Namibia; Rais, Makamu Wa Rais Wanawake
Rais mpya wa Namibia Netumbo Nandi-Ndaitwah ametangaza baraza lake la mawaziri la kwanza na kumteua Lucia Witbooi kuwa Makamu wa Rais wa kwanza mwanamke wa taifa hilo.
Kwa hatua yake hiyo, Rais Nandi-Ndaitwah ameifanya Namibia kuwa nchi ya kwanza na pekee barani Afrika yenye rais mwanamke na makamu wa rais pia mwanamke.
Nandi-Ndaitwah amewaapisha mawaziri 14, wanane kati yao wakiwa wanawake, pamoja na manaibu saba katika hafla iliyofanyika kwenye Ikulu ya mji mkuu, Windhoek.
“Sina shaka kwamba tutatekeleza kile ambacho watu wa Namibia wameagiza kifanywe”, amesema rais huyo mpya katika hafla hiyo. Rais Nandi-Ndaitwah ameongeza kuwa wizara za serikali yake mpya zinatakiwa zipange programu zinazolenga kutokomeza umaskini nchini humo.
“Kazi za watu waliotengwa kwa kutoshughulikiwa na za masuala ya ulemavu zitawekwa katika ofisi ya makamu wa rais ili kupata uangalizi wanaohitaji,” ameeleza rais mpya wa Namibia huku akiwaomba wananchi walipatie Baraza lake la Mawaziri fursa ya kutosha ya kutekeleza majukumu yake.
Wateule wengine wakuu katika serikali mpya ya Namibia ni Elijah Ngurare aliyeteuliwa kuwa waziri mkuu na Selma Ashipala-Musavyi aliyekabidhiwa wizara ya uhusiano wa kimataifa na biashara.