The House of Favourite Newspapers

Nape asiwe mgeni rasmi tu

0

mg_2571

Nape Nnauye.

NI Jumamosi nyingine tulivu ambayo wadau wa soka jioni wanajongea viwanjani au katika luninga zao kutazama mechi mbalimbali za soka iwe ndani au nje ya nchi.

Ligi Kuu Bara inaendelea wikiendi hii na klabu kadhaa zitashuka uwanjani lakini mechi gumzo ni kati ya Simba na Azam FC, leo Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Pia kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga, leo Yanga itacheza na Mgambo JKT, huu nao si mchezo mdogo kwani mara nyingi Mgambo imekuwa ikileta upinzani kwa mabingwa hao watetezi wa ligi kuu.

Nirudi katika mada kuu ya leo, kwamba Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli amemteua Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye kuwa waziri mpya wa habari, utamaduni, wasanii na michezo.

Kwanza nimpongeze Magufuli kwa kuona mbali kumteua Nape katika nafasi hiyo, kwani tunaamini ni kijana mwenzetu anayeweza kuzungumza lugha moja na sisi akatuelewa haraka.

Mara nyingi tumeona Nape akishiriki katika matamasha na hata kupiga gitaa wakati mwingine katika baadhi ya bendi anazokwenda kutazama burudani au awe amealikwa kwa kazi maalum.

Kama alivyosema Magufuli, walioteuliwa katika baraza lake la mawaziri wanatakiwa kupiga kazi na siyo kuwa viongozi majina tu, kwamba wasiishie kuzindua matamasha na kuwa wageni rasmi tu katika mechi za fainali na kuvalisha medali wanamichezo.

Yawezekana ikawa ngumu kwa watu kunielewa au hata Nape mwenyewe, lakini nitoe mfano mmoja kutoka kwa wenzetu ambao wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika soka.
Mwaka 2012 nilikuwa jijini Durban, Afrika Kusini katika kongamano la Soccerlex, hili ni kongamano linalohusisha wadau mbalimbali wa soka Afrika na wengine kutoka mataifa mengine duniani.

Mawaziri wa michezo kutoka Nigeria na Ghana walitoa ushuhuda ambao unawafanya waendelee kupiga hatua katika soka duniani na wana idadi kubwa ya wachezaji wanaocheza soka la kulipwa ulimwenguni.

Waziri wa Nigeria ndiye aliyezungumza zaidi namna nchi yake inavyoipa sekta ya michezo kipaumbele na kuwa moja kati ya chanzo kikuu cha ajira kwa vijana. Hapo jamii inafaidika lakini na serikali nayo inafaidika kupitia kodi.

Serikali ya Nigeria inafikia malengo yake mengi kupitia michezo hasa soka kwani kwa idadi ya wanasoka walio nje na ndani ya nchi, inajipunguzia mzigo mkubwa wa kuihudumia jamii isiyo na kazi huku ikijiingizia pato kwa kodi.

Sekta ya michezo na sanaa nchini humo imerasimishwa muda mrefu na kuna mfumo unaomruhusu mtu kulipa kodi, hivyo kwa kuwa serikali inaingiza kipato nayo inasaidia kwa kiasi kikubwa michezo.

Waziri huyo anasema, kuna fungu kubwa la fedha wanalotoa kwa akademi mbalimbali za nchini mwao lakini hata timu ambazo zina vikosi vya vijana.

Serikali haijali kama Shirikisho la Soka Nigeria (NFF), linatoa ruzuku kwa akademi hizo, yenyewe inaongeza zaidi fedha kwa vituo hivyo ili viendelee kufanya vizuri.

Nchini Nigeria kwa sasa michezo hasa soka ni kiwanda kingine kinachotoa mamilioni ya ajira kwa vijana na serikali haioni tatizo kuwawezesha kufikia mafanikio yao.

Hakuna urasimu wowote katika kuhakikisha vijana wanakwenda popote duniani kutafuta maisha yao kupitia soka, ndiyo maana unaona vijana wa Kinigeria wamejazana kila mahali duniani.

Waziri huyo anasema siri kubwa ya mafanikio yao katika soka ni kusimamia kwa ufasaha soka la vijana na kizazi hadi kizazi kinaendeleza falsafa hiyo na sasa ni kitu cha kawaida katika utekelezaji.

Tazama leo hii, Wanigeria wamejazana hadi Mwananyamala wapo na katika ligi yetu wengi wamecheza na watacheza sana tu, sababu kwao ni sekta rasmi iliyorasimishwa na serikali yao.

Sasa anachopaswa kufanya Nape baada ya kuteuliwa kuwa waziri wa habari, utamaduni, wasanii na michezo ni kupambana ikiwezekana bungeni ili sekta ya michezo na sanaa iwe rasmi, yaani irasimishwe.

Msanii Nasibu Abdul ‘Diamond’ sasa anaingiza kiasi kikubwa cha fedha kwa mwezi na kwa shoo yake moja tu anapata zaidi ya Sh milioni 15, huyu ana watu kama kumi wanaofanya naye kazi jukwaani. Wengine zaidi ya watano wanafanya kazi zake nyingine ikiwemo kutoa habari zake katika mitandao ya kijamii.

Katika kazi zake zote, Diamond halipi kodi kwa kuwa sekta ya sanaa haipo rasmi na hakuna anayejali kama hapo mambo yangekaa vizuri serikali ingeingiza kiasi kikubwa cha fedha.

Kwamba Diamond angewekewa mfumo wa kulipa kodi na yeye angetoza kodi hiyo kwa watu wanaomkodi kufanya shoo zake, hapo serikali ingeingiza kiasi kikubwa cha fedha kupitia wasanii.

Katika soka, Nape anatakiwa kutumbua majipu mengi katika ngazi ya uongozi hasa nyakati za uchaguzi ambapo ndipo madudu yanapofanyika kwa asilimia kubwa.

Hii ina maana, hata kama serikali itarasimisha michezo kuwa sekta rasmi, bila uongozi mzuri itakuwa sawa na bure. Ukichunguza viongozi wengi wa soka letu kuanzia ngazi ya klabu hadi vyama, wengi wameingia madarakani kimagumashi na ndiyo wanaoyumbisha maendeleo ya soka nchini.

Nape akishamaliza kutumbua majipu haya, tukapata viongozi sahihi hapo tunaweza kupiga hatua. Wanaweza kumtisha hasa katika soka kwa kusema, Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), halitaki serikali kuingilia uongozi, lakini lazima hujue klabu au vyama vya soka hupata usajili kutoka serikalini.

Hivyo, bado serikali ina mchango mkubwa wa kurekebisha uozo uliopo katika soka na Nape naamini atafanikiwa kama akitaka kwani njia ni rahisi sana na zinafahamika.
Nipo Japan huku, kesho Jumapili naenda kuwatazama Watanzania wenzangu Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wakiichezea TP Mazembe katika mechi ya robo fainali ya Kombe la Dunia la Klabu dhidi ya Sanfrecce Hiroshima kwenye Uwanja wa Nagai.
Niwatakie kila la kheri wenzetu hawa na wiki ijayo nitakuja na makala maalum kuhusu mafanikio ya soka la Japan.

Leave A Reply