The House of Favourite Newspapers

Ndoa na Shetani-9

0

ILIPOISHIA:
Nilijua lazima bwana yule atafanya kweli kutokana na taarifa za matukio ya wanajeshi, niliwahi kusikia mwanajeshi amemuua mke wake na yeye kujilipua. Ilibidi niwe mpole ili nitunge uongo wa kumuokoa yule bwana. Lakini kibaya zaidi yule mwanajeshi alikuwa amelewa lazima angefanya alichokidhamiria.
“Basi mpenzi taratibu,” nilisema kwa sauti ya kubembeleza.
SASA ENDELEA…

“Pumbavu mpenzi wako nani?” Jamaa alikuwa mjanja nilijua kazi ninayo.
Kabla sijajua nifanye ujanja gani, kofi zito lilitua kisogoni na kunifanya nione kiza mbele. Nilisikia akisema:

“Unataka kunichezea, leo ndiyo utanijua mimi ni nani! Wanangu walikuwa wanalala na njaa kwa ajili yako, wengine wapo nyumbani kwa kukosa ada ya shule wewe unaleta mchezo.”

Jamaa alisema kwa hasira mpaka povu likaanza kumtoka mdomoni. Ilionesha alikuwa na uchungu na mimi kwa muda mrefu na siku ile ndiyo nilikuwa nimeingia anga zake hivyo ningejuta kuzaliwa.
Mmh! Shughuli ilikuwa pevu lazima nilijua amepania kuua, sikukata tamaa na kusema:
“Sikuja na mtu, nipo peke yangu.”

“Konso..Konso, unataka nikumwage ubongo sasa hivi yule aliyeingia ndani ni nani? Unafikiri sijakuona kwa usalama wako nipeleke kwa hiyari.”
Mpaka kufikia hatua ile na maneno aliyokuwa akiyaongea na pombe alizokuwa amekunywa. Niliamini lazima angefanya kitendo cha kihistoria cha kumuua yule bwana na kuniua mimi kisha kujimaliza mwenyewe.

Sikuwa na jinsi, nilijikuta nikisema kwa sauti ya upole baada ya kuona kuwa nimepatikana mtoto wa kike ambaye kila kukicha siishi visanga.
“Basi niache nikupeleke.”
“Sasa ulikuwa unakataa nini.”
“Si nimekubali.”

“Haya tangulia, ukifanya ujanja nakumwaga ubongo.”
Nilianza kuongoza chumba tulichokuwa kwa kuogopa kufanya ujanja wowote nitaambulia kipigo. Tukiwa tunakata kona kuingia upande wa vyumba tulikutana na watu wakikimbizana.
Walikuja na kupita katikati yetu na kutusukuma kitu kilichofanya bastola ya yule mwanajeshi kuanguka. Kwa vile akili yangu ilikuwa ikifanya kazi kama kompyuta, kitendo kile kilinipa wazo la haraka, bila kuchelewa nilitimua mbio kukimbilia nje kupitia katikati ya kundi la watu.

Nilikimbia kwa nguvu zote, nilisikia mlio wa risasi kwa nyuma, sikugeuka hata nilipotoka nje ya hoteli niliendelea kutimua mbio kwa mwendo wa robo saa wakati huo nilikuwa pekupeku, miguu yote ilikuwa na majeraha kwa kujikwaa njiani wakati wa kukimbia na kuanguka.

Pamoja na kukimbia umbali mrefu bado nilikuwa siamini kama nimeokoka. Nikiwa nahema ovyo, niliona gari likija niliamua kulipungia mkono ili linipeleke nyumbani. Baada ya kusimama nilimwambia dereva anipeleke nyumbani dereva aliniuliza;
“Vipi sista kuna usalama?”
“Siyo muhimu kujua la muhimu niwahishe nyumbani”
“Hela unayo?”

“Hata ya kukulisha wewe na mkeo,” nilijikuta nikijibu kwa hasira.
“Ni majibu gani hayo sista?” dereva naye alinijia juu.

