The House of Favourite Newspapers

Jinsi Ya Kumpata Mwenza Katika Dunia Iliyojaa Wajeruhiwa

ULIMWENGU wa sasa, wapendanao wengi wanaishi kwa machale. Ni staili ile ya mguu pande, mguu sawa. Kwamba ukimzingua, anakuzingua. Mwaga mboga amwage ugali. Hataki kuona inakula kwake kama vijana wa sasa wanavyosema.

Kila mtu ameshaumizwa. Anaishi kwa tahadhari kuhofia asije akaumizwa tena. Kila mtu ana historia na majeraha yake. Ukimwambia mwenzako akueleze maumivu yake aliyokutana nayo katika uhusiano, utabaini ya kwako kumbe ni madogo.

Mwanamke aliishi na mpenzi wake, akamdanganya kwamba atamuoa. Akaamini kwamba kweli ataolewa, akapata moyo kwamba yupo na mtu sahihi lakini mwisho wa siku akaambulia maumivu. Anagundua aliyemuamini kumbe alikuwa ni nyoka.

Ni mtu ambaye ana msururu wa wanaume. Kusaliti kwake siyo ishu. Ni mtu ambaye pengine alikuwa akiigiza maisha ambayo si yake. Hana mbele wala nyuma. Anamueleza, haelezeki. Haambiliki. Ni mtu ambaye alikubuhu kwa tabia fulani ambayo historia yake imemganda. Hawezi kubadilika.

Na pengine hakupaswa kumuamini katika kiwango ambacho yeye alimuamini. Bahati mbaya sana, hata akiachana na huyo si kwamba amemaliza. Ataanzisha uhusiano na mwingine, na mwingine tena bado anaambulia maumivu yaleyale.

Utofauti unakuwa mdogo tu kutoka kwa huyu kwenda kwa mwingine. Wanatofautiana visa tu lakini matukio ni kama yaleyale. Huyu anaanzia Z na kumalizia na A, mwingine anaanzia A anamalizia na Z. Huyu aliingia na gia ya kusema nitakuoa, mwenzake akaamini mwisho wa siku ndoa inayeyuka.

Mwingine aliingia kwa mbwembwe, akafikia hadi hatua ya kupeleka barua ya uchumba utadhani yupo ‘serious’ kumbe wapi. Mwizi tu, alitumia barua kama mbinu. Umeingia kingi, amekutumia alivyotaka, anaendelea zake mbele.

Mwanamke anabaki kuumia. Anateseka moyoni kwani hakutegemea. Alimuamini, kumbe mwenzake alikuwa na lake kichwani. Anabaki kutawaliwa na majeraha ya mapenzi. Kuna wakati anaweza asitamani kabisa kupenda, anajiona mwenye bahati mbaya.

Kinachofuatia hapo yeye ni kuishi kwa machale. Kila mwanaume anayemuona mbele yake anajua ndiyo walewale. Kichwa chake kimefungata matukio mengi ya wanaume walaghai wa mapenzi.

Hiyo haimtokei mwanamke pekee, mwanaume vivyo hivyo. Anakutana na mtu, anaanzisha naye uhusiano na kumkabidhi moyo wake. Anampenda kwelikweli. Anamgharamia kila kitu kulingana na uwezo wake.

Anamjali kupita maelezo. Hamuachi ateseke, anapambana kwa kila hali kuhakikisha mwenzake anafurahi lakini mwisho wa siku naye anaambulia maumivu.

Anajuta kuwekeza nguvu, akili na fedha. Anajuta kuweka upendo wake kwa mtu ambaye pengine hakustahili. Anabaini ni kunguru asiyefugika. Anapomueleza kuhusu kubadilika, mwenzake hugeuka mbogo. Hataki kubanwa maana maisha ya kubanwa hayawezi.

Na bahati mbaya sana mapenzi ni upofu. Alipokuwa anapenda, ilikuwa ni vigumu sana kubaini kwamba anadanganywa. Mwishoni anabaini ukweli, anateseka moyoni. Akihamia kwa mwingine, anakutana na maumivu ya aina hiyohiyo. Anakuwa sugu.

KATAA KUUSONONESHA MOYO

Baada ya kukutana na changamoto hizo, tulia. Usiuchoshe moyo wako kwa mawazo. Simama, japo moyo unauma lakini chagua kuwa huru. Usiteseke, amini kwamba unayo nafasi nyingine. Usijione kwamba huna bahati, chukulia kama ni changamoto katika safari ya kuelekea kwenye mafanikio.

USIWE NA PAPARA

Vuta subira. Usiwe na haraka katika kuanzisha uhusiano mpya. Changamoto ulizopitia, zikupe mwongozo mzuri wa kufanya uchaguzi sahihi. Hakuna uongo usioujua. Hivyo ni vyema kufanya tathimini ya muda mrefu hadi kufikia hatua ya kufanya maamuzi.

MSHIRIKISHE MUNGU

Kila jambo jema huwa linafanikiwa vizuri zaidi unapomtanguliza Mungu. Mwombe Mungu akupe mtu sahihi. Macho ya kibinadamu yanaweza kukupotosha lakini unaposimama kwake hakuna litakaloshindikana.

Utampata mwenza sahihi ambaye hatakuumiza na itafika wakati utasahau yote na kusema ‘kumbe yale yote yalikuwa ni mapito ya muda na sasa nimefika nilipokuwa nataka kufika.’ Tukutane wiki ijayo hapahapa!.

Comments are closed.