Ndugai Alivyowafanya Wabunge Hawa Kuwa Gumzo!

 

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai ameeleza kutotambua barua ya Chadema kuhusu ukomo wa ubunge wa aliyekuwa Mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe. Kitendo hicho kimemfanya Mwambe kutinga bungeni hali inayofanya kiongozi huyo wa bunge kuwa gumzo.

 

Amekuwa gumzo kwa sababu awali alikuwa na mgogoro na wabunge watatu ambao wawili waling’olewa.

Februari 15, mwaka huu, Mwambe alitangaza kujivua uanachama wa Chadema akiwa ofisi ndogo za Makao Makuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Lumumba jijini Dar na kupokewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho tawala, Humphrey Polepole.

 

Hivi karibuni Spika Ndugai aliwaeleza wabunge kuwa alipokea barua ya Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika ikieleza kwamba, Bunge lisimtambue Mwambe kama mbunge na asipate stahiki zozote.

 

“Lakini barua yenyewe jinsi ilivyoandikwa ni fupi, niwasomee tu,” anasema Ndugai na kuongeza; “Bwana Cecil Mwambe alikuwa Mbunge wa Jimbo la Ndanda aliyekuwa amedhaminiwa na Chadema. Hata hivyo, Februari mwaka huu alitangaza kupitia vyombo vya habari kwamba amehama chama hicho.

 

“Hivyo basi, kwa mujibu wa Ibara ya 7 (1 F) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amekoma kuwa mbunge na ameacha kiti chake katika Bunge, kwa hiyo Bunge lisiendelee kumpatia sitahiki zozote.”

 

Ndugai anasema; “Sasa namshangaa Mnyika kwa sababu hayo maneno anayosema alipaswa aambatanishe na barua ya Mwambe inayothibitisha haya anayosema, hakuambatanisha.

“Pili, mimi sina barua ya Mwambe ya kusema kwamba kaacha ubunge kwa hiyari yake mwenyewe na kama ni chama hiki (Chadema) kimechukua hatua, sina viambatanisho vinavyoonesha vikao halali vilivyofanya maamuzi hayo, kwa hiyo hii barua haina maana, haina mantiki.”

 

Akizungumza na redio moja, Mwambe alisema, tayari yuko Dodoma kusikiliza wito wa Ndugai kwa kuwa alitakiwa kuendelea na shughuli zake za kibunge.

Alipoulizwa kuwa atakuwa mbunge wa chama kipi kwa sababu tayari alishajiuzulu uanachama wa Chadema, naye alihoji kwani awali alikuwa mbunge kwa chama kipi?

 

Katika hilo, alisisitiza kuwa ataendelea kuwa Mbunge wa Ndanda kupitia Chadema.

Kuhusu kama ataendelea kuwa mwanachama wa Chadema, alisema; “Nilijiuzulu uanachama wa Chadema, nikaacha ubunge mheshimiwa spika amenitaka nije nimalizie muda wangu uliobaki, naweza kuwa si muumini wa Chadema, lakini mwisho wa siku nimerudi bungeni kwa mujibu wa mwongozo uliotolewa na spika.

 

Uamuzi wa Spika kumrudisha Mwambe bungeni, umezua mjadala mkali uliowaibua wanasheria ambao wengi wao wameonekana wazi kutounga mkono hoja za Ndugai hasa kwa kuzingatia kwamba Mwambe alitangaza hadharani kujiondoa mwenyewe na si Chadema kumfukuza.

 

Uamuzi wa Ndugai unakumbusha mengi kuhusu maamuzi yake ambayo wabobezi wa sheria kama Wakili Albert Msando anasema ukishajiunga na chama kingine, tayari umekuwa umejiondoa na chama cha awali. “Anaenda bungeni kwa chama kipi?” Alihoji Msando kupitia ukurasa wake wa Twitter.

 

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ruaha, Profesa Gaudence Mpangala anasema kumrudisha Mwambe bungeni ni kinyume cha sheria na Katiba ya nchi. “Mimi nashangaa kwa nini spika anavunja sheria na katiba ya nchi…hata wabunge wa Chadema walipojitoa na kujiunga CCM walipoteza ubunge hadi uchaguzi mwingine ulipofanyika, tunapaswa kutoa haki kwa wote,” anasema.

Huko nyuma Ndugai aliwahi kuwa na migogoro na wabunge kama ifuatavyo;

 

NDUGAI NA MASELE

Spika Ndugai alijikuta katika mgogoro na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Bunge la Afrika (PAP), Stephen Masele, akisema sababu ni utovu wa nidhamu wa kiongozi huyo na kugonganisha mihimili ambapo alitangaza kusitisha kwa muda uwakilishi wa Masele.

 

Ndugai alimtuhumu Masele kuwa alikuwa akipeleka maneno ya uongo kwa viongozi wa ngazi za juu serikalini na kwamba Bunge lilikuwa likimuita Masele arejee nchini kuhojiwa na Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, lakini alikaidi.

 

Baadaye Ndugai alimwandikia barua Rais wa PAP, Roger Dang, kumweleza juu ya kusitisha kwa muda uwakilishi wa Masele katika Bunge hilo ili arudi kujibu tuhuma zilizokuwa zikimkabili. Sakata hilo liliisha kwa Ndugai kumsamehe Masele.

 

NDUGAI NA NASSARI

Machi 14, mwaka jana, Ndugai alitangaza kuvuliwa ubunge kwa Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki, Joshua Nassari, baada ya kupoteza sifa ya kuwa mbunge, hatua ambayo ilifikiwa huku mbunge huyo akiwa katika ziara ya kutekeleza majukumu ya kibunge kupitia Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii iliyokuwa Chuo cha Mweka mkoani Kilimanjaro.

 

NGUGAI NA LISSU

Katika tukio lingine, Ndugai alitangaza kumvua ubunge aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, kwa madai ya kutohudhuria vikao vya bunge bila taarifa na kutowasilisha taarifa rasmi kuhusu mali na madeni, ambapo aliitaarifu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuandaa uchaguzi katika jimbo hilo.

 

Katika uchaguzi huo wa marudio ulioitishwa Julai, mwaka jana, mgombea wa CCM, Miraji Mtaturu, alipitishwa kama mshindi kutokana na kuwa mgombea pekee aliyerejesha fomu za kuwania nafasi hiyo.

 

Kifupi ni kwamba, katika uongozi wake Ndugai kwa wabunge umekuwa gumzo kwani mambo mazito yamekuwa yakiibuka, kwani sasa anawakodolea macho wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa kuwaita watoro baada ya kujiweka kwenye karantini. Sasa tusubiri tuone maendeleo ya sakata hili!


Toa comment