Namna Bora ya Wapendanao Kusherehekea Sikukuu

couple-wapendanao-mahabaWENGI bado wana dhana kwamba sikukuu ni kusherehekea kwa kunywa, kula. Wapo ambao bado wanaamini sikukuu huwa haikamiliki bila kupiga muziki mzito wenye kiwango cha kushindana au kuwazidi majirani wanaowazunguka.

Kuna wengine bado wana ile dhana kwamba siku ya sikukuu, ndiyo siku ya kuonesha kufuru ya kutumia hela. Kuonesha kwamba pochi yake imetuna kiasi gani. Bahati mbaya sana watu wa aina hiyo hujikuta katika maumivu makali pindi mwaka unapoanza.

Kama ana familia, inahitaji matumizi  ya watoto shule nakadhalika. Kesho ndiyo Krismasi. Wapendanao wana nafasi yao katika kuisherehekea sikukuu hiyo, baada ya hapo wanajiandaa kwa sikukuu nyingine, Mwaka Mpya. Kwa kifupi huu ni msimu wa sikukuu.

Kwa wapendanao, wakiitazama sikukuu kwa jicho la tatu, watabaini kwamba hayo yote niliyotangulia kuyataja hapo juu, hayana ulazima sana.

Huyachukulia kama ni kitu cha ziada, watayadhibiti ili sikukuu zikiisha wasiwe na maumivu makali na kujikuta wakianza kuhaha namna ya kuishi.

Yawezekana wewe na mwenzi wako mmeshasherehekea sikukuu nyingi lakini pengine haikuwa katika namna bora, ni vizuri kujifunza na kuifanya iwe na tija katika ustawi mzima wa penzi lenu. Namna bora ni ipi? Twende pamoja katika mada hii, utanielewa!

Kusherehekea sikukuu kwa wapendanao, kuna zaidi ya zawadi. Kuna zaidi ya kuoneshana upendo. Ni zaidi ya kutumiana maua au picha mbalimbali zinazoashiria upendo. Mtasherekeaje? Sherehekeeni huku mkitafakari mustakabali wa uhusiano wenu.

Uhusiano wenu ni wa aina gani? Je, mlikuwa gizani kwa muda gani? Yawezekana katika kipindi chote cha mwaka mzima, mlikuwa hamjadili mipango endelevu ya penzi lenu.

Mlikuwa mnaishiishi tu. Uhusiano usiokuwa na macho, bora liende.

Mwenzako akiamka asubuhi atakusalimia, ukiwahi wewe unafanya hivyo.

 Hakuna kitu cha ziada kinachowafikirisha katika safari yenu.

Mna ratiba ambayo Wazungu wanasema fixed. Yaani haina mabadiliko, kusalimiana asubuhi na kutakiana usiku mwema jioni.

Hampati hata muda wa dakika kumi au kumi na tano kujadili ‘future’ yenu. Nyinyi mnawaza mtakutana, mtatimiza haja ya matamanio yenu na baada ya hapo kila mtu anachukua hamsini zake. Hilo ni tatizo.

Kwenye kipindi hiki cha sikukuu za kuumaliza mwaka mnapaswa kufanya kitu cha ziada.

Tumieni Krismasi na Mwaka Mpya kwa kutenga muda mzuri katika eneo fulani ambalo mtaona linafaa. Hakuna sababu ya kutafuta eneo la gharama kubwa,  mnaweza kwenda ufukweni, eneo ambalo halina gharama kubwa hususan kama kipato chenu hakiruhusu, mkapata utulivu wa kujadili.

Mnaweza pia kwenda hotelini. Mnaweza kwenda kwenye mgahawa mkapata chakula cha mchana au cha jioni, kulingana na uwezo wenu. Msilazimishe kutumia gharama kubwa ambazo baadaye mtakuja zijutia.

Kulingana na kipato chenu, nendeni sehemu inayowafaa. Jadilianeni kuhusu mustakabali wenu wa baadaye. Kama bado hamjaingia kwenye ndoa, wekeni mikakati ya kufanya hivyo. Mpange je ni mwakani? Au mnafikiri ni baada ya miaka mingapi mtakuwa tayari kuoana rasmi?

Msioneane haya. Ulizaneni mpate majibu. Mnaishi kwenye penzi la giza mpaka lini? Nini mfanye ili kuweza kujikwamua? Mikakati gani muiweke? Kwa muda gani mtakuwa mmeweza kufanikisha jambo hilo?

Kwa hilo na mafanikio yenu yote kwa ujumla yanahitaji fedha, mna vyanzo vizuri vya mapato?

Kama hamna, nini mfanye ili muweze kufikia malengo yenu? Kama ni biashara, jadilini mfanye biashara gani? Mtapata wapi mtaji na mambo mengine kama hayo. Kama mlipanga hivyo mwaka uliopita na mkashindwa kutimiza malengo, ni wakati wa kujifunza kupitia kile kilichowakwamisha ili msije kukwama tena.

Suala la kujitathimini haliishii kwa wale ambao hawajaingia kwenye ndoa, hata wale ambao wamo, nao wanapaswa kutathimini safari yao. Kutazama wapi  walikosea ili katika mwaka unaokuja waweze kupiga hatua zaidi kimaisha.

Tumia hii nguvu ya ziada

Hakuna nguvu kubwa kama kusali. Baada ya kuweka mikakati yenu ya kibinadamu, mshirikisheni Mungu kupitia maombi. Sala ndio kila kitu. Kila hatua mnayoipiga, ishini katika matakwa ya Mungu, muombeni Yeye, atawafanyia wepesi katika kutimiza malengo yenu.

Bongo Movie Watoa Damu Hospital ya Mwananyamara

 


Loading...

Toa comment