Naibu Waziri Ndejembi Apamba Uzinduzi wa Strategis Insurance Dodoma

Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deogratius Ndejembi (wa pili kushoto) na Naibu Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania, Khadija Saidi wakifunua pazia ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa Tawi la Kampuni Binafsi ya Bima ya Strategis jijini Dodoma. Kushoto ni Afisa Mtendaji Mkuu (Mali), Jabir Kigoda na kutoka kulia ni Afisa Mtendaji Mkuu (Bima ya Afya), Dk Malav Manek na Afisa Mtendaji Mkuu Kiongozi,Dk. Flora Minja.

 

Moja ya makampuni binafsi ya bima yanayoongoza nchini, Strategis Insurance, imezindua rasmi tawi la Dodoma katika jitihada za kujitanua zaidi na kusambaza huduma zake Tanzania.

 

Akizindua tawi hilo jipya, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais-Utumishi na Utawala Bora Mh. Deogratius  Ndejembi alisema amefurahishwa na hatua kubwa iliyofikiwa na kampuni hiyo ambayo mwaka huu inatimiza miaka 20 tangu ianze kutoa huduma za bima nchini.

 

“Kama tunavyofahamu Dodoma ndio makao makuu ya nchi yetu sasa na tayari serikali imeshahamia jijini hapa kwa ukamilifu. Inapendeza kuona mashirika kama Strategis yanaunga mkono juhudi hizi za Serikali ,” alisema Mh.Ndejembi.

 

Vilevile, aliipongeza Kampuni ya Strategis kwa kuwa kampuni ya pili kwa ukubwa nchini katika kampuni binafsi zinazotoa huduma za bima za mali na ajali na ya kwanza katika bima ya afya.  “Munastahili kuigwa kwa namna yoyote kwa sababu ya utendaji wenu lakini pia ubora wa huduma zenu,” alisema.

 

Alisema kampuni hiyo inastahili pongezi kwa kuhakikisha madai ya wateja yanashugulikiwa ndani ya muda mfupi kama wanavyohitaji wateja huku akitoa wito kwa makampuni mengine ya bima yaige mfano huo.

 

Naibu waziri huyo pia alisema  hatua ya sasa ya Strategis kujikita katika bima za mali na ajali ili kuwafikia watanzania wengi zaidi ni nzuri na kutoa wito kwa watanzania wajenge utamaduni wa kukata bima na sio kusubiri wakati wa majanga tu.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deogratius Ndejembi akiwa katika picha ya pamoja.

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Bima ya Strategis, Dk. Flora Minja alisema wanayo kila sababu ya kujivunia kuhusu kukua kwao katika zaidi ya miaka 20 ya biashara ya bima na ndio maana wameona umuhimu wa kufungua matawi zaidi ili kuwafikia watanzania wengi kwa haraka zaidi.

“Kwa sasa tupo Dar es Salaam, Mwanza, Zanzibar, Arusha na sasa Dodoma,” alisema na kuongeza tawi jipya la Dodoma pia litatumika kuwafikia wateja walioko mikoa ya jirani kwani Dodoma panafikika kwa urahisi lakini pia wataendelea kufungua matawi mengine katika siku za usoni kulingana na mahitaji.

 

Alisema kampuni hiyo itaendelea kuwekeza zaidi katika teknolojia ili kuongeza ufanisi katika utendaji hasa katika kushugulikia madai ya wateja ili waweze kuhudumiwa kwa muda mfupi zaidi iwezekanavyo.

 

Alisema hapo awali walijikita sana katika bima ya afya  lakini kwa takribani miaka minne sasa wamepanua wigo wao na kutoa bima za mali na ajali.  “Bima hizi zinajumuisha bima za magari, biashara, uhandisi, kazi, usafirishaji mizigo nchi kavu na majini, bima za safari, moto, wizi, fedha na nyinginezo,”

 

Alisema kwa mwaka uliopita, ukuaji wa kitengo cha bima za mali na ajali ulifikia asilimia 70% na kwa ujumla kampuni ilikua kwa takribani asilimia 20.  “Na hivyo leo ninayo furaha kuwashirikisha kwamba kwa sasa, tunashika nafasi ya pili kwa ukubwa kati ya makampuni yote ya binafsi ya bima nchini,” alisema.

 

Hafla hiyo yenye kufana pia ilihudhuriwa na Naibu Kamishna wa Bima Khadija Issa Said, uongozi wa kampuni hiyo na wadau wengine wa bima wakiwemo wateja.

Kampuni ya Bima ya Strategis ni moja ya kampuni kongwe za binafsi za bima nchini ambayo ilianza shughuli zake mwaka 2002 huku ikiendelea kujitanua mwaka hadi mwaka kwa lengo la kutoa bima za uhakika na zenye bei nafuu kwa wateja wake.2173
SWALI LA LEO

Kupanda Kwa Bei ya Mafuta Nchini, Nini Kifanyike Kupunguza Bei?
Toa comment