MBUNGE wa Mtama na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Nape Nnauye, amesema kitendo cha Serikali kuamua kufyeka miti katika mbuga ya wanyama ya Selous ili kutekeleza mradi wa umeme, hakikubaliki kwa sababu kinakiuka sheria ya bunge mwaka 2004 ya usimamizi wa mazingira kimkakati.
Nape ameyasema hayo bungeni leo alipokuwa akichangia bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2018/19 iliyowasilishwa jana na Waziri wa Wizara hiyo, Dk. Hamis Kigwangalla, na kuitaka serikali kusitisha zoezi hilo hadi pale ambapo tathmini ya kimkakati itakapokamilika huku akimtaka mwanasheria mkuu wa serikali, (AG) kuisaidia serikali kufanya kazi kwa kufuata sheria.
“Wakati tunamalizia kazi yetu ya kamati, Tanzania Forest Services (TFS) ilitangaza tenda ya ukataji miti katika hifadhi ya Selous ambalo ni eneo linalokadiriwa kufikia zaidi ya cubic meter milioni 3, hili eneo lina ukubwa zaidi ya Mkoa wa Dar es Salaam au Unguja, imensihtua sana.
“Ikumbukwe mwaka 2004 Bunge lilitunga sheria ya Usimamizi wa Mazingira Kimkakati, kabla ya kutangaza tenda na kuanza kukata miti hiyo, ilitakiwa tathmini iwe imekamilika, lakini sasa hivi bado haijakamilika. Sasa nimuombe Mwanasheria Mkuu aishauri serikali ijenge utamaduni wa kuheshimu sheria tunazotunga, naiomba serikali isitishe zoezi hili isubiei tathmini ya kimkakati ikamilike.
“Selous inahusisha mikoa mitano ya Morogoro, Pwani, Lindi, Mtwara na Ruvuma, haiwezekani kupuuza maisha ya watu, mimea na wanyama kwa mikoa mitano, nadhani tusubiei tahmini ifanyike kwanza, ili kuokoa maisha ya watu hawa,” alisema Nape.
Wakati huohuo, Spika wa Bunge, Job Ndugai, amesema huku akidai ni kwa utani: “Ukikata idadi kubwa ya miti katika hifadhi ya Selous huwezi kubaki salama na badala yake utalaaniwa.”
Comments are closed.