SHINDANO la National Public Speaking Competition limeingia katika raundi nyingine ambayo washiriki 30 watawekwa kambini na kunolewa vilivyo kabla ya kuendelea katika raundi inayofuata. Wafuatao ni washiriki waliofanikiwa kutinga 30 bora.
ANTHONIA ANTHONY SANGEDA (24)
Ni mkazi wa Morogoro na mhitimu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe. Kwa sasa ni mjasiriamali.
“Taarifa za mashindano nilizipata kutoka kwa rafiki yangu niliyesoma naye chuo, ambaye alikuwa anatambua uwezo wangu wa kuzungumza mbele ya hadhara.
“Nilianza kufuatilia kwenye mtandao wa Global na kupata taarifa za mchakato wa shindano hili. Nilisafiri kutoka Morogoro na kuja Dar kuchukua fomu na kuijaza, kusubiri siku ya michuano.
“Siku ya kwanza, nilikutana na vijana wengi sana wenye vipaji mbalimbali kwenye tasnia ya uzungumzaji na nilitengeneza marafiki kadhaa.
“Hadi kufikia hatua ya kuingia 30 bora, ninajivunia kwa sababu ni mafanikio ambayo pia nalazimika kuwashukuru majaji na waandaaji kutunoa vilivyo.
“Matarajio yangu ni kuona mashindano haya yanakuwa chachu kwa vijana wenye ndoto za kuwa wazungumzaji mbele ya hadhara na hivyo kutumia nafasi hii kujifunza ili mwakani waweze kujitokeza kwa wingi.
“Changamoto katika mashindano haya zilikuwa nyingi kwani kila kijana alionekana kujua alichoenda kufanya, hivyo kuwaweka majaji kwenye wakati mgumu kutambua nani anafaa zaidi.
“Rai yangu kwa wote wanaoendelea na 30 bora ni kuwaomba watumie nafasi hii kuongeza ujuzi na kufanya vizuri zaidi ya awali ili mwisho wa siku wapatikane washindi wengi wakiwakilishwa na watatu watakaobahatika.”
ABDILLAH RASHIDI MPEHE (20)
Ni mwanafunzi wa Chuo cha Diplomasia. Anasoma Shahada ya kwanza ya Uhusiano wa Kimataifa na Diplomasia.
“Taarifa za shindano hili la NPSC, nilizipata kupitia kongamano la wanachuo wenzangu ambapo mkurugenzi wa Global Publishers, Eric Shigongo, alitangaza rasmi kuhusu shindano hilo.
“Siku ya kwanza niliingiwa na hofu kushiriki shindano hili, maana nilikutana na watu zaidi ya 300. Ila sikukata tamaa, nilimtanguliza Mungu mbele na kuyarekebisha makosa madogo madogo ambayo majaji waliyakosoa.
“Kupita hatua zote tatu haikuwa kazi rahisi, maana washiriki wote walikuwa na uwezo mkubwa wa kuzungumza na hadhira. Hakika ni mapenzi ya Mwenyezi Mungu tu.
“Kuingia katika kundi la watu 30 bora katika shindano hili, kunanipa hamasa ya kujiandaa na kufanya vyema zaidi ili niweze kushinda. Naamini kwa uwezo wa Mungu nitashinda tu.
“Pia kwa nafasi ya pekee, ninaushukuru uongozi wa Global Publishers kwa kuandaa shindano hili. Hakika mmegusa viini vya mioyo ya wengi.”
MOSI RAINA KILONGOSI (28)
“Taarifa za shindano hilo niliziona katika mabandiko yaliyokuwa yamebandikwa katika chuo cha Biashara (CBE).
Sikuweza kuchukua fomu kwa wakati hadi siku ya mwisho, ndipo nilipofanikiwa tena kwa kukopeshwa fedha.
Matarajio yangu ni kujifunza ili nipate ujuzi utakaonifanya niwe mzungumzaji mzuri. Pia shindano hili linaniwezesha kutengeneza marafiki wapya wengi.
“Haikuwa rahisi sana kufika 30 bora kwa sababu ushindani ulikuwa mkubwa. Ila namshukuru Mwenyezi Mungu licha ya changamoto za muda mdogo wa maandalizi, lakini nimepenya raundi hii.”
BARAKA MWILAPWA KONKARA (28)
Ni mkazi wa Sinza Dar es Salaam na mhitimu wa Shahada ya Mawasiliano kwa umma na masoko kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Ni muandaaji wa matukio kupitia kampuni ya Sonetra communications & sports agency.
“Nilipata taarifa za shindano kupitia mitandao ya Global Publishers pamoja na Global TV Online. Pia rafiki yangu aliona mtandaoni.
Nilihamasika kushiriki shindano hili hasa pia kwa kupitia rafiki yangu ambaye alinihamasisha kwa kuwa anajua uwezo wangu wa kuzungumza mbele ya hadhara.
“Nilijaza na kurejesha fomu tarehe za mwishoni, ila nilishangazwa na mwitikio wa wingi wa washiriki niliowaona siku ya kwanza.
“Ninafurahi kushiriki shindano hili kwa kuwa majaji waligundua madhaifu yangu na kunipa mbinu za kuniboresha zaidi.
“Matarajio yangu ni kuwa mshindi na kuwa kioo cha wazungumzaji ndani na nje ya nchi.”
MAKALA: MWANDISHI WETU