The House of Favourite Newspapers

Ndalichako: Mitihani Kidato cha Sita na Ualimu Itaanza Juni 29

0

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, amesema mitihani ya kidato cha sita nchini itaanza Juni, 29 na kukamilika Julai 16, mwaka huu.

 

Akizungumza leo na waandishi wa habari jijini Dodoma, Ndalichako amezitaka shule zote zenye wanafunzi wa kidato cha sita kufanya maandalizi ili masomo yaanze Juni Mosi, mwaka huu kama alivyotangaza Rais John Magufuli.

 

“Wanafunzi watakapofungua shule waendelee na masomo kama kawaida na Juni 29, mwaka huu wataanza mitihani na watamaliza Julai 16, mwaka huu,”amesema.

 

Ametumia fursa hiyo kuliagiza Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) kusambaza mitihani hiyo mara moja, lakini pia kuhakikikisha matokeo yanatoka kabla ya Agosti 30, mwaka huu ili wanafunzi watakaofanya vizuri wapate muda wa kutuma maombi vyuo vikuu bila kuathiriwa na muda.

 

Kuhusu Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Vyuo Vikuu amesema tayari bodi hiyo ina fedha kiasi cha sh.bilioni 122.8 kwa ajili ya wanafunzi wenye sifa ya kupata mikopo hiyo.

 

Amesema kinachotakiwa ni vyuo kuwasilisha nyaraka muhimu huku akisema hadi Mei 28, mwaka huu nyaraka hizo ziwe zimewasilishwa Bodi ya Mikopo ili itoe fedha hizo mara tu wanafunzi wanapofika vyuoni.

 

“Mara nyingi ucheleweshaji huwa unatokea vyuoni, tunaomba nyaraka ziwahi maana fedha zipo,” amesema.

 

Amevitaka vyuo vijipange na kuweka maafisa wa kutosha kufanya malipo ili kukimbizana na muda. Pia amewataka wanafunzi nao kuwasilisha nyaraka zao muhimu ili wapatiwe fedha. Aidha, amevitaka vyuo na shule kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa corona kwa kuweka ndoo za maji na sabuni katika maeneo mbalimbali.

 

 

Leave A Reply