The House of Favourite Newspapers
gunners X

NBC Yaunga Mkono Ujenzi wa Kituo cha Abiria cha Vivuko cha Maruhubi Zanzibar

0
Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imesisitiza dhamira yake ya kuendelea kuunga mkono maendeleo ya kiuchumi ya Zanzibar kupitia ufadhili wa miradi mikubwa ya kimkakati ya miundombinu, baada ya kuunga mkono ujenzi wa Kituo cha Abiria cha Vivuko cha Maruhubi (Mpiga Duru) kupitia mkopo rafiki. Ukamilishwaji wa kituo hicho unatarajiwa kuimarisha sekta za utalii, biashara na usafirishaji katika visiwa hivyo.
NBC, ikiwakilishwa na Mkurugenzi wa Idara ya Wateja Wadogo na Wakubwa, Bw. Elibariki Masuke, leo ilishiriki katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho, hafla iliyoongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdullah.
Kituo cha Abiria cha Vivuko cha Maruhubi kinajengwa kupitia mfumo wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) kati ya Shirika la Bandari Zanzibar na Kampuni ya Zanzibar Ferry Development Company Limited. Mradi huu unalenga kupunguza msongamano katika Bandari ya Malindi na kuboresha ufanisi wa usafiri wa abiria, ambapo baada ya kukamilika, kituo kinatarajiwa kuhudumia takribani abiria 8,000 kwa siku, sawa na karibu abiria milioni tatu kwa mwaka.
Kituo hicho cha kisasa kitahudumia vivuko vya abiria, vivuko vya kasi, meli za Roll-on/Roll-off pamoja na teksi za baharini. Pia kitajumuisha eneo la bidhaa zisizotozwa ushuru (duty-free), maduka ya rejareja, marina na kituo cha ndege za baharini (seaplane), hatua itakayoiimarisha Zanzibar kama kitovu cha kikanda cha usafiri wa baharini na utalii.
Mradi huo unakadiriwa kugharimu takribani dola za Marekani milioni 400 na utatekelezwa kwa awamu mbili ndani ya kipindi cha miaka mitatu, huku Benki ya NBC ikiwa miongoni mwa wafadhili wakuu wa mradi huo.
Akizungumza pembezoni mwa hafla hiyo, Bw. Masuke alisema NBC inajivunia kuunga mkono mradi unaoendana na vipaumbele vya maendeleo ya Zanzibar.
Leave A Reply