NEC; aliyetimiza masharti asizuiwe kupiga kura

lubuva1.jpgMwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva

Mungu ni mwema, ndivyo ninavyoanza kusema katika makala haya, tumshukuru kwa amani tuliyonayo nchini hasa wakati huu tunapoelekea kwenye uchaguzi mkuu.

Nchi nzima ipo katika mchakato wa kuwapata viongozi kwa njia ya kura kwa nafasi mbalimbali za kisiasa kupitia vyama vyao vya siasa, wakati hayo yakiendelea kumekuwepo na taarifa za mchakato huo kufanyika katika hali ya amani na utulivu katika maeneo mengi nchini, isipokuwa machache.

Vyama vingi hivi sasa vina wagombea wake katika ngazi za urais udiwani, ubunge na uwakilishi.

Vyama vyote kwa kiwango kikubwa vimefanikiwa kuwachuja na kuwapata wagombea wao katika maeneo mengi nchini na wadadisi wa masuala ya kisiasa wameeleza kuwepo kwa ishara ya kukua kwa demokrasia ndani ya vyama hivyo na kwa mara ya kwanza tukashuhudia  idadi kubwa ya wanachama waliojitokeza kugombea nafasi za uongozi.

Mbali ya sifa hiyo, pia katika maeneo kulikofanyika kampeni za wagombea mbalimbali, kumeripotiwa kuwepo kwa hali ya amani na utulivu, licha ya kuwepo kwa idadi kubwa ya watu wanaojitokeza kusikiliza sera za vyama wakati wagombea wakipeperusha bendera za vyama vyao kwenye mikutano ya hadhara wanayofanya.

Hali kama hiyo imeripotiwa kujitokeza kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ACT-Wazalendo, Chama cha Wananchi (CUF), Chama cha NCCR-Mageuzi na vingine vingi ambavyo vimepata wagombea wake maeneo mengi nchini katika hali ya utulivu.

Kitendo hicho cha vyama vya siasa nchini kukamilisha kuwapata wagombea wao katika hali ya amani na utulivu na kuingia kwenye kampeni kwa zaidi ya mwenzi mmoja sasa ni kitendo kinachopaswa kuungwa mkono na Watanzania wote kwani kinaashiria mwanzo mzuri wa kufanyika uchaguzi mkuu kwa amani.

Ingawa vipo viashiria vingine vinavyotajwa na wadadisi wa masuala ya kisiasa kwamba vinaweza kusababisha uchaguzi mkuu usiwe huru na wa haki, na hivyo kuashiria uwezekano wa kutoweka kwa amani na utulivu ikiwemo suala la uandikishaji wapiga kura katika mashine za Biometric Voters Registration (BVR), lakini hatua ya kampeni kufanyika kwa amani huku wasikilizaji wa sera wakiwa wengi kwenye mikutano ya vyama vyote vikubwa, ni jambo linalotia moyo.

Kwa hali hiyo basi ni jukumu la Watanzania kwa makusudi kuanza kuunga mkono jitihada au vitendo vyovyote vinavyotoa dira ya uchaguzi mkuu ujao kuwa na utulivu ili kuchochea mazingira ya amani kupanuka zaidi na kupinga vitendo au viashiria vya kusababisha amani kupotea.

Kama historia inavyosema; Tanzania ni miongoni mwa nchi chache sana barani Afrika ambayo imekuwa inafanikisha chaguzi zake katika hali ya amani na utulivu licha ya kuripotiwa kwa baadhi ya matukio ya vurugu katika maeneo machache.

Mara zote imekuwa ni aghalabu sana kuona rais, diwani au mbunge wa Tanzania ameingia madarakani kwa kumwaga damu za watu kama inavyotokea kwa baadhi ya nchi barani Afrika na nje ya bara hili.

Kwa mantiki hiyo, basi ni lazima Watanzania kwa umoja wao wakaungana pamoja katika kuhakikisha kuwa wanaziba mianya inayoashiria kuzuka kwa vurugu katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, ili kulifanya taifa letu kuendelea kusifika duniani kote kuwa ni kisiwa cha amani na utulivu.

Niiombe Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) chini ya Jaji Damian Lubuva, kutumia vyombo vya habari kuelimisha wapiga kura taratibu zitakavyokuwa siku ya kupiga kura hasa tukizingatia kuwa kutokana na foleni kuwa ndefu wakati wa kuandikisha wapiga kura, baadhi ya watu walijiandikisha sehemu ambazo siyo makazi yao. Kifupi ni kwamba Nec ihakikishe kila mwenye shahada halali ya kupigia kura siku hiyo, Oktoba 25, mwaka huu anapiga kura.

Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.


Loading...

Toa comment