The House of Favourite Newspapers

Najua zilikokwenda zile kontena

Yaani we acha tu. Nimekaa hapa nafikiria wapi zilikopotelea kontena mia tatu arobaini na tisa.

Inahitaji akili sana kupoteza kontena zote hizo. Lakini mimi kama mimi, nina mawazo ya kusaidia kujua wapi kontena hizi zimekwenda, uzalendo ni kitu muhimu sana na mimi ni mzalendo, lazima nisaidie kuishauri dola ili mali hii ijulikane ilikwenda wapi.

Wote tunaelewa kuwa Wabongo wengi ni wajasiriamali wa hali ya juu na kila mara wakipata fursa huzitumia haraka sana.

Mimi nadhani ili kuzipata kontena zile japo chache, vyombo husika viwakamate wajasiriamali ambao hutengeneza vifaa vya bati. Nimewaza kwa kutumia akili ya hali ya juu na kugundua kuwa inawezekana kontena zile zilikatwakatwa zikatengenezwa makarai, ndoo au hata pengine masufuria makubwa ambayo hupikiwa pilau kwenye masherehe.

Hivyo haraka sana sufuria kubwa zote nchini zikamatwe na zipimwe ili kuona kama bati zilizotumika kutengeneza sufuria hizo siyo aina ile ya zile kontena. Ikiwa hili limepita bila kupata ushahidi, makarai na ndoo zote za chuma pia zikusanywe nchi nzima na kupimwa pia.

Kuna uwezekano mkubwa sana wa kupata ushahidi wapi kontena mia tatu arobaini zilikopotelea. Ni vizuri hawa wanaotengeneza koroboi pia wakapelelezwa wapi walikopata bati za kutengenezea koroboi zao, hivyo wananchi wote wenye koroboi wazipeleke kwenye ofisi zao za serikali za mitaa, huko zisajiliwe na kupelekwa wilayani ambako wataalam wazipime ili kupata uhakika wa uhalali wa koroboi hizo.

Inawezekana tunahangaika kumbe kontena zimetengenezwa vibatari. Katika msako huu ni muhimu kuwakusanya hawa wanaopita mtaani na kununua chuma chakavu, hawa wanawezekana sana walinunua kontena hizi na kuziuza kama chuma chakavu, hivyo nao vyombo husika viwakusanye wote na kuwahoji.

Mimi kama mzalendo wa nchi hii nimeona nitoe ushauri huu uliotukuka ili kusaidia katika harakati za kujua wapi zilikopotelea kontena mia tatu arobaini na tisa.

Kama ushauri wangu utasababisha mafanikio katika kutatua kitendawili hiki naomba nisisahaulike kwenye kupewa zawadi ya mwananchi bora wa mwaka. Wasalaam!

Comments are closed.