NDOA YA MISS TANZANIA, MTOTO WA MAKAMBA… USIPIME!

Victoria Martin na Thuwein Makamba.

DAR ES SALAAM: Ni historia! Harusi ya Mrembo aliyetinga Top Five ya Miss Tanzania 2007, Victoria Martin na mtoto wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Yusuf Makamba, Thuwein Makamba imeacha gumzo la aina yake kutokana wawili hao kuangusha sherehe baa’kubwa.

NI TANGA Wawili hao walifanya tendo hilo jema kwa Mwenyezi Mungu, Ijumaa iliyopita mkoani Tanga ambapo waalikwa waliizungumzia kama ni ndoa ya kihistoria kwani kwa kipindi hiki, haijawahi kufungwa ndoa na watu kunywa, kula hadi kusaza kwa kiasi hicho.

CHANZO KINAIFUNGUKIA

Chanzo makini ambacho kilianza kushuhudia sherehe za wawili hao kuanzia send off hadi harusi, kilisema matukio hayo yote yalipambwa na kufuru ya vinywaji na vyakula kiasi ambacho kila aliyeingia ukumbini alitoka akiwa nyang’anyang’a.

“Yani kwa kipindi hiki cha Magu (Rais Dk John Pombe Magufuli) sherehe kubwa kuandaliwa kwa kiwango hiki ni tukio la aina yake maana watu kwa kweli hawana hela. “Lakini kwenye sherehe hizi za Victoria na huyu mtoto wa Makamba ilikuwa ni tofauti.

Watu wamekunywa, wamekula hadi wamesaza. Vyakula vilivyobaki vilitosha hata kufanyia sherehe nyingine kama hii tuliyoifanya,” kilinyetisha chanzo hicho.

MAMBO YALIANZA ALHAMISI

Kikizidi kumwaga ubuyu, chanzo hicho kilianza kueleza eneo lilipofanyika sherehe ya send off kabla ya ndoa kufungwa, siku ya Ijumaa. “Mambo yalianzia Alhamisi (iliyopita), baada ya vikao kufanyika vya send off, waalikwa tulitegemea tutakuta sherehe ya kawaida kutokana na bajeti yetu lakini mambo yalikuwa ni tofauti.

“Sherehe ilikuwa kubwa mno. Watu walifurika katika Ukumbi wa Regal Naivera, tulikunywa kwa kweli kama mimi hadi naondoka pale nilikuwa sijitambui,” kilisema chanzo hicho.

Thuwein Makamba na kaka yake, Janury Makamba.

 

NDOA SASA…

Chanzo hicho makini kilizidi kumwaga ubuyu kuwa, kutokana na mrembo huyo kuwa Mkristo na mumewe kuwa Muislam, alilazimika kubadili dini kumfuata mumewe na ndoa ikafungwa katika Hoteli ya Mkonge ambayo ni miongoni mwa hoteli za gharama jijini Tanga. “Si unajua Vick ni Mkristo, alilazimika kumfuata mumewe ili kuondoa migongano ya kidini,” kilisema chanzo hicho.

HARUSI USIPIME

Chanzo hicho kilifunguka kuwa, mara baada ya kunywa hadi kutojitambua siku ya send off, balaa lilihamia siku ya harusi katika Hoteli ya Tanga, Beach Resort hapo ndipo mambo yaliponoga zaidi.

“Wee hapo ndipo mambo yaliponoga balaa, tulikunywa sana, tukacheza kweli na kifupi kila kitu ndani kilikuwa rasmi sana. “Mashampeni yalikuwa hayana idadi, yani ilikuwa ni full burudani kwa kweli.

Watu wangu wa karibu ambao ni hodari kwa kunywa, walikunywa hadi wakatambaa lakini mzigo bado ulikuwepo wa kutosha,” kilieleza chanzo hicho.

 

Ndoa ilivyonoga.

TANGA YAWA GUMZO

Kutokana na umaarufu wa Victoria na Thuwein, sherehe hiyo ilikuwa gumzo katika viunga mbalimbali vya burudani mjini Tanga kutokana na watu wengi kuijadili.

“Yani gumzo mpaka sasa ni harusi ya Thuwein na Vick, kila mtu amebaki na kumbukumbu yake. Kuna ambao walifurahishwa na mandhari ya Tanga Beach maana palipambwa, pakambambika.

“Kuna wengine walifurahishwa na shampeni zilivyokuwa nyingi lakini wengine walipenda kuona watu maarufu waliokuwemo akiwemo kaka wa bwana harusi, January Makamba,” kilieleza chanzo hicho.

 

HUYU HAPA BWANA HARUSI

Amani lilimtafuta bwana harusi, Thuwein kupitia simu yake ya mkononi ambapo alipopatikana alisema anamshukuru Mungu kwamba sherehe yake imeenda vizuri na anawashukuru watu wote waliojitoa kufanikisha maana peke yake asingeweza kufanikisha.

“Namshukuru Mungu, sherehe ilikuwa nzuri. Nawashukuru wote walionichangia hadi kufanikisha sherehe nzuri,” alisema Thuwein.

Kwa upande wake Victoria, alisema hana la kuzungumza zaidi ya kumshukuru Mungu kwa hatua hiyo aliyoifikia. “Namshukuru Mungu, nimekuwa mke wa mtu sasa. Nawashukuru wote waliofanikisha,” alisema Victoria.

UMAARUFU WA VICTORIA

Mrembo huyo aliwahi kuwa Miss Tanga 2007, akaingia Top Five mwaka 2007, akawa Balozi wa Redds. Tangu hapo, jina lake lilikuwa kubwa katika vyombo vya habari hivyo mrembo huyo kuwa maarufu hususan kutokana na urembo wake.

 

STORI: WAANDISHI WETU| AMANI

Breaking News: Chadema Wafunguka Lissu Aachiwe, Ngeleja Akamatwe


Loading...

Toa comment