The House of Favourite Newspapers

NDOA YA AMBER RUTTY SIRI YAFICHUKA!

DAR ES SALAAM: BAADA ya kuzungumzwa mengi kuhusu picha zinazomuonesha video queen, Muscat Abubakary ‘Amber Rutty’ amevaa shela akiwa na mpenzi wake Said Bakary Mtopali na watu kutojua ukweli wake, Risasi Mchanganyiko limechimba na kubaini uhalisia wake.

 

Picha hizo zilizua gumzo Jumapili iliyopita baada ya kuvuja kwenye kurasa mbalimbali za mitandao ya Instagram huku baadhi ya watu wakiwapongeza kwa hatua hiyo, wengine wakiwaponda kwa kusema itakuwa ni kiki ya filamu au wimbo.

 

RISASI LAMSAKA AMBER RUTTY

Baada ya kuona mitazamo mbalimbali na watu wengi kubaki njia panda mitandao kwa kushindwa kung’amua kama ni kweli wawili hao wameoana au la, juzi Jumatatu, Risasi Mchanganyiko lilimvutia waya Amber Rutty ili kujua ukweli wa mambo.

 

APOKEA MTOPALI

Simu hiyo ya Amber Rutty ilipokelewa na Mtopali ambaye aliomba kuongea yeye kwa niaba ya Amber Rutty ambaye wakati huo alikuwa amelala akidai kuwa mkewe huyo alichelewa sana kulala siku iliyopita.

 

MAHOJIANO YALIKUWA HIVI

Risasi: Tulikuwa tunataka kujua ukweli wa hizi picha ni kweli mmeoana au ni kiki?

Mtopali: Hiyo ni ndoa kweli, tumefunga nyumbani kwa mama yake Amber Rutty, Mtoni Mtongani.

Risasi: Je, ilikuwa ni mipango yenu tangu awali au imetokea tu ghafla mkaona mfunge ndoa?

Mtopali: Ilikuwa ni mipango yetu tangu tunaanza uhusiano wetu. Kama vile wapendanao wowote wanavyokuwa na mipango yao katika uhusiano, hata sisi tulikuwa tumepanga tuoane sema tu ndiyo lilitokea lile tatizo.

 

WALIIPIKA MUDA TU…

Tulipanga zamani kidogo sema matatizo yale bwana yalipotokea kila kitu kikaharibika. Sasa tukiwa nje kwa dhamana, tukajadili na mwenzangu tukaona ni vyema tu kutimiza ahadi yetu wakati huu kabla mwaka 2018 haujaisha.

Risasi: Mlifunga ndoa hiyo kwa imani gani? Kikristo au Kiislamu?

Mtopali: Ndoa ya Kiislamu, sisi wote ni waislamu hivyo hatuwezi kufunga ndoa ya imani nyingine.

Risasi: Inasemekana mmeokoka baada ya kwenda kwa Mchungaji Daudi Mashimo ambaye aliwawekea dhamana mahakamani sasa imekuwaje mkaamua kufunga ya Kiislamu?

Mtopali: Mchungaji ni sehemu ya familia, tunamshukuru sana kwa aliyotutendea lakini sisi hatujaokoka.

Risasi: Lakini si ilisemekana mnakaa pia kwenye nyumba ya kanisa baada ya kutoroka kule nyumbani kwa mama yake Amber Rutty (Mtoni Mtongani)?

Mtopali: Hapana, hatukuwahi kutoroka wala kuishi katika nyumba ya kanisa. Sisi tunaishi kivyetu licha ya kuwa mchungaji tunashirikiana naye katika mambo mbalimbali.

 

KUHUSU SHEREHE

Risasi: Vipi mlifanya sherehe kubwa au ndoa ilikuwa ya kimyakimya?

Mtopali: Hapana tuliona hakuna sababu ya kufanya hivyo, tulifunga tu ndoa na hakukuwa na sherehe ya aina yoyote baada ya ndoa.

 

ISHU YA MAHARI

Risasi: Labda pengine mahari ilikuwa kiasi gani?

Mtopali: Hilo kwa kweli siwezi kuliweka wazi kimsingi wewe fahamu tulikubaliana na ndoa tukafunga.

Risasi: Vipi kuhusu ndugu wa upande wa mke walikuwepo?

Mtopali: Baba yake alimtuma muwakilishi, yeye hakuweza kuja lakini baadhi ya ndugu wengine walikuwepo lakini kwa kuwa hatukutaka kufanya tukio kubwa, hata ndugu walikuwa wachache.

 

MIPANGO 2019

Risasi: Nini mipango yenu kwa mwaka 2019?

Mtopali: Tunamshukuru Mungu kwa yote yaliyotokea, tumejifunza mengi na tunazidi kumuomba Mungu kwa mwaka mpya uwe na mafanikio.

Risasi: Asante Mtopali, niwatakie mafanikio tele kwa mwaka 2019.

Mtopali: Asante na karibu tena.

 

TUJIKUMBUSHE

Amber Rutty na mumewe huyo wanakabiliwa na mashtaka matatu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar yakiwemo ya kufanya mapenzi kinyume na maumbile na kusambaza picha za ngono kupitia mitandao ya kijamii. Kesi hiyo bado inaendelea mahakamani hapo baada ya wawili hao kuachiwa kwa dhamana.

Stori: ERICK EVARIST, RISASI MCHANGANYIKO

Comments are closed.