Ndoa Yako Imekuwa Adui au Rafiki wa Mafanikio?

Attractive couple having an argument on couch at home in the living room

Attractive couple having an argument on couch at home in the living room

Nimshukuru Mungu kwa kunijaalia uzima ulioniwezesha kuandaa makala haya. Ndugu zangu, leo nataka kuzungumzia suala la mafanikio na namna ndoa inavyoweza kuwa rafiki au adui wa mafanikio yako.

Naandika mada hii kutokana na ukweli kwamba, wapo watu wengi huko mtaani ambao wamekimbilia kuingia kwenye ndoa na watu ambao hawana ndoto za mafanikio, matokeo yake wamekuwa hawana nyuma wala mbele licha ya kwamba walishaanza kuelekea kwenye njia iliyonyooka.

Yupo kaka alimenipa kisa kilichonisukuma niandike makala haya. Awali alikuwa akifanya biashara, alikuwa na maduka mawili jijini Dar na alimiliki pia magari mawili ya mizigo na moja la kutembelea.

Mwanga wa mafanikio alishaanza kuuona, akaona atafute mwenza ili wapambane pamoja kuelekea kwenye malengo yake. Akampata binti ambaye ni msomi wa mambo ya biashara, akaona huyo angemfaa.

Akamchumbia na kufunga ndoa, kwa bahati mbaya kumbe yule dada hakuwa na mapenzi ya kweli kwa mwanaume yule bali alifuata utajiri tu.
Katika hatua za mwanzo, mapenzi yalikuwa motomoto lakini kuna wakati yule mwanamke akabadilika.

Hebu msikie mwanaume anavyolalamika: “Ilifika wakati akawa anapenda sana starehe na mimi nilikuwa sina mambo hayo. Nilipanga pesa yangu itumike kwenye mambo ya msingi kuliko starehe kwani nimeona ndizo zimewaangusha wengi kimaisha.

“Ikawa nikimkatalia kwenda baa au klabu ananinunia. Ukimuachia pesa anazitumia kwenye kununulia nguo na vitu vya thamani. Mbaya zaidi miradi ambayo nilimuachia aisimamie akaanza kutumia pesa kufanyia mambo yake tena kwa siri. Ndoa ikawa chungu na biashara nazo zikaanza kusuasua, hapo ndipo nikajuta kuoa.”

Unaweza kuona ni kwa jinsi gani ndoa imekuwa adui wa mafanikio kwa mwanaume huyo. Lakini pia kuna dada aliyejitambulisha kwa jina la mama Sudi, mkazi wa Arusha aliwahi kunipa malalamiko yake yanayofanana na ya huyu mwanaume.

Mama Sudi alisema, alipohitimu kidato cha sita hakufanikiwa kuendelea na masomo. Mjomba wake aliyekuwa na uwezo akampatia mtaji akafungua saluni aliyoamini ingemletea mafanikio makubwa.

Alikuwa makini katika kila shilingi aliyopata, mara akafungua duka ambalo lilimfanya akaongeza lingine na hatimaye kununua gari. Mpaka anafikia kipindi cha kuolewa alikuwa na mafanikio makubwa.

Mungu jaalia akapata mchumba aliyekuwa akifanya kazi ya uhasibu kwenye kampuni moja maarufu nchini. Akakubali kuwa naye akijua atamsaidia kwenye kusimamia biashara zake.

Tofauti na matarajio yake, baada ya kuolewa akagundua mume ni mfujaji wa pesa. Lile jukumu alilopewa la kusimamia biashara, akawa anatumia pesa nyingi kwenye anasa hadi biashara zikafa.

Sasa hivi ninavyoandika makala haya mwanamke huyo anaishi kwa kutegemea mshahara wa mume. Kupitia mkasa huo ni dhahiri utakuwa umejifunza kitu kwamba usipokuwa makini mweza wako anaweza kukurudisha nyuma kimafanikio lakini pia ukibahatika, unaweza kushangaa ubavu wako unakuwa na mchango mkubwa kwenye mafanikio yenu.

Ndiyo maana nikakuuliza kwamba, tangu umeingia kwenye ndoa unadhani huyo mwenza wako amekuwa rafiki wa mafanikio au amekuletea tu gundu kwenye maisha yako? Ni vyema ukafanya uchunguzi katika hilo kabla ya safari ya maisha kuendelea.

Loading...

Toa comment