The House of Favourite Newspapers

Nape Afunguka Kuhusu Kuzuiwa Mikutano ya Kisiasa Nchini

0
Nape Nnauye.
MBUNGE wa Mtama, Nape Nnauye amesema kuzuiwa mikutano ya kisiasa si kuminya demokrasia kwa kuwa  kuna bunge ambalo linaweza kutumika kutolea maoni yao. 
Akihojiwa na kituo cha Televisheni cha  KTN kutoka nchini Kenya katika kipindi cha siasa za kanda kuhusu demokrasia katika Afrika, Nape amesema demokrasia inatakiwa kutafsiriwa kulingana na maeneo tuliyopo.
“Afrika hatuwezi kuwa na demokrasia iliyo sawa na Marekani,” amesema.
Nape alitakiwa kutoa maoni yake kuhusu viongozi wa Chadema kudai kwamba, Rais John Magufuli anaminya demokrasia hasa kuzuia mikutano ya hadhara. Akijibu, Nape amesema nchi za Afrika hazitakiwi kutafsiri demokrasia kwa kujilinganisha na nchi zilizoendelea za Magharibi.
“Hapa kwetu baada ya uchaguzi mkuu tunaruhusiwa kufanya mikutano kwenye majimbo yetu haturuhusiwi kufanya mikutano nje ya majimbo yetu,” amesema.
Amesema uchaguzi ukishamalizika siasa zinahamia bungeni ambako wabunge wanaweza kutoa maoni yao.
“Sioni kama hapa demokrasia inaminywa au kuna udikteta kwa sababu hiyo inawahusu wabunge wote kutoka chama tawala na vyama vya upinzani,” amesema.
Nape ambaye alikuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, amesema zamani wanasiasa waliruhusiwa kufanya mikutano katika maeneo mbalimbali ya nchi. Nape amesema wakati wa uchaguzi mkuu shughuli nyingi huwa zinasimama kwa sababu ya mikutano ya wanasiasa.
“Kwa hiyo kuna umuhimu wa viongozi wa kisiasa kwenda kutekeleza yale waliyowaahidi wananchi,” amesema.
Nape amewataka wasomi kutoa tafsiri kwa upana kuhusu dhana ya demokrasia  ili wananchi waweze kuitekeleza kulingana na maeneo waliyopo.
Leave A Reply