The House of Favourite Newspapers

Ndugu Zangu Walinichukua Msukule-5

0

MSIMULIAJI: Obedi Masanja

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:

Waliposikia sauti yangu walikuwa wakipiga mayowe huku wakikimbia na kusema walinisikia kisha nikatoweka kimiujiza. Kuna siku nikiwa nakwenda nyumbani, niliwakuta marafiki zangu niliokuwa naishi nao  wakiogelea mtoni, nikaanza kuwaita kwa majina.

ENDELEA MWENYEWE…

Basi nilimwita mmoja wa marafiki zangu, anaitwa Esther. Nikamuuliza mbona nyie huku mnaishi maisha mazuri sana yaani hadi mnaoga wakati mimi hapa huwa siogi nateseka tu kule.

Nilipotamka maneno hayo hakuna aliyebaki pale wote walikimbia huku wakipiga kelele kuwa wamesikia sauti yangu na mimi nilipotea.

Siku nyingine nilikuwa nakwenda nyumbani nasogea mpaka kwenye mtungi wa maji ya kunywa maji au nakwenda kufunua katika vyungu na kula chakula kilichopikwa huku nikimwambia mama kuwa wao wanakula chakula kizuri sana kuliko hata mimi na hapo ilikuwa ikitoka sauti ya huzuni na kuwafanya watu wakimbie huku wakinitaja kuwa tumesikia sauti ya Obedi.

Ile hali iliendelea na kuna wakati nilikuwa nikitaka kula chakula cha nyumbani nakula kwanza halafu ndiyo naongea kwa sababu nisipokula wao wakisikia sauti yangu wanakimbia nje na kupiga mayowe.

 Kitendo hicho kilinifanya nishindwe kula, kwa sababu ya kelele wakawa wanatoka nje na kwenda kuwaambia majirani kuwa wanasikia sauti yangu niko hai sijafa wengine wakawa wanapinga na hiyo hali ndiyo ilisababisha mpaka nikapatikana.

Aliyesababisha nikapatikana ni mwenyekiti wa kijiji ambaye . nilikuwa karibu naye kwa sababu wakati nilipokuwa nyumbani nilikuwa nabadilishana naye mifugo kwa chakula.

Kwa hiyo tukawa na ng’ombe wengi. Naye mwenyekiti alikuwa na mifugo ya kutosha. Kwa hiyo wakati mwingine hata yule mchungaji tuliyekuwa tumemuweka kwa ajili ya kutuchungia mifugo yetu siku niliyokuwa nina nafasi nilikuwa namwambia apumzike mimi ndiyo naenda kuchunga na mwenyekiti sehemu moja.

Tulikuwa tunachanganya mifugo yetu kuanzia asubuhi hadi jioni, tunapiga stori mpaka akawa anasema kijiji kingekuwa na vijana watano kama mimi kungekuwa na mabadiliko makubwa.

Sasa, siku moja nilimtokea mwenyekiti akiwa anachunga, nikamwambia mwenyekiti tulikuwa tunachunga wote, sasa angalia wewe unaendelea kuchunga mimi sijui mifugo yangu ipo wapi na hapa nilipo sijitambui.

Mwenyekiti aliposikia sauti yangu alilala kwenye nyasi kama nyoka kisha akakimbia, mimi nilikuwa namuona lakini yeye hakuwa na uwezo huo.

Mtu akishachukuliwa msukule anakuwa kama zezeta lakini uwezo wake wa kuona au kufanya mambo ni mkubwa kuliko wa binadamu wa kawaida ambapo anaweza akaona lakini asionwe.

Mwenyekiti alikimbia sana, breki ya kwanza alikwenda kusimama nyumbani kwetu, akawaambia wazazi wangu kuwa ‘kumbe kijana wenu yupo hai, nawashangaa mnasikia ya watu mnadharau.’

Baada ya mwenyekiti kuongea na wanafamilia, kesho yake akaitisha mkutano wa hadhara kijijini, wakachagua wazee mashuhuri, wale waliokula chumvi nyingi. Wakasema wataunda kamati watafute fedha halafu  waende nchini Zaire kwa ajili ya kunitafuta kwa waganga wa kienyeji. Ni baada ya kugundua kuwa mimi nilikuwa na vijana wengine wa kijijini waliokufa kabla yangu.

 Kwenye mkutano huo, watu wengine wakasema ‘huyu kijana yupo hai tunasikia sauti yake mara kwa mara, atakuwa  amefichwa sehemu.’

Walichanga fedha, wakaangalia nyumbani kulikuwa na kiasi fulani, wakauza na mifugo iliyokuwepo na kijiji pia kikaongezea pesa wakachaguliwa baadhi ya wana kijiji ndipo safari ya kwenda Zaire ikaanza.

Walifikia sehemu moja inaitwa Lubumbashi. Na hapo mimi nilikuwa nasimuliwa baada ya kupatikana. Wakampata mtaalam huku msimamizi wa zoezi lile akiwa mwenyekiti wa kijiji na ndiye aliyekuwa anamfahamu vizuri mtaalam huyo.

Walimpa majina yangu, akaangalia kwenye ‘vipimo’ vyake na akakuta mimi nilikuwa kamili, yaani sikukatwa ulimi.

Wale wazee walioneshwa waziwazi na watu walionichukua msukule. Walikuwa ishirini na mbili, wakiwemo baadhi ya ndugu zangu niliokuwa naishi nao kijijini kwetu na waliokuwa wakiishi vijiji vya mbali.

Wakati zoezi lile likiendelea kule Zaire, kwenye ile ngome nilipokuwepo wakawa tayari wameshatambua kuwa, mimi natafutwa. Kwa sababu wenyewe wana kitengo cha ‘upelelezi’. Walivyopata taarifa kuwa natafutwa wakapanga wanihamishe.

Je, nini kiliendelea? Usikose kusoma wiki ijayo mkasa huu unaoitwa Ndugu Zangu Walinichukua Msukule.

Leave A Reply