The House of Favourite Newspapers

NBC Yazindua Kadi Uanachama Msalaba Mwekundu, Dkt Biteko Aguswa na jitihada zake

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Dotto Biteko amepongeza jitihada za Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) kuunga mkono jitihada za serikali katika kuongeza ujumuifu katika huduma za kifedha (financial inclusion) sambamba na kusaidia ufanikishaji wa miradi mikubwa ya kitaifa ukiwemo ujenzi wa miundombinu ya maji Mkoani Tanga kupitia hati fungani ya kijani iliyosimamiwa na benki hiyo.

Dkt Biteko alitoa pongezi hizo mwishoni mwa wiki alipotembelea banda la benki hiyo lililokuwa kwenye viunga vya ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma ambapo yalifanyika Maadhimisho ya miaka 62 ya Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania. Dkt Biteko alimuwakilisha Rais Samia Suluhu Hassani kwenye maadhimisho hayo ambayo pia yalihusisha uzinduzi wa kadi mpya za Kielectronic za wanachama wa chama hicho kupitia benki ya NBC.

Akizungumza mara baada kupokea taarifa ya Meneja wa Kanda ya Kati wa benki ya NBC Miraji Msuya kuhusu jitihada mbalimbali za benki hiyo katika kuhudumia jamii ukiwemo usimamizi wa hati fungani ya kijani ya ujenzi wa miundombinu ya maji Mkoani Tanga na utambulisho wa kadi mpya za Kielectronic za wanachama wa chama cha Msalaba Mwekundu, Dkt Biteko aliipongeza benki hiyo kwa jitihada hizo huku akitoa wito kwa taasisi za fedha nchini kuendelea kushirikiana na serikali kubuni huduma mbalimbali zinazolenga kuwakwamua wananchi kwenye changamoto zinazowakabili.

 “Niwapongeze sana NBC kwa jitihada hizi na wito wangu kwa taasisi za fedha ni wao kuendelea kushikirikiana na serikali katika utekelezaji wa miradi mbalimbali inayolenga kutatua changamoto za wananchi kama ujenzi wa miundombinu ya maji pamoja na kuendelea kuvutia wananchi wengi zaidi waingine kwenye mfumo rasmi wa huduma za kifedha,’’ alisema.

Dkt Biteko pia aliongoza zoezi la uzinduzi wa kadi mpya za Kielectronic za wanachama wa chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania kupitia benki ya NBC akiwa sambamba na viongozi wengine waandamizi wa serikali wakiwemo mawaziri, viongozi waandamizi wa Chama cha Msalaba wakiongozwa na Rais wa chama hicho ambae pia ni Naibu Waziri wa Uchukuzi David Kihenzile pamoja na maofisa wa benki hiyo wakiongozwa na Meneja wa Kanda ya Kati wa benki ya NBC Miraji Msuya.