The House of Favourite Newspapers

Nasreddine Nabi Awakomesha KMC

0

KOCHA Mkuu wa Yanga, Mtunisia, Nasreddine Nabi, amesema kuwa hatawadharau wapinzani wake KMC na badala yake atatumia kikosi chake kamili kupata pointi tatu.

 

Yanga itavaana na KMC katika mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaopigwa leo Jumanne kwenye Uwanja wa Majimaji mkoani Ruvuma.

 

Timu hiyo tayari ipo Songea tangu juzi Jumapili baada ya kusafiri kwa ndege huku katika msafara huo akiwemo kipa namba moja raia wa Mali, Djigui Diarra aliyechelewa kujiunga na kikosi hicho akitokea kwenye majukumu ya timu ya taifa.

 

Akizungumza kwa niaba ya kocha huyo, Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh, alisema maandalizi ya mchezo huo yamekamilika na hakuna majeruhi yeyote kati ya wachezaji 24 waliokuwepo katika msafara huo.

 

Saleh alisema kikosi chao hakitakuwa na mabadiliko, badala yake ataendelea kuwatumia wachezaji wote wa kikosi cha kwanza akiwemo Diarra, Fiston Mayele, Shaban Djuma, Jesus Moloko na Yannick Bangala.

 

“Kocha amepanga kuchukua pointi tatu katika kila mchezo, hiyo ni kuhakikisha tunafanikisha malengo yetu ya ubingwa tuliyojiwekea.

 

“Tayari tumechukua pointi sita katika michezo miwili mfululizo ya ligi tuliyocheza dhidi ya Kagera Sugar na Geita Gold, pia anazitaka na hizi za KMC.

 

Jana usiku kocha alifanya kikao na wachezaji wake wote mara baada ya chakula cha jioni sambamba na kuangalia video za mechi mbili za mwisho za ligi ambazo KMC imecheza kwa lengo la kuangalia upungufu na ubora uliokuwepo kwao,” alisema Saleh.

 

Akizungumzia mchezo huo, Ofisa Habari wa KMC, Christina Mwagala, alisema wamejiandaa vema na kikubwa wanahitaji pointi tatu.“Hatuangalii tunacheza na nani, kikubwa benchi letu la ufundi limefanya maandalizi ya kutosha kuhakikisha tunapata ushindi ambacho ndiyo kitu cha umuhimu ketu,” alisema Mwagala.

 

Rekodi zinaonesha kwamba, timu hizo zimekutana mara sita kwenye Ligi Kuu Bara ambapo Yanga imeshinda tatu, KMC imeshinda moja na sare mbili.

WILBERT MOLANDI, Dar

Leave A Reply