NDANI YA MWEZI MTUKUFU… BINTI AKIONA CHA MOTO

MOROGORO: Wakati waislam wakiwa ndani ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, binti mmoja aliyefahamika kwa jina la Sharifa mkazi wa Mji Mpya mkoani Morogoro, juzikati alikiona cha moto baada ya kutuhumiwa kuiba kiasi cha shilingi 120,000 kwa wakala aliyefahamika kwa jina la Ally Lusanga.

 

Tukio hilo lililoshangaza wengi hasa kutokana na muonekano wa binti huyo, lilitokea Mtaa wa Misufini Kata ya Mafiga Manispaa ya Morogoro ambapo inaelezwa kuwa, kama si huruma ya baadhi ya watu, mauti yangeweza kumfika.

Awali mwandishi wa habari hii alipigiwa simu na msamaria mwema na kuelezwa kuwa, kuna dada alikuwa akipewa kichapo kwa madai ya kuchikichia pesa za watu.

 

“Kiongozi njoo haraka hapa Mtaa wa Msufini kuna dada anapigwa, alitaka kutapeli pesa kwa wakala mmoja hapa, wee njoo fasta uchukue tukio,” mtoa habari huyo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini alimtaarifu paparazi wetu.

 

Kufuatia tipu hiyo, paparazi wetu alichukua usafiri wake wa bodaboda na kuwahi eneo la tukio ambapo alipofika alimkuta mdada huyo akiwa chini ya ulinzi huku akiwa amechakazwa kwa kichapo.

 

Akihojiwa na gazeti hili Wakala Lusanga alisema: “Huyu dada alifika hapa akanipa namba akiomba nimtumie pesa ndugu yake laki moja na elfu ishirini, kimsingi sikutegemea kama mrembo huyu ni tapeli, nikaamua kutuma hiyo pesa.

“Nilipomaliza kutuma pesa na kumtaka anipe pesa yangu, akawa anajifanya kumpigia ndugu yake ambaye alidai eti pesa hiyo haijafika kwake huku akiondoka hapa dukani, nikatoka na kumfukuza huku nikimwitia mwizi na ndipo wananchi wenye hasira wakamkamata na kumpa kipigo kikali,” alisema wakala huyo.

 

Mwandishi wetu alimshuhudia dada huyo akiwa amevimba uso na hata alipotakiwa kuongea lolote alishindwa ndipo watu waliokuwa eneo hilo walipomchukua na kumpeleka polisi kwa taratibu za kisheria.


Loading...

Toa comment