The House of Favourite Newspapers

Nape aishukuru Kampuni ya Global Publishers

0

napeBrighton Masalu

KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye ameishukuru Kampuni ya Global Publishers, wachapishaji wa Magazeti ya Uwazi, Ijumaa, Risasi, Amani na Championi kwa mchango wake mkubwa katika kuelimisha jamii, pia jitihada zake za kukiunga mkono kwa asilimia kubwa chama hicho katika kipindi chote cha kampeni za uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari ndani ya ofisi za Global Publishers, Mwenge- Bamaga jijini Dar, hivi karibuni, Nape alisema ushindi wa CCM kushika dola umechangiwa kwa kiasi kikubwa na kampuni hiyo ambapo magazeti yake yaliandika kwa kina juu ya chama hicho.

Nape, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mtama, mara nyingi alipokuwa kwenye mizunguko ya kampeni zake, alijionea jinsi magazeti hayo yalivyokuwa yakisomwa na watu wengi hususan akina mama, jambo ambalo lilisaidia kufanikisha ushindi wake.

AFAFANUA BAO LA MKONO

Katika kipindi cha maswali kutoka kwa waandishi, Nape aliulizwa juu ya kauli aliyowahi kuitoa ya ‘Bao la Mkono’ ambapo alisema ilitafsiriwa tofauti na maana halisi kwani lengo lake ni kuhamasisha upigaji kura kwa kuwa zoezi hilo hufanywa kwa kutumia mkono na yeye alimaanisha kupitia kura CCM itawashinda wapinzani wake.

“Kwa hiyo watu walilikuza jambo hilo tofauti kabisa na nilichokimaanisha, kwani jamani kura hupigwa kwa miguu? Si ni kwa mkono, ndiyo maana nilisema tutashinda kwa bao la mkono, tusipende kukuza mambo jamani,” alisema Nape.

AJINASIBU KUTOKUWA NA DOA RUSHWA

Katika mahojiano yaliyodumu kwa takriban saa mbili, Nape alitumia nafasi hiyo kujipambanua kwa kuwa mstari wa mbele katika vita dhidi ya ufisadi na kwamba katika kipindi chote cha utumishi wake ikiwemo ukuu wa wilaya, hajawahi kuomba, kupokea wala kutoa rushwa.

“Wakati napigania jengo la vijana, fedha zilikuwa zinazunguka nyumbani kwangu, lakini nilikataa, wakati nikiwa mkuu wa wilaya kule Masasi, niliwahi kukamata Basi la Buffalo likiwa na pembe za ndovu, rushwa ilikuwa nje nje lakini nilikataa hadi sasa basi hilo lipo pale Masasi linateketea, kwa hiyo rekodi zipo, tunataka kiongozi anayepinga rushwa kwa vitendo na si maneno,” alisema Nape.

AMZUNGUMZIA MAGUFULI

Katika mazungumzo hayo, Nape alimzungumzia Rais John Pombe Magufuli kuwa ni mtu mchapakazi, asiye na vinasaba vya CCM, hivyo atasaidia kukibadili chama kwa baadhi ya mambo ambayo si sahihi na kwamba ana imani naye.

“Magufuli hana u-kijanikijani, maana yake si mtu wa CCM sana, hana mchezo kwa hiyo tumepata mtu sahihi kama chama na kama taifa,” alisema.

UKAWA WAMEIPA SOMO CCM

Hata hivyo, Nape alisema katika kipindi ambacho CCM imepata changamoto kubwa ni katika uchaguzi ulioisha ambapo mwamko mkubwa uliamshwa na vyama vya upinzani baada ya kuungana, hivyo kuna mambo ambayo CCM imejifunza na itayafanyia kazi. Pia, alisema kuondoka kwa Lowassa kuliwapa  changamoto kwa kuwa anazijua baadhi ya mbinu za ushindi wa CCM ambazo ni za halali, hivyo kuliwalazimu kupanga mikakati mipya ya ushindi.

Leave A Reply