The House of Favourite Newspapers

Namna ya kukabili hasira kuepukana na madhara

0

KWENYE maisha kuna nyakati za kutofautiana na kukasirishana. Katika hali ya kawaida,  kipindi hiki huwa ni cha hatari kwa sababu husababisha madhara makubwa.
Sote tunajua, watu hupigana, huachana, hujeruhiana, hutukanana, hudhalilishana wakiwa na hasira. Hata hivyo, si wote wanaojua wafanye nini wanapojikuta wameingia kwenye hatua hiyo mbaya.
Msomaji wangu, hebu jaribu kukumbuka ugomvi mmoja uliotokea kati yako na rafiki au ndugu yako wa karibu.  Ikiwezekana jikumbushe mlivyoanza!  Utabaini kuwa mlianza kama utani na mkajikuta mmefura kwa hasira, mkatwangana makonde, mkatamkiana maneno makali ya kuudhi.
Yote hii ni kwa sababu mlikosa elimu ya mazungumzo. Ingekuwa mmoja wenu hasa yule aliyekuwa wa pili kukasirika anafahamu hatua za kuzungumza na mtu aliyekasirika, angechukua jukumu la kutuliza machafuko na kuleta amani.  Katika somo hili nakuletea  hatua tano za kuzungumza na mtu aliyekasirika.

MPUNGUZE MHEMKO

Hasira hujaza kifua, huathiri mzunguko wa damu na ufahamu. Mtu aliyekasirika  huwa vigumu kwake  kusikiliza au kutazama mambo kwa jicho la tatu. Mwenye hasira huwa hafikirii matokeo yajayo, badala yake hutazama zaidi tukio na jinsi ya kupata ushindi iwe kwa maneno au kwa mapambano.
Katika hali ya namna hiyo, mtu mwingine akija na busara za kutaka kumgeuza harakaharaka hawezi kumuelewa. Muhimu hapo ni kuacha kumwandama, kujibizana naye, kumshawishi asikilize, badala yake mpe nafasi ya kusema atakavyo, abwate ajuavyo huku wewe ukimuitikia na kumkubalia lawama zake.  “Basi ndugu yangu, mwenye makosa ni mimi.” Kauli za aina hii zitampunguza hasira kwani atajiona mshindi.

MSOME SAIKOLOJIA YAKE

Tumia ufahamu wa kawaida kubaini endapo mwenye hasira amepunguza au bado? Zoezi hili linaweza likachukua muda mrefu au mfupi,  hii inatokana na mtu mwenyewe. Ukishabaini kuwa hasira za mtu zimepungua, hapo ndipo unapoweza kuchukua hatua ya kutafuta suluhu au kufafanua haki kati yenu.

MRUHUSU AKUJIBU

Pamoja na kumsoma kisaikojia na kumwambia kinagaubaga makosa yake, usimzuie kujitetea, mpe nafasi ya kuzungumzia kilichomkasirisha. “Unaona bado unanitukana, sasa naamini siku ile ulikuwa umedhamiria.” Usisiseme hivyo, mwache ajibu hoja hata kama atakuwa anakukandamiza na kuzidi kujijengea ushindi. Mvumilie aoshe ubongo wake.

EPUKA MALUMBANO

Asili ya wanadamu hupenda sana kuficha makosa yao ili wasionekane hawana akili. Watu wa namna hii unapowarejeshea mazungumzo  wanaweza kujikuta wanahamaki tena.
“Kwa hiyo ulikuwa unasemaje?…Nilifanya ndiyo… Wewe unaamuaje?” Mkifika kwenye alama hiyo usikubali kulumbana naye, mwache aseme halafu wewe ingia kwenye hatua ya tano.

MUOMBE MSAMAHA

Hata kama atakuwa yeye ndiye mwenye makosa na amekataa kukiri, usijali, chukua jukumu la kumuomba msamaha na kueleza tena nia yako ya mazungumzo ilikuwa ni kuelewana si kugombana. Kumbuka hata kama amekiri kosa, bado unatakiwa kumuomba radhi kwa kurejea yaliyopita. “Ndugu yangu inawezekana nikawa nimekuudhi kwa niliyosema, nakuomba sana tusameheane.”
Bila shaka kwa haya machache msomaji wangu utakuwa umejifunza na kuchukua hatua za kuzuia migogoro mikubwa inayotokana na hasira. Shime, binadamu kama ndugu hatuna budi kupendana na kuzishinda hasira zetu.

Leave A Reply