The House of Favourite Newspapers

KIGOGO ANASWA LIVE USIKU, ASEMA “NAOMBA NIPIGWE RISASI”

MOROGORO: “Jamani kwa hii aibu sitaweza kuendelea kuishi, naomba nipigwe tu risasi nife,” hayo ni maneno ya kuonesha kukata tamaa aliyoyatoa kigogo mmoja aliyedaiwa ni Injinia wa Maji aliyefahamika kwa jina la Laurent baada ya kunaswa laivu akiwa na mke wa mtu gesti.

NI TUKIO BAYA

Laurent alinaswa usiku akiwa na mke wa mtu katika gesti moja iitwayo Monile Travellers iliyopo Kigurunyembe Mtaa wa Kolla B Kata ya Kilakala ambapo inadaiwa kubambwa huko kulitokana na mtego uliowekwa kwa muda mrefu baada ya mwenye mali aliyefahamika kwa jina la Roma Masai ambaye ni Injinia wa Ujenzi kubaini kuwa anamegewa penzi lake.

 

MSIKIE SHUHUDA

Akizungumza na Amani, kijana mmoja aliyeomba jina lake lisiandikwe gazetini aliyekuwa mmoja wa waliokuwa wameongozana na mwenye mume alisema kuwa, kulikuwepo na madai ya Laurent kumendea penzi la mke wa mtu huyo ambapo siku hiyo ilibidi wamuwekee mtego na hatimaye kumnasa.

“Unajua kumekuwepo na madai kwamba Laurent kajiweka kwa mke huyo wa mtu, hivyo siku hiyo mtego ulipowekwa ndipo ukafyatuka. Hatukufanya fumanizi kienyeji maana tunajua kuna mambo ya kisheria, tulikwenda polisi tukapewa askari, lakini pia tukaenda kumchukua mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Kolla B ilipo gesti hiyo, Asidilile Ulisaja Mwaitebele na tulipofika na kugonga ndipo tulipowakuta laivu.

 

“Ni fedheha kwa kweli, jamaa alijisikia vibaya sana kuona mwenye mali yuko mbele yake. Mbaya zaidi wanajuana vizuri, wanaitana shemeji. Yaani alitamani ardhi ipasuke aingie. Akabaki kujutia tu hadi na sisi wenyewe tukaanza kumuonea huruma,” alisema shuhuda huyo.

Shuhuda huyo aliendelea kutiririka kuwa, baada ya kigogo huyo kuona ameikanyaga aibu isiyomithilika, akaanza kusema kuwa, bora apigwe risasi afe. Ikaelezwa kuwa, baada ya Laurent kuonekana kama aliyepagawa huku akitaja suala la kifo, askari walilazimika kumpiga pingu ili asije kufanya tukio lolote la kujidhuru.

 

“Alichotaka yule mwenye mali ni kumnasa anayeiyumbisha ndoa yake, hakutaka kumdhuru wala kumfanyia kitu chochote kibaya, ila inavyoonekana angeachwa aondoke bila mazungumzo, huenda angeweza kwenda kujidhuru,” alisema mhabarishaji huyo. Mwandishi wetu alifanikiwa kuzungumza Roma Masai ambaye alisema:

“Nilipoona mke wangu kabadilika kitabia niliamua kufanya upelelezi na kubaini kwamba huyu Lau anamzuzua, baada ya kupata uhakika nikatega mtego na leo umefyatuka. “Kilichoniuma zaidi baada ya kuipekua simu ya mke wangu nilikuta sms za huyu jamaa akiniponda mimi, eti mke wangu asiniogope. Iliniuma sana.”

 

Baada ya tukio hilo, mwandishi wetu alijaribu kupiga namba ya simu ya Laurent, alipopokea na kuulizwa ilikuwaje akaamua kujiweka kwa shemeji yake, alikata simu na hata alipopigiwa tena, hakupokea. Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kolla B, Asidilile Mwaitebele alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kufunguka hivi:

“Siku hiyo maafisa wa polisi walifika nyumbani kwangu na kunieleza kuwa, kuna mtu alikwenda kuripoti polisi kwamba anahisi mke wake yuko katika gesti ile, kwa hiyo kwa kuwa hawakutaka kutokee uvunjifu wa amani wakaona waje kwangu wakijua mimi ndiye mwenyekiti wa usalama katika mtaa huu, mimi nikaongozana nao mpaka mahali hapa na kweli tumewakuta, nikawakabidhi askari wawachukue watu hao na kwenda nao polisi katika hali ya amani na usalama na hakuna aliyejeruhiwa.”

Comments are closed.