The House of Favourite Newspapers

Ndege Zagongana Angani, B-52 Yaangusha Mabomu ya Nyuklia

0
Bomu la nyuklia B-52.

 

NI miaka ipatayo 50 iliyopita wakati wa Vita Baridi baina ya nchi za Mashariki na Magharibi, yaani baina ya nchi za kibepari na za kikomunist zilizokuwa zinahasimiana, kila upande ukitaka kusambaza itikadi yake duniani.

Wakati huo, kama ilivyokuwa kwa zana na majeshi yote ya kivita, ndege za Marekani na washirika wake, na za Urusi na washirika wake, zilikuwa ‘zinazurura’ kila mahali katika anga la dunia hususan katika eneo lililozigawa nchi za Magharibi na Mashariki barani Ulaya.

 

Huko ndiko kulikuwa kumelimbikizwa silaha zote za maafa na ambako majeshi ya anga, ardhini na majini yalikuwa yanakabiliana kwa tukio lolote la kivita wakati wowote. Hali hiyo inaendelea hadi leo japokuwa silaha zimepunguzwa.

Ndege 12 za Marekani zikiwa zimebeba mabomu ya nyuklia muda wote zilizunguka anga la Ulaya tayari kwa vita dhidi ya Urusi na washirika wake pindi ikitokea.

 

Siku ya Januari 17, 1966, wasiwasi ulimwenguni uliongezeka pale ndege mbili za Marekani, moja ya kivita B-52 na ya kubebea mafuta aina ya KC-135 (tanker), zilipogongana angani wakati B-52 inajiweka sawa hukohuko angani chini ya tumbo la ‘tenka’ hiyo, ili iweze kujazwa mafuta juu ya pwani ya kusini mwa Hispania.

Ndege hiyo iliyokuwa na mabomu manne ya nyuklia (hydrogen) na ikiwa imetokea North Carolina nchini Marekani kwa kukatiza kwa kasi Bahari ya Atlantic, ikagongana na ile ya kujaza mafuta na zote zikalipuka na kutawanyika ambapo watu saba walikuwa na mabomu ya nyuklia yakaponyoka kwenye B-52 ambapo matatu yakaanguka katika Kijiji cha Palomares, Hispania, na moja likaanguka katika Bahari ya Mediterranean.

 

Bomu la nyuklia B-52.

 

 

Rubani wa B-52 Meja Larry Messinger, Wendorf na wengine wawili, walirushwa nje na mitambo maalum ya kujiokoa ya ndege hiyo kabla haijatawanyika, lakini watu wengine waliokuwemo waliuawa.

Watu wanne wote waliokuwa katika KC-135 waliangamia baada ya kulipuka kwa moto ambapo mabaki ya ndege hizo yalianguka katika kijiji cha walima nyanya cha Palomares, Hispania, ambapo pia na Wamarekani wanne waliorushwa kutoka B-52 walianguka na kuokolewa na kupelekwa hospitali.

 

Mabaki hayo ya ndege kijijini hapo hayakumdhuru mtu yeyote, lakini wakazi wake hawakujua kulikuwa kumeanguka pia mabomu manne ya hydrogen, moja likiwa limeangukia baharini.

Mabomu hayo ambayo kwa bahati hayakulipuka, yalikuwa na nguvu ya uharibifu mara 70 zaidi ya bomu la nyuklia la Marekani lililotupwa Hiroshima, Japan wakati wa Vita Kuu ya Dunia.

 

Ndipo zikaanza juhudi za siri za Marekani na Hispania kuyatafuta kimyakimya mabomu hayo. Eneo lote la Palomares likajaa askari na raia kibao wa Marekani ambao hawakusema walichokuwa wakikitafuta ambapo mabomu matatu yaliyoanguka ardhini yalipatikana bila matatizo makubwa. Tatizo likawa kulipata lililoanguka katika Bahari ya Mediterranean!

Hata hivyo, ilipofika Machi 2 bila kuliona, Marekani ilikiri ilikuwa inatafuta bomu la nyuklia nchini Hispania lakini ikakana madai ya Urusi kwamba bomu hilo lingeyatia sumu ya mionzi ya nyuklia maji ya bahari hiyo.

 

Kazi hiyo iliendelea hadi Machi 14, 1966 nyambizi ya Alvin ilipoliona bomu hilo la nne likiwa mita 762 chini ya bahari.

Mitambo na mashine mbalimbali zililetwa Machi 26 kulivuta lakini kamba za kulivutia zilikatika na likapotelea majini tena hadi nyambizi Alvin ilipoliona tena Aprili 2 ambapo Aprili 7, 1966 bomu hilo lilitolewa majini – kiasi cha miezi mitatu baada ya kuangukia humo.

 

Lilibebwa na kuwekwa katika meli ya kivita ya USS Petrel ambapo waandishi wa habari waliruhusiwa kulipiga picha, ikiwa ni mara ya kwanza kwa Marekani kuonyesha hadharani silaha ya nyuklia.

Mwandishi: Walusanga Ndaki | RISASI JUMAMOSI | Nakujuza Zaidi

Leave A Reply