Wiki iliyopita tuliwaletea maswali na majibu ya Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Khamisi Kigwangalla ambapo alieleza mengi. Leo anazidi kufafanua mambo mbalimbali, fuatana nasi:
Hivi sasa kuna shida ya upatikanaji wa dawa hasa katika zahanati vijijini na mijini, wizara ina mpango gani wa kuhakikisha dawa zinapatikana?
Jibu: Serikali ina mpango mzuri kuhakikisha vituo vya afya vijijini na zahanati zinapata dawa, chanzo cha kupatikana dawa ni wateja wao kuchangia au kwa kuchangia mfuko wa jamii na halmashauri. Tumekuja na suluhisho la kutaka wananchi waingie mfuko wa jamii wa afya au bima ya afya.
Tunaboresha huduma hiyo kwani kadi ya afya itakuwa na uwezo wa kutumika hadi kwenye hospitali ya mkoa. Tunataka kila mtu achangie huduma hii ili mfuko wa afya ukue na asilimia 67 za fedha ziingie kwenye bajeti ya dawa, hivyo dawa zitakuwepo tu. Tumegundua dawa hizi, baadhi ya watendaji vijijini wanaiba au kugawana. Niwaonye, tukiwakamata tutawapeleka mahakamani.
Mpango mpya ni kwamba dawa zote za serikali zitakuwa na logo ya serikali, rangi maalum na asilimia 5 ya mapato watapewa Kamati ya Afya ya Kijiji ili kuwapa motisha wa kuzisimamia.
Kamati itatakiwa kubandika kwenye ubao wa matangazo taarifa ya dawa zilizoingia na zikiisha wabandike tena kwenye ubao huohuo wananchi wajue njinsi dawa zilivyotumika.
Kuna ishu ya vipodozi feki hasa kwa wanawake maarufu kwa jina la ‘Mchina’ ambayo inashika kasi mjini na vina madhara kwenye miili yao, wizara inafanya nini kukomesha uingizaji wa vipodozi hivyo?
Jibu: Ili kuingiza vipodozi ni lazima kusajiliwa. Ni kosa kutosajili vipodozi, vinasajiliwa na TFDA (Mamlaka ya Chakula na Dawa). Kabla ya kusajiliwa lazima vikaguliwe na TBS (Shirika la Viwango Tanzania), TFDA na Mkemia Mkuu wa Serikali. Watakaokutwa na vipodozi visivyosajiliwa na kuwa na vibali, watakamatwa na watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Sasa tugeukie suala la matabibu wa tiba asili, wizara ina utaratibu gani wa matabibu hawa kujitangaza?
JIBU: Upo utaratibu wa kujitangaza. Awali tulizuia matangazo yao lakini Waziri wa Afya (Ummy Mwalimu) ametoa miezi mitatu waendelee kutangaza kibinadamu kwa kujua kuwa kuna wengine wana mikataba katika vyombo vya habari wanavyotangaza.
Kwani baada ya miezi mitatu hawatakuwa wanajitangaza?
JIBU: Hapana. Itatakiwa wafuate utaratibu. Tabibu ili atangaze dawa zake au biashara yake, atatakiwa apeleke tangazo lake kwenye Baraza la Tiba Asili ili lihakikiwe kwanza kabla ya kutangaza. Tumefanya hivyo kuzuia watu wasio na ujuzi kufanya kazi za kidaktari kwa mfano, kuna wengine walikuwa na tabia za kuwaingiza vidole watu sehemu nyeti huku wakijua kuwa hawana ujuzi wa kutambua magonjwa kwa njia hiyo. Kwanza huo ni udhalilishaji.
Kuna utaratibu gani unaotakiwa kufuata ili tabibu wa tiba mbadala dawa yake iweze kusajiliwa na serikali?
JIBU: Ili dawa isajiliwe, utaratibu wa sasa ni kwamba mpaka ziende maabara, TBS, kwa Mkemia Mkuu wa Serikali na TFDA kufanyiwa utafiti.
Nini mikakati yako kuhusiana na changamoto mbalimbali jimboni kwako za kuwaletea maendeleo wapiga kura wako?
JIBU: Nina mikakati mingi ya kuwawezesha kiuchumi wapiga kura wangu. Tunataka kutengeneza vikundi mbalimbali kama vile vya kuzikana, kukausha mbogamboga, vikundi vya miradi kama vile vya bodaboda na tunawagawia pikipiki kwa awamu ili wajiajiri, vikundi vya kukamua alizeti ili wauze mafuta, mradi wa pamba ili wawe na zao la biashara. Wanawake tunawaangalia zaidi kwa sababu wakiwa na kipato hawanyanyasiki.
Tunatarajia kujenga shule tano za High School (kidato cha tano na sita), katika hilo bado shule tatu, mbili zipo tayari na nitazindua.Tunaboresha kiwango cha elimu, tumepata walimu wengi na tutawapelekea huduma za intaneti na mitandao ya simu huko vijijini pamoja na watumishi wa afya ili kuwapa motisha ya kuwahudumia wapiga kura wangu. Tutajenga kambi kwa ajili ya wanafunzi wanaofanya mitihani kwa mwaka husika lakini pia tutaboresha vituo vitano vya afya, kimoja tutahakikisha kinakuwa na chumba cha upasuaji.
Vipi kuhusu changamoto ya barabara, umeme na maji katika jimbo lako?
JIBU: Hizo zipo. Tutaboresha barabara za vijijini, tutaweka makalavati sehemu korofi. Tutahakikisha vijiji vinapata umeme wa uhakika. Kuhusu maji tutachimba visima, asilimia 65 tumechimba kwa fedha zangu na wafadhili na halmashauri bado tutawaomba wafadhili wengine kutusaidia kutanzua tatizo hili.
Asante kwa ushirikiano wako.
KUNUNUA NA KUSOMA MAGAZETI YA GLOBAL PUBLISHERS ONLINE, INGIA HAPA==>VODACOM M-PAPER APP
*********
JIUNGE NA SOCIAL MEDIA ZETU:
KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA
INSTAGRAM: @Globalpublishers
ERIC SHIGONGO INSTAGRAM: @ericshigongo
TWITTER: @GlobalHabari
FACEBOOK: @GlobalPublishers
SUBSCRIBE YOU TUBE: GlobalPublishers
GLOBAL TV ONLINE: www.globaltvtz.com
HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, ERIC SHIGONGO FACEBOOK PAGE: @shigongotz