The House of Favourite Newspapers

Namba tisa yawapasua kichwa Yanga

0

Ngoma-3.jpg
Wilbert Molandi,
Dar es Salaam

BENCHI la ufundi la Yanga chini ya Mholanzi, Hans van Der Pluijm lipo kwenye mikakati ya kuimarisha kikosi chao na limepanga kusajili straika hatari zaidi ya Malimi Busungu kwenye usajili wa dirisha dogo msimu huu wa Ligi Kuu Bara.

Usajili huo wanaoufanya timu hiyo ni katika kuhakikisha safu hiyo ya ushambuliaji inakuwa tishio katika kuelekea ligi kuu na Ligi ya Mabingwa Afrika (Caf).

Miongoni mwa wachezaji wanaotajwa kufanya mazungumzo ya awali na Yanga ni Mnigeria, Abasirim Chidiebere  anayeichezea Coastal Union kwa ajili ya kuiongezea mkali safu hiyo ya ushambuliaji inayoongozwa na Mzimbabwe, Donald Ngoma, Amissi Tambwe na Malimi Busungu.

Kwa mujibu wa chanzo cha habari kutoka ndani ya uongozi wa timu hiyo, kitendo cha kocha wa timu hiyo kumhamishia Busungu winga namba 11, ndicho kimesababisha benchi la ufundi kupendekeza straika mwingine mwenye uwezo zaidi ya Busungu.

Kilisema kuwa, kocha wa timu hiyo hivi sasa hamtumii Busungu kucheza nafasi ya ushambuliaji namba 9 au 10, kama walivyomsajili kwenye msimu huu wa ligi kuu na badala yake wanamtumia 11, baada ya kuona kocha hana winga zaidi yake.

Kiliongeza kuwa, hivyo viongozi wamependekeza kumsajili mshambuliaji mwingine atakayekuwa mbadala wa Ngoma na Tambwe kwenye usajili wa msimu huu katika kukiimarisha kikosi chao kwenye usajili wa dirisha dogo.

“Kamati ya Utendaji ya Yanga hivi sasa ipo kwenye mipango ya kumuongeza mshambuliaji mwingine mwenye uwezo wa kufunga mabao zaidi ya Busungu katika usajili wa dirisha dogo.

“Hiyo ni baada ya kocha kumbadilisha namba Busungu kutoka namba 9 na 10 zinazochezwa na Ngoma, Tambwe na kumhamishia winga namba 11 katika kikosi chake cha kwanza.

“Hivyo kocha amependekeza kumsajili mshambuliaji mwingine mwenye uwezo zaidi ya Busungu katika usajili wa dirisha dogo, hivyo viongozi wapo kwenye mazungumzo na baadhi ya wachezaji watakaowasajili,” kilisema chanzo hicho.

Alipotafutwa Pluijm kuzungumzia hilo alisema: “Siwezi kuzungumzia usajili katika kipindi hiki, samahani kwa hilo, sasa hivi nipo mapumzikoni na familia yangu.”

Leave A Reply