The House of Favourite Newspapers

NBC Yazindua Mwezi wa Huduma kwa Wateja kwa kuwatembelea Mawakala, Wateja

0
Mkurugenzi wa Wateja wadogo na Binafsi wa Benki ya NBC Elibariki Masuke akizungumza na wafanyakazi, mawakala wakubwa na wadogo wa benki hiyo wakati viongozi na wafanyakazi wa benki hiyo walipotembelea wakala mkuu wa benki hiyo eneo la Goba, jijini Dar es Salaam leo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya mwezi wa huduma kwa wateja wa benki hiyo.

Benki ya Taifa ya Biashara imetumia maadhimisho ya mwezi wa huduma kwa wateja kwa kuwatembelea mawakala mbalimbali na wateja wa benki hiyo katika maeneo mbalimbali ili kuthibitisha na kutambua thamani na mchango wa wadau hao muhimu katika kuwahudumia wateja na ukuaji wa uchumi kwa ujumla.

Zoezi hilo la kuwatembelea wadau hao limefanyika mapema leo jijini Dar es Salaam likihusisha wafanyakazi wakiongozwa na viongozi waandamizi wa benki hiyo akiwemo Mkuu wa Uendeshaji NBC Bi. Alelio Lowassa, Mkuu wa Kitengo cha Compliance NBC Bi Sarah Laiser, Mkuu wa Kitengo cha Uwakala Bw Gaudence Shawa na Mkurugenzi wa Wateja wadogo na Binafsi wa Benki ya NBC Elibariki Masuke  aliemuwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi.

Elibariki Masuke  (wa pili kulia) akimkabidhi zawadi mmoja wa wakala mkuu wa benki hiyo Bi Beatrice Shayo wa eneo la Goba, jijini Dar es Salaam ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wa huduma zinazotolewa na wakala huyo kwa wateja wa benki hiyo na ukuaji wa uchumi kwa ujumla. Hatua ya benki hiyo ni sehemu ya maadhimisho ya mwezi wa huduma kwa wateja ambapo benki hiyo iliwatembelea mawakala na wateja wa benki hiyo katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam leo. Wanaoshuhudia ni pamoja na Mkuu wa Uendeshaji NBC Bi. Alelio Lowassa (Kulia) na Mkuu wa Kitengo cha Uwakala Bw Gaudence Shawa (Kushoto)

Akizungumza kwenye tukio hilo lililohusisha maeneo ya Goba, Sinza na Tandale, Bw Masuke aliesema hatua ya benki hiyo kuelekeza maadhimisho hayo kutambua zaidi mchango wa mawakala wa benki hiyo ni kutokana na kuthamini kazi kubwa inayoendelea kufanywa na mawakala hao katika kuwahudumia wateja kwa ukaribu, uaminifu na kwa weledi wa hali juu.

“Tumeona tuyatumie maadhimisho haya kwa kuwatembelea mawakala wakuu sambamba na baadhi ya mawakala wadogo bila kuwasahau wateja wetu ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wao muhimu kwa ustawi wa benki na uchumi kwa ujumla na hiyo ndio sababu kauli mbiu yetu ni NBC Timu Huduma kwasababu huduma zetu tunazitoa kama timu.’’

Mkuu wa Kitengo cha Compliance NBC Bi Sarah Laiser, (wa tatu kushoto) akimkabidhi zawadi mmoja wa wateja wa benki hiyo Bi Jacquelene Madili (kulia) ambae ni Mkurugenzi wa duka la vifaa vya nyumbani la Jaden Home Store lililopo Sinza jijini Dar es Salaam  ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya mwezi wa huduma kwa wateja ambapo benki hiyo iliwatembelea mawakala na wateja wa benki hiyo katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam leo.

