The House of Favourite Newspapers

Naibu Waziri Chande Aipa Kongole Benki ya Mkombozi

0
NAIBU Waziri wa Fedha, Hamad Chande ameipongeza Benki ya Biashara ya Mkombozi,kuwa imepanda kutoka hatua moja kwenda nyingine ndani ya muda mfupi huku amewasihi watendaji wa Benki hiyo kutoridhika na hatua waliyofikia, badala yake waendelee kufanya uhamasishaji ili kuifanya Mkombozi Benki iendelee kukua.
Akizungumza Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Chande katika Hafla ya Mkombozi Benki kupandishwa Rasmi kutoka Soko la Ukuzaji Mitaji la DSE (EGM) na kwenda kwenye Soko Kuu la Uwekezaji (MIMS) iliyofanyika Kambarage House jijini Dar es Salaam.
“Hongereni sana Mkombozi Bank kwa hatua hii mliyofikia, kwa sababu mmepanda hadhi kutoka hatua moja kwenda nyingine ndani ya muda mfupi sana. Lakini niwaombe, msiridhike na hatua hiyo mliyoifikia, kwa sababu kuna maneno yanasema ‘Mpanda patosha, huvuna pa mkwisha.”
“Endeleeni kuhamasisha ili Bank hii ya Mkombozi iendelee kukua. Kwa hiyo naomba kutangaza rasmi kwamba Mkombozi Bank imepandishwa rasmi kutoka Soko la Ujasiriamali (EGM) na kuingizwa Katika Soko Kuu la Uwekezaji (MIMs),” amesema Naibu Waziri.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Mkombozi, Respige Kimati amesema kuwa Benki hiyo imewekeza nguvu nyingi ili kuanza kutoa gawio kwanzia mwakani 2025, kuwa Benki hiyo imekuwa mstari wa mbele kuungana na Serikali katika kuwashika mkono watu waliopatwa na majanga mbalimbali ndani ya jamii.
“Tumeshuhudia ukuaji mkubwa wa faida, ongezeko la amana za wateja, ongezeko la mikopo iliyotolewa kwa watanzania hasa sekta binafsi, kupanuka kwa mtandao wetu wa matawi na uwekezaji mzuri katika huduma za benki kwa njia ya Mtandao, hususani uanzishwaji na usambazaji wa huduma za Benki kwa njia wa Mawakala”. amesema Kimati
Aidha, Kimati amesema Malengo ya benki hiyo ni kumkomboa Mtanzania katika wimbi la umasikini kwa kutoa huduma za kibenki hasa mikopo midogo midogo kwa watu binafsi wakiwemo vijana na wanawake na mikopo ya kati na mikubwa kwa makampuni, taasisi za huduma na wafanyabiashara wa kati na wadogo.
Hivyo, hatua hii mpya ya kuwa sehemu ya Soko Kuu la Uwekezaji (MIMS) katika Soko la Hisa la Dar es Salaam, tunayo imani kubwa kwamba mafanikio zaidi yanakuja mbele yetu, tunahitaji kuendelea kupata msaada wenu wa dhati na tunawaomba washirika wetu, wateja wetu, wanahisa, mamlaka mbalimbali za usimamizi wa sekta ya fedha nchini na watunga sera kuendelea kutuunga mkono katika safari hii ili Msaada wenu ni muhimu sana katika kuhakikisha tunatimiza malengo yetu ya muda mrefu na kuboresha huduma zetu kwa wateja wetu.
Leave A Reply