The House of Favourite Newspapers

NDOA SIYO NGUO, USEME UTAJARIBISHA UIACHE!

NINA kila sababu ya kumshukutu Mwenyezi Mungu kwa wema wake, kwa kunipa na kukupa nafasi wewe msomaji wangu kujumuiika nami katika kuelimishana juu ya maisha na uhusiano wa kimapenzi.

 

Ni wengi ambao walitamani kuiona siku hii, lakini hatunao kwani kifo kimekuwa hakina huruma hata kidogo kwa siku tulizonazo. Ni vema kama wan­adamu tukajiandaa kwa ajili ya kifo kwani hakina taarifa.

 

Hayo tumwachie Mungu na turejee kwenye mada yetu ta leo. Ni mada pana kidogo juu ya wale ambao waliamini au wanaamini kuwa ndoa ni jambo la kawaida. Wanad­hani ni  kama kwenda kununua nguo kwenye Soko la Kariakoo na kuvaa, lakini fasheni yake ikipita, basi unalitupa kule au unali­gawa.

 

Ukweli ni kwamba weka kwenye akili yako, ndoa si jambo lelemama. Ndugu yangu, ndoa siyo ya hivyo, ndoa ni mkataba wa maisha, mkataba wa kudumua na kuvumiliana kwenye shida na raha, jua na mvua, mchana na usiku. Uzuri wa mapenzi bana hasa kwenye uhusiano rasmi wa ndoa, ukishaingia umeingia, haijalishi uliingia kwa mtindo upi, kitu kikishakukolea hata ufanyaje!

Siku ya leo napenda ku­washauri sana wale ambao wako nje ya ndoa kuwa ndoa siyo nguo useme unaweza kuinunua, ukaivaa na baadaye ukaiacha au kuijaribisha. Ndoa ni kiapo, tena kiapo cha kifo hasa, kwani mnashauriwa ili kuacha basi ni hadi pale Mola anakapomtwaa mmoja wapo. In­gawa inawezekana kiapo hicho ni tofauti kwa imani nyingine, lakini sehemu kubwa ndoa ni muunganiko wa jinsi mbili tofauti ambazo zinaungana na kuwa mwili mmoja.

 

Jambo lako ndiyo la mkeo, la mumeo ndiyo lako, hiyo ndiyo maana ya ndoa kisha yanafuatia mambo mengine kama kusaidi­ana, mambo ya kawaida na hata yale ya kimapenzi. Wasaa wangu kwako ambaye bado hujafanikiwa kuoa ni kuwa makini sana na uchaguzi wako. Ni kuwa makini sana na mtu ambaye unataka kuingia naye kwenye kiapo cha maisha yako.

 

Usikurupuke kwa sababu jamaa anaonekana ni hand­some, achana na urembo wake, weka pembeni hako kagari kake alikokuja nako nyumbani kwenu, kwanza yawezekana kakaazima, ka dada yake au shemeji yake au kakodi ilimradi akutie roho juujuu tu mtoto wa watu.

 

Achana na kazi au elimu nzuri aliyonayo, mwanaume au mwa­namke wa ndoa hachaguliwi kwa mtindo huo. Hachaguliwi kwa kuangalia vigezo hivyo bali ni lazima uijikridhishe je, ana vile vitu unavyovihitaji katika maisha yako.

Kama hana basi huyo hakufai maana itafika sehemu una­muacha au utamtafutia sababu za hapa na pale ili muachane. Kwa mfano unapenda mwan­amke au mwanaume ambaye ni mpole, basi tafuta mwanaume mwenye hulka na tabia hizo ili uishi katika ndoa ambayo un­aipenda. Lakini ukiolewa ilimradi umeolewa nakwambia itakuko­sti baadaye.

 

Vijana wengi wa sasa wanach­agua watu wa kuishi nao kama wanandoa kwa sababu ya kitu fulani na ndiyo maana baada ya muda fulani unasikia ndoa ile ambayo ilivunja rekodi kijijini imevunjika. Ukichunguza kwa ndani imevunjika kwa sababu kile kilichowaunganisha kimeisha au kimepotea.Kwa leo naishia hapa, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine moto!

Comments are closed.