The House of Favourite Newspapers

Namna ya kugundua, kuepuka utumwa wa Mapenzi

MUNGU yu mwema, kwa uwezo wake tunakutana tena leo hapa kwenye ukurasa wetu ambao tunajifunza kuhusu uhusiano na mapenzi. Naamini ukurasa huu umekuwa na faida kwako, bila shaka ukibadilisha fikra zako kuhusu mahusiano na kukujengea uhusiano imara wenye dira mbele yako.

Leo tunahitimisha mada yetu iliyoanza wiki mbili zilizopita, tukiangalia zaidi utumwa wa mapenzi na namna ya kuuepuka. Hebu sasa twende tukamalizie vipengele vilivyosalia. Je, vipi ikiwa wazazi wako wanakulazimisha kuingia kwenye ndoa na mtu ambaye hujamkubali moyoni mwako? Tuliona kidogo wiki iliyopita, sasa tuendelee kuona hatua unazopaswa kuchukua.

ZUNGUMZA NA WAZEE WAKO

Ikiwa wewe unayesoma mada hii wazazi wako wanakulazimisha kufunga ndoa na mpenzi ambaye siyo chaguo lako, usikubali kabisa! Zungumza na wazee taratibu, wape hisia zako. Kama haupo tayari kuoa/kuolewa kwa sasa waambie, lakini pia kama una mpenzi mwingine ambaye unampenda waeleze na ikiwezekana wakutanishe naye.

Siku zote ukweli ni silaha ya mwisho, hata kama unauma, kueleza ukweli wako utawavunja nguvu wazee wako kuendelea kukung’ang’anizia mahali ambapo hujapenda.

Ikiwa watamkataa mpenzi wako, waambie wakupe sababu za msingi, kama ni kweli zitakuwa za maana, kubali kuachana naye lakini wakati huo ukisubiri mwingine utakayempenda kwa dhati. Kamwe usikubali kuishi na mpenzi ambaye huna mapenzi naye.

TOA HISIA ZAKO

Pamoja na kwamba mapenzi yanauma hasa mmoja anapokuwa amezama katika bahari ya mapenzi kwa mwenzake, ni vizuri kukaa chini na huyo ambaye anataka kufunga ndoa na wewe na umweleze unavyojisikia.

Zungumza naye kwa upole huku ukizingatia kiwango cha juu cha ustaarabu, mwambie huhitaji ndoa kwa muda huo (hasa na yeye) lakini hakikisha humfanyi ajisikie vibaya, kumnyanyampaa au kumwonyesha aina yeyote ya dharau.

Mweleze kwa uhuru huku ukimpa nafasi aeleze hisia zake. Kama ni muungwana atakuelewa, lakini kama hataonyesha kukuelewa, kipengele kinachofuata ni muafaka sana kwako.

TAFUTA MSAADA

Hapa itakusaidia kwa pande zote mbili, yaani kwa wazazi wako na upande wa pili ni kwa huyo ‘mchumba hewa’ wako. Kikubwa unachotakiwa kufanya hapa ni kutafuta msaada zaidi kwa watu wa nje!

Ikiwa wazazi wako hawakukuelewa na hata huyo anayetarajia kukuoa, zungumza na wazee wanaoheshimiana na wazazi wako au mshenga wa mhusika!

Waeleze ukweli, kwamba kitakachokuja kutokea siyo ndoa badala yake ni matatizo. Hutakiwi kuonyesha woga wala aibu katika kutetea masilahi ya penzi lako.

Kuwa mkweli, muwazi na unatakiwa kuonyesha kweli hujafurahishwa na penzi hilo la kitumwa. Kwa vyovyote vile, hadi kufikia hatua hii, lazima wazazi/mwenza wako watakubaliana na wewe na kukuachia uhuru wa kuatafuta mwingine, haijalishi kama utakuwa umewakwaza, lakini angalau sasa utaishi kwa amani.

FURAHIA MAISHA

Kuingia katika ndoa ya kitumwa ni sawa na kukaribisha huzuni katika maisha yako yote, haipingiki kwamba mafanikio kwako itakuwa ni ndoto za mchana. Tafiti mbalimbali zinaonyesha kwamba wengi waliofanikiwa maishani baada ya ndoa, ni wale ambao wanaishi na wenzi wanaowapenda kwa mioyo yao.

Nyumba inapokuwa na upendo ni rahisi riziki kuingia, pia huachia mianya ya wanandoa kupanga mustakabali wa maisha yao, lakini kubwa zaidi ibilisi atapitia wapi katika familia yenye upendo?

Pumua kwa nguvu, furahia ushindi wako na uishi kwa amani ukisubiri yule ambaye ukimuona tu, moyo wako unabadilisha mapigo, siyo kwa sababu ya hasira bali penzi la dhati. Naamini umenisoma na kamwe hutakubali kuingia kwenye utumwa wa mapenzi.

Joseph Shaluwa ni mshauri wa maisha, uhusiano na ujasiriamali anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vingi, kikiwemo Maisha ya Ndoa kinachopatikana kwa oda. Kwa sasa anaandaa kitabu chake kipya cha SIRI ZA NDOA YENYE FURAHA kitakachotoka hivi karibuni.

Na Joseph Shaluwa  Simu 0718 400146

Comments are closed.