NAPASUA JIPU: Damu Isiyokuwa na Hatia Haitawaacha Salama Wauaji Kibiti

 

NEEMA na baraka za Mungu maishani mwangu ni za kipekee mno. Ni vyema kujijengea utaratibu wa kumshukuru Mungu kila tunapopata nafasi ya kuiona siku iitwayo leo.

 

Asante Mungu kwa kila unalonifanyia maishani mwangu, siku zote za uhai wangu chini ya jua, sitaacha kulihimidi jina lako.

Naipenda sana nchi yangu. Hili liko wazi na nimekuwa nikilisema mara kwa mara kupitia maandishi na hotuba zangu nyingi. Mapenzi yangu kwa nchi yangu, yanisukuma mimi na mke wangu kufikia uamuzi wa kumuita binti yetu, jina la Tanzania. Hii ni alama na kielelezo tosha kabisa kwamba, naipenda Tanzania.

 

Miaka mingi iliyopita, vitendo vya uhalifu vilikuwa kitendawili nchini kwetu. Tulizoea kusikia mauji yakitokea nchi za jirani, nchi yetu ilitawaliwa na amani na upendo mkubwa mno, kiasi cha kuwa mfano wa kuigwa na mataifa mengine, makubwa kwa madogo.

Leo stori inaanza kubadilika. Nchi inaanza kugubikwa na taswira mbaya ya umwagaji wa damu, mauaji kila kukicha tena kwa raia wasiokuwa na hatia.

 

Mtanzania yeyote mwenye akili timamu na mapenzi kwa nchi yake kama ilivyo kwangu, lazima yuko kwenye maumivu makali mno, juu ya mauaji yanayoendelea huko Kibiti, Rufiji mkoani Pwani.

Jambo moja ambalo nimekuwa nikijiuliza, hivi inakuwaje mtu unashika silaha na kuielekeza kwa binadamu mwenzako na kumwaga damu yake? Unapata wapi ujasiri huo? Wengine ni waoga hata kuchinja kuku tu, iweje mtu anamuua mwenzake tena na kwa tambo nyingi na maneno yenye kuashiria kufurahia jambo hilo? Nimekuwa nikijiuliza maswali haya lakini jibu lake sijapata.

 

Haijalishi mtu amekukosea kiasi gani, hakuna mwenye haki ya kutoa hukumu, tena hukumu yenyewe ikiwa ni kumwaga damu. Siko tayari kuishuhudia nchi yangu ikipoteza taswira na heshima ya kuitwa kisiwa cha amani, ndiyo maana napaza sauti na kulaani vikali mno vitendo vya mauaji huko Kibiti na maeneo mengine ndani ya nchi yangu.

 

Kitu kimoja ambacho wauaji na watu wote tunapaswa kujua ni kwamba, damu ya mtu haijawahi kumwagika na kukaa kimya. Sauti yake huendelea kumlilia aliyeimwaga. Nachelea kusema kuwa, mwisho wa wauaji wa raia na baadhi ya viongozi na askari wetu, hawatabaki salama kwa namna yoyote.

 

Imani yangu ni kwamba wamemwaga damu ambayo haina hatia na usalama wao ni mdogo mno. Naamini serikali iko katika mapambano makubwa kuhakikisha mauaji haya yanatokomezwa, lakini neno langu ni kwamba hata kama kwa sasa wataukwepa mkono wa serikali, lakini chozi la damu isiyokuwa na hatia haitawaacha salama wauaji hao.

 

Binafsi nakosa usingizi, ni mara nyingi nimekuwa nikiamka katikati ya usiku na kuanza kutafakari kwa kina juu  ya mauaji haya. Nani yuko nyuma yake? Anatekeleza hayo kwa faida ya nani? Mwisho wake ni nini? Amekosewa na watu wote hao? Kosa gani amefanyiwa? Maswali haya yananikosesha usingizi sana.

Ni jukumu letu sote Watanzania kusimama pamoja na kupaza sauti zetu kupinga kwa nguvu zetu zote mauaji haya, kwani sisi leo tunaishi kwa furaha na kufaidi mema ya nchi yetu, zikiwa ni jitihada za waasisi wa Taifa letu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Karume na wengine kupigana kwa nguvu kuhakikisha nchi inakuwa salama na yenye amani tele.

 

Inasikitisha mno kuona kama taifa tumefikia huku. Kuuana kinyama namna hii, tena wakati mwingine hadi kwa walinzi wetu wa usalama yaani polisi.

Hakuna mtu aliyewahi kufanya uovu wowote kisha dunia ikamuacha salama, mshahara na marupurupu ya kila mtu hulipwa hapahapa duniani!

 

Mauaji ya Rufiji, Mkuranga na Kibiti, hayawahusu wana Pwani peke yao, ni msiba wa Watanzania wote, hivyo tuungane na serikali kuhakikisha tunatokomeza uhalifu huu kwa sisi raia kutoa taarifa sahihi za kufichua aina yoyote ya uovu ambao unafanywa na baadhi ya watu au vikundi vidogovidogo ili tubaki na nchi yetu ikiwa salama kwetu sisi na hata vizazi vyetu vijavyo.

Nimalize kwa kuweka mzani sawa kwamba, kuipoteza amani huwa ni rahisi mno, lakini kuirejesha ni kazi nguvu kuliko inavyoweza kufikiriwa.

 

Nchi nyingi zinajuta kwa kukubali kuichezea amani waliyokuwanayo zamani, leo hii ni machafuko na mapigano kila kona ya nchi zao, majuto ni makubwa.

Vitendo vihatarishavyo amani, huanza kidogokidogo kama hivi, hatimaye hushamiri na kujikuta nchi nzima ikiingia kwenye machafuko ya mauaji kwa kushindwa tu kukemea mapema. Tushirikiane na jeshi la polisi chini ya IGP Simon Sirro, hakika tutashinda.

 

Namuomba Mungu azipokee roho za marehemu wote waliouawa huko Mkuranga, Rufiji na Kibiti, lakini adhabu kwa wauaji ni maradufu kwao na vizazi vyao, kwani Mungu huwapatiliza watu maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu, cha nne na cha wamchukizao.

Mungu Ubariki Mkoa wa Pwani, Mungu Ibariki Tanzania na Mungu Ibariki Afrika.

Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.

Eric Shigongo| Dar es Salaam

 

Hivi Ndivyo Wauaji Kibiti Walivyochoma Gari, Pikipiki


Loading...

Toa comment