Nape; Hili la Kuwalipa Wasanii Liangalie kwa Jicho la Tatu

mg_2571Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye.

KWAKO Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye. Habari ya siku kaka? Pole na shughuli nzito za kuiendesha wizara hiyo adimu inayogusa vijana kwa kiasi kikubwa.

Kitambo kidogo hatujaonana, najua ni kwa sababu ya majukumu yako na yangu pia, lakini ukitaka kujua hali yangu, mimi ni mzima namshukuru Mungu. Naendelea na majukumu yangu kama kawaida, kuuhabarisha umma kupitia magazeti yanayopendwa zaidi nchini ya Global Publishers.

Dhumuni la kukuandikia barua hii ni kutaka kwanza kukupongeza kwa kuanza vizuri kuitumikia wizara yako. Umeanza vizuri kwa kuonesha kwa vitendo kwamba unakerwa na changamoto mbalimbali zilizopo kwenye wizara yako. Nimekusikia umezungumzia masuala ya michezo, nimesikia pia ukiwazungumzia wasanii.

Kwenye eneo la wasanii ndipo kwenye kiini cha barua yangu ya leo kwako. Nakumbuka mara baada ya kuteuliwa kuongoza wizara hiyo, wewe pamoja na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage mliahidi kusimamia sheria itakayowalipa wasanii pindi nyimbo zao zitakapochezwa kwenye vituo mbalimbali vya redio na televisheni.

Mliahidi sheria hiyo itaanza kufanya kazi kuanzia Januari Mosi. Nilifurahi sana maana niliona ni jambo jema kwa wasanii wetu, wataneemeka na pengine hatutaona wakiishi kimaskini. Lakini nasikitika kuona bado suala hilo limegubikwa na giza nene ambalo halitoi nuru ya tunakoelekea.

Kaka yangu, hadi sasa utekelezaji wa suala hilo unaonekana kuwa mgumu. Nashuhudia tu sinema zikiendelea kila uchwao. Wasanii wenyewe nao hawajakubaliana na mfumo huo kutokana na sababu mbalimbali. Wamiliki wa vyombo vya habari nao wamekaa kimya, wanaendelea kupiga nyimbo bure kama kawaida.

Vyombo mlivyovipa dhamana ya kusimamia suala hilo kama Chama cha Hakimiliki nchini (COSOTA) Kampuni ya CMEA ambayo imeingia mkataba na COSOTA ili kuweza kusimamia mapato hayo ya wasanii bado wapo kimya, mambo yanakwenda kama zamani.

Kimsingi kaka yangu Nape, huu mfumo bado una changamoto nyingi. Nafikiri unapaswa kuzitazama upya kwa upana wake kisha kuja na suluhu ya kudumu. Wadau wengine wanauelezea kuwa endapo utaanza kutumika, huenda ukawapoteza wasanii wadogo maana vituo vya redio na televisheni vitakuwa vinawalipa wale wasanii wakubwa ambao kwao wana ‘impact’ na wale wachanga wakakosa nafasi.

Hivyo inapaswa kujifunza pia kutoka kwa nchi za wenzetu kama Marekani ambako wameanza kuutumia muda mrefu ili kuweza kuona kama unaweza kufanya kazi hapa kwetu na kwa kiwango gani.

Walikutana na changamoto gani kabla ya kuanza kuutumia? Walizitatuaje? Msanii mkubwa na mdogo atalipwaje?
Tuletee utaratibu mzuri ambao unaweza kuwa rafiki kwa wasanii na wamiliki wa vyombo vya habari.

Naamini tayari mlishautazama kwa mapana yake lakini kuna kila sababu ya kuangalia ni wapi tunapokwama. Kama ni vyombo vilivyopewa dhamana, vishughulike tu.
Nina imani utaifanyia kazi barua yangu, nikutakie utekelezaji mwema.
Wako katika ujenzi wa taifa,

Erick Evarist

Loading...

Toa comment