YANGA imethibitisha kuwepo katika mazungumzo ya mwisho na mshambuliaji wa UD Songo ya nchini Msumbiji, Jimmy Ukonde, atakayetua kuichezea timu hiyo kwenye msimu ujao wa Ligi Kuu Bara, ni baada ya mazungumzo kwenda vizuri.
Hiyo yote ni katika kuhakikisha wanaisuka vema safu hiyo ya ushambuliaji ambayo tayari wapo kwenye mipango ya kukamilisha usajili wa washambuliaji Heritier Makambo wa Horoya AC ya Guinea na Tuisila Kisinda anayekipiga AS Vita ya DR Congo.
Wakati ikipanga kusajili nyota hao, tayari imepanga kuachana na baadhi ya washambuliaji wa kimataifa, David Molinga, Yikpe Gnamien, Patrick Sibomana na Mybin Kalengo kwenye msimu huu.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatatu, mabosi wa GSM kwa kushirikiana na viongozi wa Yanga, wamepanga kukamilisha dili hilo la usajili wa staa huyo aliyekuwa anacheza pamoja na kiungo mshambuliaji wa Simba, Luis Miquissone.
Mtoa taarifa huyo alisema jina la Ukonde ni kati ya yale yaliyopendekezwa na Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mbelgiji Luc Eymael katika kuhakikisha anakisuka kikosi hicho katika msimu huu.
Aliongeza kuwa kocha huyo tayari ameshakabidhi ripoti ya usajili kwa viongozi wa timu hiyo ambayo tayari wameijadili na kuahidi kutimiza yale yote aliyoyapendekeza katika usajili wake ikiwemo safu ya ushambuliaji.
“Ukonde unatarajiwa kuwa usajili wa tatu baada ya Makambo na Tuisila ambao wote ni washambuliaji, hiyo yote ni katika kuisuka safu hiyo ya ushambuliaji inayoongozwa hivi sasa na wazawa Nchimbi na Tariq.
“Ni baada ya washambuliaji wa kimataifa kushindwa kuonyesha umahiri wao wa ufungaji mabao ambao ni Yikpe na Molinga ambao kwenye usajili mkubwa wamepangwa kuachwa.
“Mipango yote ya usajili ya Ukonde imeshakamilika, ni suala la muda pekee kama ilivyokuwa kwa Makambo na Tuisila viongozi hivi sasa wapo kwenye mazungumzo na klabu zao wanazozichezea kutokana na kuwa na mikataba,” alisema mtoa taarifa huyo.
Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela alipotafutwa kuzungumzia hilo, alisema: “Tupo kwenye mazungumzo na baadhi ya washambuliaji wa kimataifa ambao majina yao ni siri, kila kitu kitajulikana baada ya kila kitu kukamilika.
“Kati ya washambuliaji hao huenda akawepo Ukonde kwani ni kati ya washambuliaji wazuri wenye uwezo mkubwa wa kufunga mabao.”
WILBERT MOLANDI, Dar es Salaam