“Mawakala hawa wameonyesha weledi,uaminifu wa hali ya juu na hivyo wamekuwa wakitoa huduma kwa ukaribu zaidi hata katika maeneo ambayo matawi yetu hayajafika tena kwa viwango vilevile kama ambavyo tunatoa huduma kwenye matawi yetu mengine. Hivyo tumeona wanastahili heshima hii sambamba na zawadi mbalimbali ambazo tumewapatia hii leo tukilenga kuwahamasisha na kuwahimiza kufanya vyema zaidi katika majukumu yao. ,’’ alibainisha.

Kwa mujibu wa Bw Masuke pamoja na mtandao mpana wa takribani mawakala 12,000 wa benki hiyo kote nchini, bado benki hiyo inaendelea na mkakati wake wa kufungua matawi mapya katika maeneo mbalimbali nchini ili kurahisisha huduma kwa wateja na  mawakala hao.

“Tumeona tuyatumie maadhimisho haya kwa kuwatembelea mawakala wakuu sambamba na baadhi ya mawakala wadogo bila kuwasahau wateja wetu ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wao muhimu kwa ustawi wa benki na uchumi kwa ujumla na hiyo ndio sababu kauli mbiu yetu ni ‘NBC Timu Huduma’  kwasababu huduma zetu tunazitoa kama timu.’’ – Elibariki Masuke | Mkurugenzi wa Wateja wadogo na Binafsi wa Benki ya NBC

Akizungumza na baadhi ya wateja waliotembelewa na benki hiyo Mkuu wa Kitengo cha Compliance NBC Bi Sarah Laiser aliwashukuru wateja hao kwa kuendelea kuiamini benki hiyo huku akiahidi kuendeleza ushirikiano huo sambamba na kubuni huduma mbalimbali zinazolenga kurahisisha huduma zinazotolewa na wateja hao zikiwemo huduma za malipo.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Huduma kwa Wateja wa Benki ya NBC,Bi Salama Mussa aliwashukuru mawakala na wateja wa benki hiyo kwa mchango wao katika kufanikisha ustawi wa benki hiyo sambamba na kupongeza ustawi wa biashara zao kufuatia huduma za kisasa zinazotolewa na benki hiyo. Aliahidi kwa niaba ya benki hiyo kuendelea kutoa huduma bora zitakazokidhi mahitaji ya wakati uliopo na ujao wa wateja na mawakala hao.

Kwa upande wao Mawakala na wateja waliotembelewa walitoa shukrani zao za dhati kwa huduma na  ushirikiano unaoendelea kutolewa na benki hiyo huku wakiipongeza benki hiyo kwa namna inavyeondelea kubuni huduma zinazolenga kutatua changamoto za wateja sambamba na kuwapatia elimu ya mara kwa mara inayolenga kuwajengea uwezo katika kutumia huduma mbalimbali zinazotolewa na benki hiyo.

“Imekuwa ni heshima kubwa kwetu kwa kutambuliwa na Benki ya NBC. Utambuzi huu unatupa motisha ya kufanya kazi nzuri zaidi kwa wateja wetu, kuhakikisha tunawapa huduma bora iwezekanavyo. Zaidi tunawashukuru sana NBC kwa huduma zao kwetu sisi mawakala wakuu ikiwemo huduma ya ulinzi masaa 24, huduma ya kuongeza mitaji yetu yaani ‘Wakala boost’ sambamba na mafunzo mbalimbali kuhusu huduma zao ikiwemo huduma ya Bima” alisema Bi Beatrice Shayo, Wakala Mkuu wa benki hiyo, eneo la Goba.

Naye mmoja wa wateja wa benki hiyo Bi Jacquelene Madili Mkurugenzi wa duka la vifaa vya nyumbani la Jaden Home Store aliishukuru benki hiyo kwa huduma zake kwa wateja huku akionyesha kuvutiwa na huduma ya malipo ya POS inayotolewa na benki hiyo kutokana na namna inavyorahisisha huduma za duka hilo kwa wateja wake.

Leave A Reply