Nani kasema mwanamke aliyezaa haolewi?

healthycouple-lifemagKaribuni wapenzi wanajamvi. Ni siku nyingine tumepewa na Mungu tuweze kupeana elimu katika safu yetu hii ya uhusiano. Ninaamini Mungu ametujalia neema hii ya kujifunza ili tuweze kuishi vyema kwenye uhusiano. Unajua Mungu hapendi mifarakano na migongano kwenye familia zetu.

Napata shida sana kuona bado kuna jamii au watu ambao wana mawazo mgando katika vichwa vyao, eti mwanamke aliyezaa hawezi kuolewa na mwanaume ambaye hakumzalisha? Hayo ni mawazo potofu, tena ni ya kizamani, yasiyo na muono wa mbele kuhusu maisha.

Kama mwanamke aliyezaa hawezi kuolewa, vipi kwa wewe au yule aliyemzalisha? Kwa nini aruhusiwe kuoa? Hapa unakuwa unawatenga na kuwanyanyapaa waliozalishwa, unawaonea dada, mama, shangazi na bibi zetu wakati ukweli ukiangalia chanzo ni wewe mwanaume. Inauma sana na inakera. Tusisahau, makosa yetu hayaondoi ubinadamu wetu!

Nasema na wewe ambaye umekataa kumuoa msichana fulani kwa sababu tu eti amezaa na mtu mwingine. Nazungumza na ninyi wazazi ambao mmemkataza kijana wenu kumuoa binti wa jirani kisa ana mtoto. Hivi kama dada au mtoto wako akifanyiwa hivyo utajisikia? Ewe mzazi au mlezi mwenye tabia hiyo, tafakari upya juu ya mtazamo huo.

Si sawa, huo ni ubaguzi wa kijinsia. Nani kasema kuzaa ni umalaya, kushindikana au ni dalili ya kushindwa kudumu kwenye ndoa? Hapana! Kumbuka kuna wengine walibakwa. Kuna wengine ugumu wa maisha ulichangia wakapata mimba. Kuna wengine kutokana na mapito ya utotoni walishindwa kujitambua, matokeo yake wakapata watoto.

Wakati mwingine yawezakana hata binti mwenyewe alikuambia kuwa ana mtoto. Ukakubali halafu leo wazazi wanaingilia, wanakuambia usimuoe. Hivi kweli inaingia akilini? Wewe ni mzazi wa aina gani unayechangia vijana waendelee kuchepuka wakati wanaweza kuoana?

Jamani ya Mungu mengi! Unaweza kuoa ambaye hajazaa kwa kudhani atakuwa mke mwema lakini ukajikuta umeangukia pabaya. Unaweza kumuona ambaye amezaa hata watoto wawili nakuendelea lakini ukafurahia maisha na penzi lake kwani hakusumbui. Hana tabia ya ajabu na pengine mwenza wake ndiye aliyekuwa tatizo ndiyo maana wakaachana au aliachwa.

Rai yangu, kama umempenda mdada au mwanamke ambaye amezaa, siyo poa kumuacha kwa sababu eti ana mtoto. Huo siyo utu, kikubwa ni kijiridhisha kwa tabia na mwenendo wake kama anakufaa basi mkaribishe moyoni mwako. Nanyi wazazi au walezi haipendezi kuwachagulia na kuwafanyia uamuzi watoto wenu wanapohitaji kupata wenza wao.

Mkifanya hivyo, mnawaumiza sana kwenye uhusiano wao bila kujua. Hebu pata picha wewe uliyemchagulia mwanao mwanamke wa kuishi naye huko Bukoba halafu uliyemchagulia (mwanao) anaenda kuishi Mtwara kila wakikorofishana, mwanao anakulalamikia kwa kumlazimisha kumchagulia mchumba. Haipendezi tuwape uhuru vijana wetu.

Usikose kutembelea ukurasa wetu wa Mimi na Uhusiano kwenye Mtandao wa Kijamii wa Facebook, Insta:mimi_na_uhusiano au unaweza kujiunga kwenye group letu la WhatsApp kwa namba za hapo juu.


Loading...

Toa comment