Biblia na anafundisha elimu ya maisha hivyo amekuwa akiwagusa wengi. Anapata mialiko mingi sana na ndiyo maana umeona amekuja pia nchini,” alisema.

MAISHA YAKE…

Mwenyeji wake huyo alizidi kumuelezea mchungaji huyo kuwa, mbali na umaarufu wake wa kuhubiri neno la Mungu, amekuwa maarufu pia kwa aina ya maisha yake anayoishi huku ukizingatia ni mrembo.

 

“Anavaa kisasa, ukimuona unaweza usidhanie kama ni nabii, anajiremba, anatupia tisheti na jinsi kama vile watu wa kawaida na bahati nzuri Mungu kamjalia umbo zuri la kuvutia.

MIKOKO KAMA YOTE

“Anamiliki magari ya kifahari kama yote ambayo yapo yenye jina lake la huduma analotumia Miracle kuanzia Oracle 1 hadi 7.

 

“Miongoni mwa magari hayo anayomiliki ni pamoja na Toyota Harrier Lexus, Toyota Fortuner, Mercedes Benz E Class, Toyota Land Cruiser V8, Range Rover Sport na mengine makali. Ukimuangalia jinsi alivyo simpo huwezi kumdhania kabisa kama ndiyo yeye mwenye mali kiasi hicho,” alisema.

 

ANAMILIKI NDEGE

Aidha, mwenyeji huyo alisema nabii Lucy pia anamiliki ndege yake binafsi, jambo ambalo linamfanya awe miongoni mwa wachungaji wachache Afrika Mashariki na Kati wanaomiliki usafiri huo wa angani.

IJUMAA WIKIENDA LAJIRIDHISHA

Ijumaa Wikienda lilijaribu kuchimba na kujiridhisha kupitia mitandao mbalimbali ya nchini Kenya ambayo iliripoti kuhusu nabii huyo kuwa na ukwasi si wa kitoto.

 

Mitandao tofauti ilimtaja kama miongoni mwa manabii ambao wamechipukia kwa kasi, lakini wana mafanikio makubwa kwa upande wa kiroho na kimwili. Mitandao ilionesha amekuwa akifanya mikutano mingi na video zake zikionesha umati mkubwa kila anapohubiri huku mafundisho yake yakiwagusa mno watu.

WAUMINI WAMZUNGUMZIA

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Gazeti la Ijumaa Wikienda, baadhi ya waumini waliohudhuria semina yake iliyofanyika katika Viwanja vya Tabata-Liwiti jijini Dar, walisema wameguswa na mafundisho yake na kwamba wanatamani afungue kanisa hapa nchini.

 

“Kwa kweli nimeguswa mno na mahubiri yake, anajua kuhubiri amenifanya nimgeukie Mungu kwa hiyari, anafundisha pia maisha ya kawaida kabisa ya kuishi na watu jambo ambalo wachungaji wengine hawafanyi, kwa kweli ikiwezekana afungue tu kanisa maana mimi habari zake nilizipata kwa jirani yangu, nilipofika kweli zile sifa alizonipa nikazikuta,” alisema John Abiod, mkazi wa Tandika, Dar.

 

Mbali na huyo, waumini wengine wengi walisema wamenufaika na uwepo wake nchini na kusema kwa jinsi alivyotikisa Bongo kwa siku kadhaa, wanatamani arudi tena na tena.

AZUNGUMZA NA IJUMAA WIKIENDA

Ijumaa Wikienda lilifanya jitihada ya kumsaka nabii huyo kabla hajaondoka nchini ambapo alipopatikana alifunguka kuhusu huduma yake sambamba na ukwasi alionao.

 

“Huduma hii ni maono ambayo nayapata kutoka kwa Mungu, mimi natumika kama daraja kufikisha kile ninachopewa. Namshukuru Mungu kuona huduma yangu inazidi kukua, ninazunguka kwenye nchi mbalimbali kama hivi nimekuja Tanzania na nchi nyingine.

 

KUHUSU MAGARI, NDEGE?

“Hayo kwangu si kitu, kikubwa ni huduma. Kumiliki hivyo vyote ni kwa neema ya Mungu na mimi kwa kweli siangalii sana kuhusu hivyo vitu, zaidi sana ni kuhakikisha nawafikishia watu wote ujumbe wa Mungu na furaha yangu ni kuona wanabadilika na mwisho wafike kwa Mungu,” alisema nabii huyo ambaye bado hajaolewa.

STORI:ERICK EVARIST, DAR


Loading...

Toa comment