The House of Favourite Newspapers

NAY WA MITEGO NA WEWE UNATAKA KIKI

0
Emmanuel Elibariki ‘Nay wa Mitego’

 

NI True Boy tena, Emmanuel Elibariki maarufu kwa jina la Nay wa Mitego. Safari hii amekuja na kibao chake kipya, Moto ambacho kama ilivyo kawaida yake, ndani amewaponda wasanii wenzake, akiwataja kimafumbo, ambayo kwa wanaofuatilia Muziki wa Kizazi Kipya wanaelewa anamzungumzia nani. Lakini achana na mafumbo kwa wasanii wenzake ambayo ni kama alama yake kimuziki, kwa mara nyingine tena, ameweka maneno mengi yenye viashiria vya matusi, hata kama siyo moja kwa moja, ila kwa watoto wa mjini, wanaelewa.

 

Maneno kama Wapumbavu na Kula kiboga, siyo maneno yenye tafsiri nzuri, hasa yanapotamkwa na mtu anayesemwa kuwa ni kioo cha jamii. Nirejee tena, mimi ni shabiki wa Nay. Napenda namna alivyojitengeneza kwa aina yake ya muziki. Lakini kama mwandishi, ninatofautiana naye kwa namna anavyojaribu kuharibu taswira yake kama msanii mkubwa.

 

Nay ni mwanamuziki mzuri, anayejua vizuri kuitumia sauti yake na hata aina ya midundo anayokwenda nayo, inamfaa kwa kiwango chake. Sijui, huenda ndiyo kiki au hulka, lakini namuona ni kama msanii ambaye anatumia nguvu kubwa kutoka nje ya mstari kuliko kukaa kwenye line! Utakumbuka ile hatua ya kukamatwa kwake kwa ujio wa wimbo wake wa Wapo.

 

 

Kama si busara ya Rais Dk. John Magufuli, leo hii tungezungumza kuhusu mambo mengine. Hii siyo sawa, ni mtu gani anajiweka matatizoni kila mara kwa kuzungumza mambo binafsi ya watu ambayo hayana tija kwa taifa? Kama hulka ya Nay ni mtu mkweli, anayeguswa, mbona mashabiki wake wana kero nyingi tu? Kwa nini haimbi kuhusu tabia ya wanasiasa kujipa uungu mtu wa kutaka mawazo yao ndiyo yaheshimiwe kuliko wengine.

 

Wanapata wapi ujasiri wa kujitamkia tu mtu aswekwe lupango kwa sababu tu hawakupendezwa na maoni ya watu wengine? Mbona haimbi juu ya mashabiki wake wanaouziwa vyakula feki katika maduka makubwa au hata uswahilini. Vipi kuhusu nyimbo zenye kuwalenga wahubiri wapigaji wanaozidi kumiminika kila siku hapa nchini? Kama ishu ni kuimba vitu vya ukweli, hakuna haja ya kutaja majina ya wasanii wenzake ambao kimsingi hawana madhara yoyote kwa jamii zaidi ya kujipa tabu wao wenyewe.

 

Watu wanalalamika maisha magumu, bei za vyakula zinapanda, gharama za maisha zinakuwa juu, lakini mishahara imebaki ileile. Kama ni ukweli, haya ndiyo mambo ya kuimba ili wahusika wasikie na wafanyie kazi, kusudi mashabiki wake wafaidike na hili litakuwa ni jambo jema, lakini anachokifanya hakina tofauti na kile ambacho wenzake wanasema kiki

 

Young D.

 

Kwani kwa mfano, kufifia kimuziki kwa mtu kama Young D, kuna faida gani kwa shabiki ambaye anaishi Nyamongo, ambaye kila siku anakimbizwa na askari wa migodini anapojitafutia mkate wake?

 

Nay, wewe ni msanii mkubwa kutokana na uwezo wako wa kazi na kwa maana hiyo, hizi kiki za kitoto ungeachana nazo, matusimatusi na maneno yasiyo na maana yanapaswa sasa yasemwe na wasanii vijana wanaotafuta kiki ya kutoka. Kila mtu huzaliwa, kutambaa, kutembea na hatimaye kukimbia na katika hatua zote hizo zina tabia zake.

 

Ni jambo la kuchekesha sasa kwa mtu kuishi na tabia za mtoto anayetambaa wakati ni mtu mzima anayekimbia mwenyewe. Mtu anayejua anachofanya, hawezi kutumia kiki ili kuhit, tunataka kazi mambo ya kitoto waachwe watoto washughulike nayo.

Rais Magufuli Aruhusu Wimbo WAMO wa Nay Upigwe Redioni Licha ya Kuiponda Serikali

Leave A Reply