The House of Favourite Newspapers

Nangasu Warema: Watanzania Wautangaze Utalii wa Nchi Yao

0

BALOZI wa utalii Tanzania, Nangasu Warema, amewataka Watanzania wa makundi yote kuutangaza utajiri mkubwa wa utalii nchini mwao ili kuinufaisha kutokana na mapato yatokanayo na sekta hiyo na kuiwezesha nchi kusonga mbele katika kuwaletea maendeleo.

 

Warema ameyasema hayo leo Desemba 3, 2020, wakati akihojiwa kwenye kipindi cha Front Page kinachoruka kupitia +255 Global Radio iliyoko Sinza-Mori jijini Dar es Salaam, ambayo inamilikiwa na kampuni ya Global Group.

 

 

Balozi huyo alisema ni muhimu zaidi kwa Watanzania kufanya hivyo sasa hususan kufuatia kupungua kwa shughuli za utalii kutokana na janga la ugonjwa wa Covid-19 ambao umeikumbadunia kwa kipindi cha karibu mwaka mzima sasa.

 

“Watanzania tujifunze kuwa wazalendo kwa kuitangaza nchi yetu katika sekta ya utalii na utajiri mwingine wa nchi yetu kwa ajili yetu,” alisema Warema akisisitiza kwamba pamojana kuzunguka kwake nchi mbalimbali duniani, bado anaamini Tanzania inaongoza katika utajiri wa utalii wa vitu vya asili.

 

“Nimezunguka karibu kila mara, nimeona uzuri wa nchi nyingi, lakini siwezi kukaa mbali na Tanzania,” alisisitiza kauli yake kuhusu utajiri ilio nao Tanzania katika sekta  ya utalii.

 

Akifafanua, amesema wakati umefika wa kubuni na kuimarisha vivutio mbalimbali vya utalii wa asili ikiwa ni pamoja na kuviweka katika miji mikubwa kama Dar es Salaam ambapo watalii wanaweza kuviona badala ya kuifanya miji kadhaa kuwa vituo vya kuteremkia tu katika safari zao na baadaye kupelekwa katika miji mingine nchini.

 

“Mji kama Dar es Salaam unatakiwa kuwa na vivutio vya kitalii ambavyo vitawafanya watalii wavione hapa, badala ya wao kufika hapa na kuondoka na kupelekwa sehemu nyingine,” alisema.

 

Aligusia kile kilichopangwa kama Dar es Salaam Tour ambacho kingelifanya jiji hilo kuwa na vivutio vyake kama vile Kijiji na Jumba la Makumbusho, na sehemu nyingine mbalimbali za jiji hilo Masaki na Kariakoo ambapo kungekuwa na vivutio kwa watalii badala ya kufika katika jiji hilo na kisha kupanda ndege kwenda kwengine.

 

 

Alisisitiza pia kuimarishwa zaidi kwa vivutio vya utalii vilivyo katika Nyanda za Kusini, Mkoa wa Pwani na kadhalika, ambavyo vinaweza kuwa vivutio vikubwa kwa watalii ambapo wanaweza kuona vitu vingine mbali na wanyama tu.

Leave A Reply