The House of Favourite Newspapers

Nani ana wajibu wa kujishusha, mwanamke au mwanaume?-2

0

WIKI iliyopita tuliianza mada hii nzuri yenye elimu kuhusu mpango wa Mungu katika ndoa.

Tuliishia pale Mungu alipokuwa akitoa adhabu kwa nyoka. Adhabu hiyo pia aliitoa kwa mwanaume (Adam) na kwa mwanamke (Eva).

ENDELEA SASA…

Mwanamke aliambiwa atazaa kwa uchungu, huo ndiyo uhalisia. Hadi leo mwanamke anaendelea kuzaa kwa uchungu. Jukumu hilo ni la kwake, si la mwanaume. Mwanaume anatekeleza lile la kwake la kutafuta na kula kwa jasho.

Hii ina maana kubwa sana katika maisha yetu. Kweli mwanaume anapaswa kumheshimu mwanamke lakini mwanamke anapaswa kumheshimu zaidi mwanaume.

Maandiko kutoka Wakolosai sura ya 3:18-19 yanasema; Enyi akina mama, watiini waume zenu, kwani ndivyo apendavyo Bwana. Nanyi waume, wapendeni wake zenu, na msiwe wakali kwao.

Hapo tulifundishwa jinsi gani Mungu alitaka wanawake wawatii waume zao. Utii kwa mwanaume agizo kwao. Kutii maana yake ni pana. Ni kuwa na nidhamu, kuheshimu. Ili kujenga ndoa, wanawake wanapaswa kweli kuwatii waume zao.

Kupitia somo hilo, wanaume nao wameagizwa kuwapenda wake zao. Wanaume kweli wanapaswa kuwapenda wake zao ambao nao pia ni watiifu. Maisha ya ndoa yanakuwa mazuri kama vitu hivyo viwili mnaviishi kila siku.

Kila mmoja atimize wajibu wake. Upendo ni nguzo muhimu sana kwa wanandoa. Pasipo pendo hakuna amani. Panapokosa amani ni vita au mfarakano. Basi mwanaume ampende kweli mke wake, mke naye amtii mumewe. Amheshimu na maisha ya ndoa yatakuwa mazuri.

Elimishaneni kuhusu upendo. Zungumzieni changamoto huku kila mmoja akitafakari mpango wa Mungu. Akifahamu mipaka yake. Mwanaume asioneshe ubabe kwa kisingizio cha yeye ndiyo kichwa cha familia. Afahamu na yeye kwamba anapaswa kumheshimu mkewe.

Mke naye asitumie kigezo cha kupendwa, akaonesha dharau. Afahamu kwamba na yeye anapaswa kumpenda mume wake kwa nguvu na akili zake zote. Huo utakuwa ndiyo upendo wa kweli. Ni hatari sana kama mmoja akawa anampenda mwenzake halafu mwenzake harudishi upendo.

Mwanamke awe mnyenyekevu kwa mumewe. Awe wa kwanza kujishusha hata kama anaamini yeye ndiyo kakosewa. Ajishushe halafu baadaye amueleze ukweli mumewe wakati jambo hilo linapokuwa limeshapita.

Si uhodari mwanamke kumvimbia mumewe. Eti ushindane naye, unategemea uwe mshindi? Halafu ukishashinda itakusaidia nini? utapata faida gani? Marafiki zangu, ndoa ukiishi katika misingi ya kujitambua, huwezi kuiona ngumu.

Mwanamke aheshimu pia kile kitendo cha Mungu kuanza kumuumba mwanaume. Mwanaume ametangulia. Mwanaume alipewa mamlaka ya kutoa majina kwa vitu vyote duniani.

Alitambua mwanaume anahitaji msaidizi na hata huyo msaidizi (Eva) alipoletwa duniani, Mungu alimpa mamlaka Adam ampe jina huyo mwanamke.

Rejea Mwanzo sura ya 2: 23-24: Huyo mwanaume akasema, “Huyu sasa ni mfupa wa mifupa yangu na nyama ya nyama yangu,  ataitwa ‘mwanamke,’  kwa kuwa alitolewa katika mwanaume.’’Kwa sababu hii mwanaume atamwacha baba yake na mama yake na kuambatana na mkewe nao watakuwa mwili mmoja.

Huo ndiyo ukweli ambao wanawake wengi wanaufahamu. Wanashindwa kuutekeleza kutokana tu na sababu mbalimbali kama kukua kwa utandawazi na mengineyo.

Wanataka wawe na sauti, ni sawa lakini kikubwa cha kuzingatia ni matakwa ya Mungu. Mheshimu mume wako naye akupende, nawe mpende daima!

Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri. Mungu awabariki wote. Nawapenda!

Leave A Reply