The House of Favourite Newspapers

Ndugu Zangu Walinichukua Msukule-3

0

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:

Bila kutambua kama muda ulikuwa ukienda, nilijikuta na mimi nimenogewa na wale ndege mpaka kufika jioni wale ndege wakawa wananisindikiza na nilipokaribia nyumbani wakawa wamepotea. Ninakumbuka nilifika nyumbani jua likiwa tayari limeshazama, nikamkuta mama nje akiwa anaandaa chakula cha jioni.

SASA ENDELEA…

Mama aliniuliza kama nilifika salama shuleni, nikamjibu ndiyo, akaniambia nikapumzike chumbani kwangu, chakula kikiwa tayari angeniamsha kwa ajili ya mlo wa usiku, nikamwambia sawa lakini  sikumsimulia kuhusu wale ndege.

Niliingia chumbani kwangu na kwenda kujilaza kitandani huku nikiwa sijielewielewi. Ukweli nilikuwa sijielewi na siwezi kusema nilikuwa najisikiaje!

Haukupita muda mrefu nikapitiwa na usingizi mpaka nilipokuja kuamka kutokana na maumivu makali ya kichwa yaliyonifanya nilie kwa sauti ya juu mpaka mama akasikia. Akaja mbio na kunigongea chumbani kwangu.

Alipoingia alinikuta nikiwa nina hali mbaya kiasi cha kushindwa hata kuongea naye. Mama alinikodolea macho ya kunishangaa, akaniuliza nina nini! Sikumjibu kitu zaidi ya kumwangalia tu kwa macho pima tena yakiwa yameganda bila kupepesa.

Nilimwona mama amechanganyikiwa sana kwa kuwa pale nyumbani alikuwa peke yake, hapakuwa na mwanaume, hivyo hakukuwa na msaada wowote. Ilibidi atoke nje na kuanza kuomba msaada kwa majirani akiwaita kwa sauti ya juu.

Wakati mama akiwa nje kuomba msaada, ghafla chumbani kwangu nilihisi hali ya joto. Pia nikahisi kuna watu wameingia. Kweli nilipoangalia sawasawa, nikawaona wanawake wanne wamesimama kwa kunizunguka kitandani huku wakiwa wameshika usinga (mkia wa mbuzi).

Hapa naomba niseme kidogo tu kwamba, tayari nilikuwa kwenye ulimwengu mwingine nje ya huu tunaoishi kiasi kwamba, mama na majirani walipofika walishtuka baada ya kuniona nimeshakata roho. Lakini kiuhalisia nilikuwa mzima na nilikuwa nikishuhudia kila kitu kilichokuwa kikiendelea mle chumbani bila wao kujua kama nilikuwa nawaona.

Nilikuwa nimesimama kwenye pembe moja ya chumba, nilisimama na wanawake wawili kati ya wale wanne walioingia. Kwangu hali hiyo niliiona ni ya kawaida na nilimshangaa mama alivyokuwa akilia.

Mama aliendelea kulia kwa uchungu huku akiwa anasogea mpaka pale kitandani na kuushika mwili wangu kama vile haamini kilichotokea. Nilitamani sana kumwambia mama kwamba sijafa, nipo hai kabisa na ni mzima wa afya lakini wale wanawake wawili wakanioneshea usinga kama walijua nataka kufanya nini.

Ghafla nilianza kutema mate hovyo huku nikijisikia vibaya. Nikabaini kila wale wanawake waliponinyoshea ule usinga nikawa kama zezeta na kutokwa mate mdomoni.

Basi wanakijiji karibu wote wakafika nyumbani na kujaa tele huku wakilia kwa kuomboleza kwamba mimi nilifariki dunia ghafla. Wengi walikuwa wakiulizana sababu ya mimi kufa ghafla bila kupata majibu.

Lakini wiki moja kabla ya kifo changu, kuna kijana mwingine pale kijijini alifariki dunia ghafla. Yeye alikuwa fundi seremala halafu kuna kijana mwingine aliyekuwa mwanafunzi aliyesifika kwa kuwa na akili nyingi sana katika kijiji kizima naye aliaga dunia katika mazingira ya utatautata.

Basi, msiba ulipamba moto nyumbani, watu walilia sana na usiku huohuo ndungu zangu walikaa kikao cha kujadili mazishi yangu yatakavyokuwa.

Baada ya vuta nikuvute ya muda mrefu, ndugu walikubaliana mwili wangu uzikwe palepale nyumbani tunapoishi lakini kwa nyuma. Hayo yote yalikuwa yakifanyika huku nikiwa pembeni yao nasikia kila kitu.

Kulipokucha, watu walizunguka nyumba na kuanza kuchimba kaburi huku waombolezaji wengi wakiwa wanasubiri muda wa kuaga mwili ufike na kukamilisha mazishi yangu.

Muda wa kuuaga mwili ulipofika waombolezaji walianza kilio upya. Si unajua mwandishi vipindi vya watu kulia msibani? Ni wakati wa taarifa, ndugu wanapofika kutoka mbali, kuuaga mwili, kuzika na kurudi kutoka makaburini.

Basi, mwili wangu wa bandia ulitolewa nje kisha ulifunuliwa kwa ajili ya watu kutoa heshima za mwisho kwangu.

Cha ajabu, mimi mwenyewe nilikuwa nauona mwili ule kwenye jeneza ni mgomba lakini waombolezaji walikuwa wanauona ni mwili wangu na kila aliyeufikia alikuwa akizidisha kilio, hasa wanawake.

Leave A Reply