The House of Favourite Newspapers

Ndoto za kufanikiwa zinaenda sawa na matendo yako?

0

ndotoWafuatiliaji wa safu hii watakuwa wanakumbuka baadhi ya makala zangu za nyuma ambazo nilizungumzia hatua za kupitia kueleka kwenye mafanikio.

Nikajaribu kutoa mifano ya baadhi ya watu waliopitia hatua nilizozieleza na hatimaye wakatimiza ndoto zao.

Kinachonishangaza ni kwamba, licha ya kuandika hayo wapo wasomaji wangu ambao mpaka leo maisha yao hayana nyuma wala mbele. Wanaishi ili mradi siku zinakwenda kwa sababu wanashindwa kufuata zile kanuni zinazoweza kuwatoa hapo walipo kuelekea kwenye mafanikio.

Hawa ni wale ambao hata wasaidiwe vipi hawawezi kufanikiwa. Wataishia kuishi maisha yaleyale ya kulalamikia ugumu wa maisha bila kujua kuwa wao ndiyo chanzo cha yote hayo.

Wapo vijana wengi ambao wanaota mafanikio kila siku lakini cha ajabu mfumo wao wa maisha hauendani na ile dhamira yao.

Hivi utakuwaje mtu unayetamani mafanikio lakini hauko makini na pesa zako hizo chache unazozipata? Sawa hupati mamilioni, hizo elfu kumikumi unazopata unazitumiaje?

Huwezi kuwa ndoto za kutaka kumiliki mamilioni wakati ukipata shilingi laki moja sehemu kubwa unatumia kwenye anasa. Yaani unaona pesa hizo ni chache kiasi kwamba hata ukiweka hazina faida, wewe mwenye mawazo hayo unakosea sana.

Nasema haya kwa kuwa nina mifano ya watu ambao wakipata kiasi flani cha pesa wanasema eti ni ‘hela mbuzi’ ya kulia bata. Wananywea pombe, wanahonga mademu mpaka zinaisha kisha wanaanza moja.

Achilia mbali hao, wapo wanaofanya kazi ambao wanaona kwa mishahara midogo wanayopata hawawezi kufanya mambo makubwa katika maisha yao.

 Naomba leo niseme hivi, wapo watu ambao wanafanya kazi zinazowaingizia mshahara mdogo kama vile shilingi laki mbili au chini ya hapo lakini wana mafanikio kuliko wale wanaopata milioni au zaidi.

Utajiuliza ni kwa nini? Ni kwa sababu kuna ambao wana nidhamu sana na kila shilingi wanayoipata. Mtu anapokea mshahara wa shilingi laki moja na ana familia lakini kwa kujibana amefanikiwa kujenga kibanda chake na maisha yanaendelea.

Mtu anafanya kazi ya ulinzi, anapopata mshahara wa shilingi laki na nusu lakini amejibana mpaka amepata mtaji wa biashara. Usiku anakuwa lindoni, mchana anakuwa kwenye genge lake na taratibu anapiga hatua kuelekea kwenye mafanikio.

Jiulize wewe ambaye unapata mshahara mkubwa na marupurupu ambayo hujayatarajia, unazitumiaje katika kutimiza ndoto zako? Au wewe ni miongoni mwa wale ambao wanasubiri wapate fedha nyingi ndiyo waote kufanya mambo makubwa?

Kama wewe ni miongoni mwa watu hao, umechelewa sana! Watu ambao wanayatamani mafanikio hawana hata shilingi ya kuchezea. Shilingi mia tano kwao ni kubwa sana. Mshahara wa shilingi laki moja wanaupigia mahesabu ya kufanyia mambo makubwa. Hawa ndiyo ambao mafanikio hayawezi kuwapitia mbali.

Leave A Reply