Ndege Iliyozuiliwa Sauzi Yatua Dar, Rubani Asimulia – Video

NDEGE ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) aina ya Airbus A220-300 iliyokuwa ikishikiliwa nchini Afrika Kusini, iliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam majira ya saa 2:30, usiku baada ya kuachiliwa huru na Mahakama Kuu ya Gauteng chini ya Jaji Lamont nchini Afrika Kusini.

 

Ndege hiyo iliwasili kutoka katika Uwanja wa Ndege wa OR Tambo jijini Johannesburg ikiwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Dk. Damas Ndumbaro na wanasheria wa Serikali baada ya Mahakama hiyo kutupilia mbali tena ombi jingine la Steyn aliyetaka, pamoja na uamuzi wa awali leo, ndege iendelee kushikiliwa hivyo ndege hiyo kukabidhiwa kwa Serikali ya Tanzania.

 

ATCL imesema kuwa safari za ndege hiyo kuelekea Afrika Kusini zitarejea siku ya Ijumaa huku Waziri Ndumbaro aliyekuwepo mahakamani akisema kuwa Tanzania imeridhishwa na uamuzi wa mahakama.

Ndumbaro pia amesisitiza kwa kuwa serikali ya Tanzania imeshamlipa Steyn dola milioni 20, maana yake wapo tayari kumalizia bakaa ya deni, lakini mkulima huyo “anatakiwa kurudi katika mahakama za Tanzania, na aache kuihusisha Afrika Kusini.”

 

Jaji aliyesikiliza rufaa amesisitiza kuwa Afrika Kusini haina mamlaka ya kisheria (jurisdiction) ya kuliamulia jambo hilo.

Kwa nini ndege ilizuiliwa?

Ndege hiyo aina ya Airbus A220-300 ilikuwa imeshikiliwa katika uwanja wa Oliver Tambo jijini Johannesburg kwa amri ya mahakama. Hermanus Steyn alifungua kesi ya fidia dhidi ya serikali ya Tanzania.

 

Steyn alikuwa anamiliki ardhi, mifugo na mali nyingi ambazo zilitaifishwa na serikali ya Tanzania miaka ya 1980. Ilipofika miaka ya 1990 walikubaliana fidia atakayolipwa, kwa ujumla wake dola milioni 33 na tayari ameshalipwa dola milioni 20 kati ya hizo.

 

Hata hivyo, katika miaka ya hivi karibuni, serikali ya Tanzania, kwa mujibu wa mkulima huyo imeacha kulipa deni hilo, na hatua ya kuomba ndege kushikiliwa ilikuwa moja ya harakati zake za kutaka kumaliziwa deni.

TAZAMA NDEGE HIYO IKIWASILI


Loading...

Toa comment