The House of Favourite Newspapers

NATASHA AFICHUA KAULI YA KANUMBA INAYOMTESA!

Suzan Lewis ‘ Natasha’

UNAPOZUNGUMZIA tasnia ya filamu Bongo, kamwe huwezi kuacha kumzungumzia mwanamama ambaye amefanya vizuri sana katika kuhakikisha anaitendea haki tasnia hiyo na kufanya kuwa kioo na kivutio kikubwa kwa jamii nzima ya Tanzania, Suzan Lewis maarufu kama Natasha ambaye pia ni mama mzazi wa msanii Yvonne Cherry ‘Monalisa’.

Amani limemfuata nyumbani kwake maeneo ya Buza jijini Dar na kuzungumza naye mambo mengi kuhusiana na maisha yake ya sanaa:

Amani: Ukiwa kama mkongwe, unazungumziaje sanaa ya zamani na sasa?

Natasha: Mh! Swali hilo ndilo ambalo huwa nashindwa kulitolea ufafanuzi lakini mimi najionea kawaida tu.

Amani: Umejaliwa kupata watoto wangapi?

Natasha: Nimejaliwa kupata mtoto mmoja tu ambaye ni Monalisa.

Amani: Umesema umejaliwa kupata mtoto mmoja tu Monalisa, nini siri ya malezi yako maana hatujawahi kumsikia kwenye skendo. Natasha: Nimemlea vizuri na kimaadili na dini pia. Unajua maji hufuata mkondo maana ukiona umemlea mtoto wako vibaya basi ni lazima akikua afanye vitu vya ajabu, mfano hivi mtu anaamua kutupia picha ambazo hazina maadili katika mitandao ya kijamii, ndiyo kama hivi unaona dunia inawapiga, wameshapata viboko viwili vitatu kwa hiyo nina imani wamejifunza.

Amani: Tukielekea kwenye sanaa, kwenye filamu ya The Lost Twins ya marehemu Kanumba uliigiza kama mama ambaye hana maadili, anatembea na vijana wadogo na unavuta sigara, unafikiri jamii inayokuzunguka inakuchukuliaje?

Natasha: Ni kwamba nashukuru kwa sababu wanaonizunguka wote wanajua mimi ni msanii kwa hivyo haiwapi shida sana ila tu walinishangaa kile kitendo cha kuvuta sigara.

Amani: Huwa unavuta sigara katika maisha ya uhalisia?

Natasha: Hapana, ni kwa vile uhusika ulikuwa unataka nifanye hivyo ikabidi nicheze na sigara, akanipa sigara fulani hivi nzito, nilipokuwa navuta nilikuwa napata shida sana kwa kuwa tulikuwa na Mzee Jengua ‘location’ akaniambia ngoja nikakuletee sigara fulani laini, kweli alivyoniletea nikavuta nikaona safi nikawa natolea moshi hadi puani mpaka watu wote wakawa wanashangaa.Image result for KANUMBA

Amani: Umecheza filamu nyingi sana na marehemu Steven Kanumba, alikuwa ni mtu wa aina gani?

Natasha: Kiukweli alikuwa ni bosi wangu lakini alikuwa ni mwenye heshima sana, alikuwa anakusikiliza nini unataka, na alikuwa siyo mtu wa kujisikia na pia kwenye malipo alikuwa ananilipa vizuri tofauti na wengine huwa wanaleta kujuana sana.

Amani: Kipi ambacho unakikumbuka kwake?

Natasha: Ambacho sitaweza kumsahau kuna siku tulikutana naye nilikuwa mimi na Monalisa tulikuwa tunaenda kanisani, akasimamisha gari tukasalimiana akasema; “Hee! Ndio mnaenda kwenye lile kanisa lenu?” Nikamjibu; ‘ndio’, akasema; “He! Hilo kanisa lenu mnasali mpaka mnamboa Mungu, mnasali asubuhi mpaka jioni!” yaani ile kauli mimi huwa inaniuma sana kila ninapoikumbuka.

Amani: Changamoto gani ambazo ulikuwa unazipata ukiwa location?

Natasha: Yaani katika kitu ambacho mpaka leo huwa nakiona kigumu ni scene ya kunywa pombe, maana unakunywa mpaka wakati mwingine unalewa na isitoshe mimi huwa sinywi pombe kwa hiyo huwa napitia kipindi kigumu sana lakini ndio hivyo ni kazi.

Amani: Mafanikio gani umeyapata kupitia sanaa.

Natasha: Namshukuru Mungu kwa kuwa nimejenga heshima kwa jamii Tanzania kwa kuwa wamekuwa na imani na mimi, Watanzania wamejenga dhana ya mimi kuwa najiheshimu na nitaendelea kujiheshimu kwa sababu kuna wengine wakishakuwa mastaa huwa heshima hawaizingatii kabisa, kingine nashukuru nimepata sehemu ya kulala na usafiri pia.

Amani: Katika wajukuu zako kuna yeyote ambaye unamuona anafuata nyayo zenu za kuigiza?

Natasha: Yah! Wako njia hiyo hiyo hasa Junior ana mwaka mmoja lakini unamuona matendo anayoyafanya, nikimuangalia nasema ndio huyu atakuwa moto kwa hiyo najitahidi kuwa nao karibu na hata hawa wakubwa zake (Sonia na Kenzo) nawaona pia wana mwelekeo kwa kuwa wanapenda kile ambacho mimi na mama yao tunakifanya.

Amani: Unawaambia nini Watanzania?

Natasha: Nawaambia kuwa wazazi wajitahidi waweze kuwalea watoto katika maadili mema na ya kumpendeza Mungu. Maji hufuata mkondo, ukimlea mtoto vibaya akikua anakuwa hivyohivyo ndio maana leo hii tunaona watoto wetu ambao hawakupata malezi mazuri au ni wale watoto ambao huwa hawawasikilizi wazazi, wanarusha picha ambazo hazina maadili mitandaoni, sisi tunapata aibu kama wazazi lakini, mimi mwanangu nilijitahidi kumlea katika malezi bora na nilimshirikisha Mungu hatimaye Monalisa amekuwa kioo cha jamii pia na namshukuru kwa kuwa tunaelewana, tunapendana maana kuna wazazi wengine huwana maelewano na watoto wao.

Comments are closed.