The House of Favourite Newspapers

Ndugu Zangu Walinichukua Msukule-2

0

MSIMULIAJI: Obedi Masanja

Ilipoishia wiki Iliyopita:

BABA ATAKA KUMPA SAPOTI, AKATAA

Baba yangu alikuwa na eneo kubwa la mashamba aliponiona nina kiu ya kusoma akataka auze baadhi ya mashamba lakini ikabidi nimweleweshe sana ndipo akakubaliana na ushauri wangu wa kujikita katika kilimo.

Sasa endelea…

Mwaka 1995, mwezi wa kwanza ndiyo nilikwenda kuanza darasa la saba katika Shule ya Msingi Mgata ambayo ilikuwa palepale kijijini kwa kusoma elimu ile ya watu wazima ambapo nilikuwa nikienda jioni na tayari nilikuwa nimeshanunua vitabu vya masomo yote ili nisiwe napata shida kujisomea hata nikiwa nyumbani.

AANZA MASOMO KWA TABU

Asubuhi nikawa nakwenda shambani, mchana narudi nyumbani kujiandaa kwenda shule japo kuna wakati mwingine nilikuwa nashindwa kwenda kutokana na uchovu na kuishia kujisomea nyumbani kwa kutumia mbalamwezi au kama mbalamwezi hakuna siku hiyo nilikuwa nikijisomea kwa kutumia moto wa kuni.

Nilikuwa nakoka moto jikoni kisha najisomea, nikiona sehemu siielewi nilikuwa nikiweka kiporo lakini ajabu ya Mungu, kwenye mitihani nilikuwa nikishika nafasi ya kwanza.

Nilisoma katika mazingira hayo na kuhakikisha nimebadili kwa kiasi fulani pale nyumbani palikuwa pameimarika kiasi kwamba kwa wakati ule kijiji kizima ni kwetu tu ndiyo kulikuwa na maendeleo kwa kujenga nyumba ya matofali na kuezeka bati.

Watu wengi walikuwa wakiyazungumzia maendeleo yetu na wengine kunisifia kwa jinsi nilivyokuwa nafanya shughuli za kilimo kwa bidii huku nikisoma.

Baadhi walikuwa wakisema kutokana na juhudi zangu ningeweza kufika mbali kimaisha.

AFANYA MTIHANI WA TAIFA

Mwaka 1995 nilifanya mtihani wa taifa, majibu yalipotoka nikachaguliwa kujiunga kidato cha kwanza mwaka 1996 katika Shule ya Sekondari Ivungo ambayo ni ya bweni. Iko Bukoba, Kagera. Nakumbuka Januari Mosi ndiyo nilitakiwa kuripoti shuleni hapo. Wakati huo nilikuwa nina umri wa miaka 20.

Kufuatia kuchaguliwa kuendelea na masomo ya sekondari, wengi walinipongeza na kunieleza juhudi zangu zilizaa matunda.

Niliwashukuru kwa pongezi na kuwaeleza kwa jinsi nilivyopenda kusoma nitafanya hivyo hadi nifike chuo kikuu.

Hata hivyo, sikuelewa kama kuna baadhi ya ndugu zangu walikuwa hawajafurahishwa na mafanikio yangu na walipanga kunirudisha nyuma kiuchawi.

Kama ningejua hilo mapema huenda ningechukua tahadhari ya kujikinga dhidi ya vitendo vya kichawi ambavyo nilikuja kufanyiwa.

AENDA SHULE, AKUTANA NA MAUZAUZA NJIANI

Nilijiandaa kwenda shule kwa vitu mbalimbli vilivyokuwa vinatakiwa lakini siku niliyokuwa nakwenda kuripoti ndipo nikaanza kukutana na mauzauza njiani wakati naelekea kituoni kupanda basi lililokuwa linakwenda Bukoba.

Ilikuwa siku ya Jumatatu, saa mbili asubuhi baada ya kuagana na ndugu zangu pale nyumbani huku mama yangu mzazi akinisindikiza, nilipokaribia kituo cha basi ndipo mama yangu akaniacha sehemu nikaanza kwenda mwenyewe.

Wakati nakaribia kituoni nyuma yangu kukatokea kundi kubwa la ndege waliokuwa wakinifuatilia, nilipofika kituoni ghafla nikaona basi limesimama na nilipoingia haukupita muda mrefu nikajikuta niko milimani nimezungukwa na wale ndege huku nikiwa kama nacheza nao.

Bila kutambua kama muda ulikuwa ukienda nilijikuta na mimi nimenogewa na wale ndege mpaka kufika jioni wale ndege wakawa wananisindikiza.

Katika hali ambayo haikuwa ya kawaida, niliendelea kucheza na wale ndege tena nikiwa mwenye furaha lakiniĀ  jambo la kushangaza nilipokaribia nyumbani wakatoweka.

Muda huo jua lilikuwa tayari limeshazama, mama aliyekuwa yupo nje aliponiona nikiwa na begi langu alishangaa na kuniuliza:

Je, nini kiliendelea? Usikose kusoma wiki ijayo mkasa huu unaoitwa Ndugu Zangu Walinichukuwa Msukule.

Leave A Reply