“Umeyataka mwenyewe,” jibu lilimziba mdomo na kukaa kimya aliponifikisha nyumbani, niliingia ndani kumchukulia pesa na nilitoka kumlipa dereva wa teksi baada ya kuliacha pochi langu hotelini.
Siku hiyo sikulala, mawazo yote yalikuwa juu ya tukio lililonitokea maana lilikuwa la pili. La kwanza nilipata kipigo na mpenzi wangu ambaye alivunjwa mbavu na kuwapoteza watu muhimu kwangu Bantu na Abdul. Lakini la siku ile lilikuwa kubwa. Nilikuwa napoteza maisha ya bwana’angu ambaye najua familia yake ingeathirika kwa namna moja au nyingine pamoja na mimi mwenyewe.

Nilijua kama nitaendelea na mwendo ule lazima mwanajeshi ataendelea kunitafuta na akinikamata lazima animwage ubongo. Ilibidi nibadili tabia yangu ambayo mwenendo wake unatishia maisha yangu. Lakini sikutaka kuachana na waume za watu kwa kujua wengi niliokuwa nao ni wastaarabu.

Niliamua kubadili mtindo wa kukutana nao nyumbani kwangu kwa kujua nitakuwa nimejiepusha na yule mwanajeshi ambaye dhamira yake ilikuwa mbaya, kumkataa ilikuwa nongwa kama angekuwa mstaarabu kama wenzake nisingekuwa na haja ya kumkataa. Eti nimesababisha maisha yake yayumbe, nilimwita?

Kuipima injini ya pikipiki kwenye semitrella kama siyo kuipasua injini ni nini. Mwanaume aliyetaka kula raha na mimi alitakiwa asiwe na fedha za mawazo, za mkopo au kusubiri mwisho wa mwezi lazima utachemsha na kuniona mwanga wako kama mwanajeshi.

Mpango wangu wa kukutana na mabuzi yangu kwangu ulikwenda vizuri kwa kila mmoja kuja kwa wakati wake na siku ambayo anapangiwa. Kwa kweli nilijikuta kumbe mpango ule ningeutumia mapema mbona masahibu ya kutokea kwenye tundu la sindano yasingenikuta.

Mambo yaliniendea vizuri, sikuwa na presha tena pesa ziliingia kama maji kwa vile kila mwanaume aliyekuja kwangu alichanganyikiwa kunikuta mtoto wa kike nipo sawa hata fedha waliyotaka kuniachia waliiacha kulingana na hadhi yangu, pia hapa penzi alilopata lilikuwa geni machoni mwake.

Niliamini mwanajeshi kila kukicha alizunguka kwenye mabaa na hoteli kunisaka ili animwage ubongo. Kwa mtaji ule nilijua angeng’aa macho mpaka yaote kengeza kwa kunitafuta. Nilishukuru wakati wa penzi letu sikuwahi kumuonesha kwangu mbona ningekoma.
****

Siku moja nikiwa natoka kufanya shopping supermarket nilivamiwa na watu ambao waliniteka na kuniingiza kwenye gari na kuondoka na mimi. Mmh! Moyoni nilijua lazima watakuwa wametumwa na mwanajeshi kama itakuwa yeye nilijua nimekwisha.

Nilifungwa kitambaa usoni na kushindwa kuelewa napelekwa wapi na kwa nini wameniteka. Kila nikiwauliza kosa langu nini niliambiwa:
“Kelele utalijua muda si mrefu.”

Sikuwa na la kuongeza zaidi ya kutulia kusubiri kujua kilichofanya wanitendee kitendo cha kigaidi. Baada ya mwendo mfupi gari lilisimama na kuamriwa kuteremka. Baada ya kuteremka nilishikwa mkono na kupelekwa ndani ya nyumba.
Je nini kilitokea? Usikose kufuatilia simulizi hii katika Gazeti la Risasi Jumamosi.

Leave A Reply