Ndugu Zangu Walinichukua Msukule-6
ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:
WAKATI zoezi lile likiendelea kule Zaire, kwenye ile ngome niliyokuwepo wakawa tayari wameshatambua kuwa, mimi natafutwa. Kwa sababu wenyewe wana kitengo cha ‘upelelezi’. Walivyopata taarifa kuwa natafutwa wakapanga wanihamishe. SASA ENDELEA MWENYEWE…
Kufumba na kufumbua nilitolewa nje haraka sana kama ninayekimbizwa kutoka kwenye ajali au janga zito. Chapuchapu nikapandishwa kwenye ungo ambao wao kule wanautumia kama ndege ya angani ya abiria.Lakini kwa jinsi nilivyoona kwa macho yangu mimi nilibaini siyo ungo bali kilikuwa kile kisu cha kukunja kwa sababu ya kuficha makali ndiyo kwa macho ya kawaida kilionekana ni ungo.
Kisu hicho kwa chini kiliandikwa maneno fulani hivi ambayo kwa sasa siyakumbuki. Wale wahusika wakawa wanaongea maneno fulani ya kishirikina huku kile kisu kikiwa kinatanuka polepole na kuwa kama ungo wa kawaida wa majumbani.
Baada ya hapo mimi nikaoneshwa ishara ya kushika sehemu kwa mikono. Wakati huo dereva naye alikuwa ameshapanda kwenye ungo huo na kukaa kwenye nafasi yake tayari kwa safari.
Nilitamani sana kuuliza napelekwa wapi, lakini moyo wangu ulisita.
Baada ya dereva kupanda, wale wengine wakaongea tena maneno fulani, ungo ukaanza kunyanyuka kwenda angani huku na mimi nikiwemo. Ndiyo safari ikawa imeanza hivyo tena kwa kasi. Ilikuwa mara yangu ya kwanza kupanda ungo kwani nilikuwa nasikia tu kwamba wachawi hutumia ungo kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
Basi, tuliendelea kwenda mpaka ikafika hatua ungo ukawa unasuasua kuendelea na safari ile. Ukawa kama unataka kuanguka na dereva alikuwa mwendo kasi kiasi kwamba, ikafika mahali ‘trafiki’ wakamsimamisha.
Hapa naomba niseme kidogo tu kwamba, ninaposema trafiki ni kweli trafiki wanakuwepo kama hawa waliopo huku kwenye dunia yetu ya kawaida.
Tulivyosimamishwa, ikabidi dereva aoneshe ishara kuwa, alikuwa na dharura ndiyo maana alikuwa katika mwendo wa kasi kiasi kile. Trafiki akaridhia na utetezi huo wa dereva akaturuhusu, tukaendelea na safari. Lakini kule hatukuweza kuendelea moja kwa moja, nusura tuanguke sehemu moja ambayo ilishindikana kupita kwa ungo. Hatimaye dereva alishusha ungo chini.
Tukiwa chini, dereva kuna kitu alikionesha kwa chini mfano wa hirizi hivi. Ghafla ardhi ikaanza kuachana huku na kule. Ungo ukawa unaruka ukiwa mdogo kwa kupita humo mpaka kuibukia juu angani.Basi, dereva akawa ameliacha lile eneo hatarishi kwa mbali sana. Tukaenda mbele kidogo na baada ya muda tukawa tumekaribia kufika kwenye ile ngome ya pili.
Lakini tukiwa angani tulikuwa tunasikia sauti za watu wakipigana, zikitokea angani. Kumbe katika ngome ile kulikuwa na uchaguzi wa kumchagua mkuu wa ngome ile.
Tulivyofika kwenye ngome, tukawa tumefika na watu kama watatu hivi ambao walikuwa wanashuka baada kushindwa. Maana yake kila anayeshindwa anateremka mpaka atakaposhuka mtu wa mwisho ndiyo atakuwa amewashinda wote.
Sasa tulivyofika pale, dereva akaulizwa; ‘vipi mmeshammaliza?’ Kwa ishara tu alikuwa akimaanisha kunikata ulimi mimi, dereva akajibu; ‘ndiyo.’
Kwa kuwa yeye ni dereva hakuwa akijua kilichokuwa kinaendelea. Kwa hiyo ni kama alijibu tu. Basi, nikachukuliwa na kupelekwa katika kundi la watu waliokatwa ndimi zao.Maisha mapya yakaanza pale kwenye ngome nyingine.
ayakutofautiana na yale ya kwenye ngome ya kwanza kwani maisha yalikuwa yaleyale, hakukuwa na kilichobadilika.
Nilianza kuishi chini ya utawala wa kiongozi mpya aliyeshinda baada ya uchaguzi lakini wakati huo ndugu zangu waliokuwa Zaire kwa ajili ya kunitafuta walikuwa wakiendelea na zoezi hilo na baadaye mtaalam akagundua kuwa nilikuwa nimehamishiwa katika ngome nyingine ambayo haikujulikana haraka.
Ilimlazimu yule mtaalam aanze kunitafuta kwa kutumia ramani alizokuwa akizijua yeye mpaka akafanikiwa kujua sehemu niliyokuwa nimehamishiwa ambapo kulikuwa na ulinzi mkali uliokuwa umeimarishwa katika kila kona ya ngome hali iliyompa ugumu mtaalam kunitafuta.
Je, nini kiliendelea? Usikose kusoma wiki ijayo mkasa huu unaoitwa Ndugu Zangu Walinichukua Msukule.