NDOA YA PILI YA MCHUNGAJI ILIYOTIBULIWA KANISANI… MAPYA YAIBUKA!

DAR ES SALAAM: Lile sakata la Mchungaji wa Kanisa la Gospel Revival Assemblies of God la Mlandizi, Julius Andrew aliyenaswa akifunga ndoa ya pili na mke mwingine aliyefahamika kwa jina moja la Stellah baada ya kumtosa mkewe Maria Stoni ambaye alifanikiwa kuitibua ndoa hiyo, mapya yameibuka; Amani limegundua.  

 

Katika sakata hilo Maria alimfumania mumewe huyo akifunga ndoa na Stellah na kufanikiwa kuitibua baada ya kuwasilisha vielelezo vya ndoa yake na mchungaji huyo kikiwemo cheti cha ndoa, picha za kumbukumbu ya siku ya ndoa yao na picha za watoto wawili waliozaa ambapo Askofu John Mzule wa Makanisa la Gospel Revival Assemblies of God alimuuliza mchungaji Julius kama alikuwa akimtambua mwanamke huyo.

 

Mchungaji Julius alikiri kuwa Maria alikuwa mkewe lakini waliachana na tayari alikuwa na hati ya talaka kutoka mahakamani ambayo aliitoa madhabahuni hapo na kumuonesha Askofu Mzule ambaye baada ya kuipitia aliahirisha kufungisha ndoa hiyo na kuahidi kulifanyia uchunguzi suala hilo.

UCHUNGUZI WA ASKOFU

Wiki moja baada ya ndoa hiyo kuvurugika mwandishi wetu alimtafuta Askofu Mzule kujua alipofikia katika uchunguzi wake ambapo alisema:

 

“Nimeshalifanyia uchunguzi suala na ndoa ya awali na nikabaini ni kweli walifunga ndoa halali kanisani lakini baadaye ikaanza migogoro. “Mwanaume alikwenda Mahakama ya Mbagala na kupewa hati ya kuachana na Maria hivyo ile hati aliyoionesha kanisani ilikuwa ni ya kweli, hivyo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haina pingamizi na ndoa yake kuvunjika ingawa kidini sisi tunayoitambua ni ndoa moja mpaka kifo.”

MGAWANYO WA MALI

Ikumbukwe kuwa baada ya ndoa hiyo kuvurugika Askofu Mzule alimtaka Maria aeleze sababu ya pingamizi lake katika ndoa hiyo kama ni kutaka kuendelea kuishi na mumewe huyo au alikuwa na sababu nyingine ya msingi.

Maria alipoulizwa swali hilo mbele ya mwandishi wetu alimjibu askofu huyo kuwa madhumuni ya kuweka pingamizi hilo ni kumtaka mumewe huyo kama hamtaki, amtendee haki ikiwemo mgawanyo wa mali walizochuma.

Kuhusu suala hilo la mgawanyo wa mali askofu alisema: “Niliongea na wote wawili na waliniambia wamechuma vitu mbalimbali na katika mgawanyo wamesema kiwanja chao kilichopo Msongola Dar, kiwe mali ya watoto, pikipiki aina ya Boxer ibaki kwa mwanaume. “Kitanda wamekubaliana achukue mwanaume, godoro na friji achukue mwanamke na vitu vingine vibaki kwa mwanaume,” alisema Askofu Mzule.

Baada ya maelezo hayo ya askofu, mwanahabari wetu alimpigia simu Maria kujua kinachoendelea naye alisema licha ya kutolewa muongozo wa kupata mgawanyo wa mali lakini mwanaume huyo bado hajampa chochote na inasemekana anataka kufunga ndoa kwingine.

 

Mwandishi wetu alipompigia simu Askofu Mzule na kumuuliza kuhusu huyo bwana kutaka kufunga ndoa kanisa lingine alisema yeye hata kama watafunga, haitambui ndoa hiyo kwani msimamo wake unabaki kuitambua ndoa ya awali.

“Kama wamefunga au watafunga ndoa sehemu nyingine hilo mimi silitambui, natambua ndoa ya awali,” alisema Askofu Mzule. Mwanahabari wetu alimpigia simu Mchungaji Julius ili azungumzie suala hilo lakini simu yake iliita kila ilipopigwa lakini haikupokelewa.

Makala: Richard Bukos, Amani

AIBU YA MWAKA! Mchungaji Afumaniwa Akioa Mke Mwingine!

Loading...

Toa comment