SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, jana Mei 6, 2020, amewataka wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) waliosusia vikao vya bunge kwa kisingizio cha kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vyacorona kurudi haraka bungeni.
Amesema endapo watakaidi agizo hilo la kurudi bungeni basi itawalazimu siku watakayorudi wawe na cheti kinachoonyesha kuwa wamepima ugonjwa wa Covid-19 na majibu yake na kurudisha pesa walizolipwa ambazo ni posho za vikao la sivyo hatua zaidi zitachukuliwa.
“Wabunge hawa ambao ni watoro walipokuwa wanaondoka walilipwa fedha za kuanzia Mei 1 – 17 jumla ya zaidi Sh Mil 110, nawaagiza, kuanzia Freeman Mbowe kurudisha Tsh milioni mbili na elfu arobaini na wenzake wote hao. Huu ni utoro wa hiari, kwa lugha rahisi huu ni wizi na wale wengine wamelipwa milioni tatu warudishe,” alisema.
Aidha ameongeza kuwa; “Nimeshangazwa na kusikitishwa sana na tangazo hilo kwa sababu Mbowe hana mamlaka ya kuitisha utoro wa wiki mbili kwa wabunge, anajaribu kuwa kama Prefect wa Shule ya Sekondari, japo wameambiana kubaki Dodoma lakini wanazurura nchi nzima, wabunge hao popote walipo warudi bungeni haraka sana kuendelea na kazi zao”.


