Ndi Ndi Ndi ya Zuchu Sijui Yatakuwaje

ZIMEBAKI siku chache kabla ya kwenda kushuhudia usiku wa mahaba ndi ndi ndi kutoka kwa muimbaji kutoka lebo ya WCB, Zuchu.
Zuchu anatarajia kufanya shoo Februari 14, kwenye ukumbi uliopo Mlimani City ikiwa ni siku ambayo dunia itaazimisha siku ya wapendanao.
Shauku imekuwa kubwa sana kuelekea kwenye usiku huo, kwani kila mmoja anajiuliza mambo yatakuwaje, kwa kuwa wengi wanahisi siku hiyo Zuchu ataweka wazi mahusiano yake.
Stori kubwa iliyopo mtaani ni kwamba Zuchu anatoka na Diamond Platinumz ambaye pia ndiye bosi wake. Wengi wanahisi siku hiyo watavishana pete.
Akizungumzia juu ya usiku huo utakavyokuwa, Zuchu alisema: “Mimi mwenyewe sijui hiyo siku ya mahaba ndi ndi ndi itakuwaje, kwa kuwa kuna vingi sana vitatokea usiku huo.
“Watu wanatakiwa kuja na wale ambao wanawapenda na kushuhudia mahaba ndi ndi ndi yatakuwaje. Sapraiz zitakuwa za kutosha sana.”
Zuchu kwa sasa anatamba na mkwaju wa Mwambieni ambao huko YouTube unakimbiza kinoma ukiwa umegonga views zaidi ya milioni 1.3 kwa muda wa siku mbili tu.

